Jumanne, 12 Aprili 2016

Mambo Yanayosababisha Mtu Kuwa na Uwezo Mdogo Kiakili


Katika utafiti ulioongozwa na profesa wa saikolojia, Thomas Joseph Bouchard na kuchapishwa katika jarida la Intelligence, toleo la 35 la mwaka 2007, ilibainika kuwa karibu nusu ya uwezo wa akili unatokana na urithi wa vinasaba.

Utafiti uliofanywa kati ya Oktoba 21 na Novemba mosi, 2013 na Taasisi ya Utafiti ya Triangle (RTI) kuhusu uwezo wa watoto kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la pili nchini, ulibaini kuwa asilimia 92 ya wanafunzi hawaelewi wanachokisoma.

Utafiti huo unaonyesha kuwa wanafunzi wengi wana uwezo mdogo wa kujibu maswali kwa sababu ubongo wao hauna ule uwezo wa kimaarifa katika kuchanganua mambo bali wanakariri tu.

Ubongo wao unaweza ukawa umekariri jambo lakini kwa
vile swali halipo moja kwa moja hushindwa kuoanisha majibu aliyo nayo na swali aliloulizwa ambalo liko kimtego zaidi.

Akizungumza katika kongamano la wazi kuhusu stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika lililofanyika Dar es Salaam, Aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Katka serikali ya awamu ya tano Dk Shukuru Kawambwa alisema “upimaji huu ulifanyika katika halmashauri 20, shule 200 na kwa wanafunzi 2,214 wa darasa la pili na ulitumia zana zilizojaribiwa na kuthibitishwa kimataifa tathmini ya awali ya kusoma (EGRA) na tathmini ya awali ya kuhesabu (EGMA).

Hali hii inaonyesha picha ndogo tu ya hali halisi ilivyo kuhusu uwezo wa kiakili wa kuelewa, kubuni, kujifunza pamoja na kufundisha mambo yalivyo katika ngazi mbalimbali za kupata maarifa hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine, tafiti mbalimbali za kisayansi zinaonyesha baadhi ya sababu zinazoathiri uwezo wa kiakili kwa watoto na hata baadaye wanapokuwa katika umri wa utu uzima.

Kimsingi ubongo wa binadamu hukua kwa haraka wakati mtoto anapokuwa tumboni hadi miaka minne na kufikia kiasi cha asilimia 90 ya ubongo wa mtu mzima.

Kipindi hiki ni muhimu sana kwa ajili ya ubongo kuwa na akili nzuri na uwezo mkubwa wa kujifunza na kubuni mambo kama inavyofahamika kitaalamu IQ kwa tafsiri ya Kiingereza ni Intelligence Quotient.

Chochote kinachodhuru ubongo katika kipindi cha utotoni hupunguza na hata kuathiri uwezo wa akili na ubunifu katika maisha yake yote.

Baadhi ya watafiti wanaamini kuwa akili za mtu hutokana na vinasaba vya urithi kwa kati ya asilimia 40 hadi 50 na asilimia zinazobaki, huchangiwa na mazingira ya nje.

Robert Crooks na Jean Stein waliandika kitabu cha saikolojia kuhusu tabia na maisha, walichokipa jina Psychology: Science, behavior and life, wanasema kuwa wazazi wenye uwezo mkubwa wa kuelewa mambo mara nyingi huzaa watoto wenye uwezo mkubwa wa kiakili pia.

Katika utafiti ulioongozwa na profesa wa saikolojia, Thomas Joseph Bouchard na kuchapishwa katika jarida la Intelligence, toleo la 35 la mwaka 2007, ilibainika kuwa karibu nusu ya uwezo wa akili unatokana na urithi wa vinasaba.

Utafiti huo uliwahusisha pacha wanaofanana na wasiofanana na ikabainika kuwa wale wanaofanana uwezo wao wa kiakili unafanana kwa asilimia 85 na wasiofanana ni kwa asilimia 60.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa kati ya mwaka 2008 na 2013 na watafiti wa Chuo Kikuu cha Granada cha Uhispania na kuongozwa na Dk Cristina Campoy, nao ulibaini kuwa uwezo wa kiakili wa mtoto wa kuelewa na kubuni mambo, hutegemea kwa kiasi kikubwa hali ya lishe ya mama yake kabla mtoto hajazaliwa na lishe ya mtoto mchanga katika kipindi cha awali baada ya kuzaliwa.

Katika utafiti mwingine uliofanywa na Mandy B. Belfort na wenzake kati ya mwaka 1999 na 2002 na kuchapishwa katika Jarida la JAMA Pediatrics toleo la Julai 2013, ilibainika kuwa watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita na kupewa lishe nzuri pamoja na kunyonya kwa kipindi kirefu wakati wa utoto, wanakuwa na akili nyingi hata wakati wa utu uzima.

Utafiti huo unaongeza kusema kuwa maziwa ya mama hasa anapokula kwa wingi samaki wasiokuwa na sumu ya mercury, yanakuwa na viini lishe aina ya ‘N-3 fatty acid docosahexaenoic acid (DHA)’ ambavyo ni muhimu kwa afya ya ubongo na hufanya mtoto kuwa na akili nyingi.

Dk Elifatio Towo wa hapa nchini, anasema kuwa maziwa ya mama yana mchango mkubwa katika ukuaji wa akili ya mtoto.

Anaongeza kusema kuwa pale mtoto anapokosa maziwa ya mama ukuaji wa ubongo wake huathirika.
“Hali hiyo inaathiri ubongo kwenye sehemu ijulikanayo kama ‘Cognition centre’ na kumuathiri mtoto katika uwezo wa kufikiri haraka,” anasema Dk Towo katika moja ya makala yaliyochapishwa katika gazeti hili la Mwananchi, Julai 11, 2014.

Tafiti nyingine zinaonyesha kuwa upungufu wa madini joto katika chakula, matumizi ya pombe, dawa za kulevya na matumizi holela ya dawa za hospitalini wakati wa ujauzito, yanaweza kuathiri uwezo wa kiakili kwa mtoto pindi atakapozaliwa.

Tatizo jingine linaloathiri akili za watoto ni sumu ya zebaki inayopatikana katika maji ya kunywa na mazingira kutokana na uchafuzi unaofanywa na wachimbaji wa madini.

Sumu ya risasi pia inahusika kwa kiasi kikubwa na kupungua kwa uwezo wa akili hasa kwa watoto.
Utafiti wa Baghurst na wenzake wa mwaka 1992, unaonyesha kuwa watoto wanaokutana na sumu ya risasi katika mazingira wanayokaa, hupungukiwa na uwezo wa kiakili.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), pia zinaonyesha kuwa risasi huathiri uwezo wa kiakili wa watoto takriban 600,000 kila mwaka.

Takwimu zinaongeza kusema kuwa asilimia 99 ya waathirika wa sumu ya risasi, wanaishi katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa mojawapo.

Utafiti wa afya ya watoto uliofanywa na Mary Azayo, Karim Manji na Festus Kalokola wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) na kuchapishwa mwaka 2008 na Oxiford University Press, ulibaini kuwa asilimia 10 ya kinamama wanaojifungua katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wana kiwango kikubwa cha sumu ya risasi katika damu inayosafirisha viinilishe kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Katika utafiti wa ‘Global Study on Lead in Paint’ uliofanywa mwaka 2009 na Toxics link, IPEN pamoja na shirika lisilo la kiserikali la AGENDA ilibainika kuwa sampuli 19 kati ya 20 za rangi ya mafuta ya kupaka majumbani, zilikuwa na madini ya risasi zaidi ya asilimia 0.045 (450 parts per million) zaidi ya kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Taifa la Kudhibiti Ubora (TBS).

Akizungumzia hali ya uwepo wa madini ya risasi, matibu mkuu wa AGENDA, Silvani Mng`anya anasema kuwa rangi zenye lead bado zipo Tanzania na zinapatikana sokoni.

Mtandao wa Environmental Expert katika tovuti yake unasema kwamba madini haya yenye sumu, yanaweza kupatikana pia katika baadhi ya vifaa vya watoto vya kuchezea kama vile madoli.

Risasi inapopatikana katika mazingira ya nyumbani na shuleni, inaweza kuwaathiri kirahisi kinamama wajawazito na watoto wanaosoma.

Watafiti pia wanahusisha hali ya afya ya mwili na uwezo wa kiakili. Watoto wanaoumwa mara kwa mara uwezo wao wa kiakili hupungua kwa kiasi kikubwa.

Tatizo huwa kubwa zaidi pale magonjwa ya mtoto yanapohusisha ubongo kama vile malaria inayopanda kichwani, homa ya uti wa mgongo, masikio kutoa usaha, kichwa kujaa maji na kifafa.

Watoto wanaozaliwa kwa shida hasa wasichana wadogo katika uzazi pingamizi baada ya mama kukaa na uchungu kwa muda mrefu ni tatizo linalochangia uwezo mdogo wa akili.

Tatizo linalowakumba watoto wanaochelewa kuzaliwa ni seli za ubongo kukosa hewa ya oksijeni kwa muda mrefu au kuumia wakati wanazaliwa.

Tatizo la namna hiyo huwatokea wasichana wadogo, chini ya miaka 20, wanaopata mimba. Tafiti nyingi za afya ya jamii zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya wanawake wanaojifungua kwa mara ya kwanza katika nchi za Afrika, ni wasichana wadogo wenye umri chini ya miaka 18.

Wataalamu wa afya pia wanasema kuwa kupata vipigo na ajali zinazohusisha kichwa, kunaweza kuathiri afya ya ubongo na uwezo wa kiakili kwa mtoto.

Tafiti nyingine zinathibitisha kuwa kuna vitu ambavyo huweza kuathiri ubongo na kusababisha uwezo mdogo wa akili.

Vitu hivyo ni kama vile ajali za barabarani, kunywa sumu, majeraha ya kupigana na kuungua moto. Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Whitley E. wa Taasisi ya Karolinska, akishirikiana na wenzake nchini Sweden na kuchapishwa katika jarida la Epidemiology and Community Health Mei, 2010.

Watoto wasiopata usingizi wa kutosha pia hupata athari za kiakili zinazopunguza uwezo wao wa kuelewa na kubuni mambo.

Watoto wenye msongo wa mawazo kwa mujibu wa watafiti, uwezo wao wa kiakili katika kipimo cha IQ, hupungua kwa asilimia 13 ikilinganishwa na wenzao wasiokuwa na msongo.
Wakithibitisha kwenye utafiti wao, Profesa Lilian Rosenbaum na Bernard Brown wa Chuo kikuu cha Georgetown walinukuliwa na gazeti la The Argus-Press la Marekani (1983) kuwa msongo wa mawazo huathiri mtoto katika uwezo wa kufikiri.

Jambo jingine linalohusishwa na uwezo mdogo wa kiakili ni hali ya umaskini wa wazazi uliokithiri.
Wahlsten D. alifanya utafiti mwaka 1995 na kuuchapisha katika jarida la ‘The Alberta Journal of Educational Research’ akisema kuwa uwezo wa kiakili wa mtoto anayeishi katika umaskini mkubwa unaweza kuongezeka kwa asilimika 16 kama hatawekwa katika mazingira bora zaidi.

Naye Eric Jensen katika kitabu chake kiitwacho ‘Teaching with Poverty in Mind’ anasema kuwa umaskini unaathiri kwa kiasi kikubwa nguvu na uwezo wa akili wa kuelewa, kutambua na kubuni mambo.
Jensen anasema kuwa uwezo mdogo wa kiakili ni mwitikio kwa hali sugu na ya muda mrefu ya umaskini. 

Hata hivyo, Jensen anasema kuwa licha ya matatizo hayo, uzuri ni kwamba uwezo wa akili ya mtu huweza kubadilika.

“Habari njema ni kwamba, bongo zetu zimeumbwa na uwezo wa kubadilika… Ili mtu afanye vizuri katika masomo, ubongo unatumia mfumo wa kujiendesha unaohusisha neva za ufahamu zinazomwezesha mwanafunzi kuwa makini, kufanya kazi kwa bidii, kuchanganua na kupangilia maudhui pamoja na kufikiri kwa kina,” anasema Jensen.

Watu wengine huamini kwamba watu weupe wana akili nyingi zaidi na ndiyo maana nchi zao zimeendelea na wamekuwa wakipiga hatua mbele ukilinganisha na Waafrika ambao wana rasilimali nyingi lakini wanashindwa kuzitumia kutajirika.

Richard T. Schaefer aliandika kitabu cha elimu ya mwenendo wa asili ya jamii, alichokiita ‘Encyclopedia of Race, Ethnicity and Society’ na kubainisha kuwa uwezo wa kiakili hautokani na matabaka ya rangi; mfano weusi na weupe.

Lakini akasema wanasayansi wengi wanaamini kuwa fikra zinazojenga jamii za matabaka haya na tofauti zao kijamii, zinaweza kuwa chanzo cha tofauti zinazoonekana katika uwezo wa kiakili na ubunifu katika jamii zao.

Wiki ijayo makala haya yataendelea kuuchanganua ubongo na safari hii itakufunza namna ya kukuza akili hata kwa wale ambao wameathirika na sasa wana uwezo mdogo wa kufikiri.

0 comments: