Haya ni magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa
mwingine kupitia vitendo vya ngono. Vitendo hivi vya ngono vinaweza kuwa
kujamiana, kubusiana, vitendo vya ngono kwa kutumia mdomo (oral-
genital sex), kujamiana kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) iwe kwa
mwanamume na mwanamke au kati ya wanaume wenyewe na
hata wale wanaotumia
vifaa vya kufanyia ngono (vibrators).Kuna aina nyingi za magonjwa ya zinaa kama:-
- Kisonono (Gonorrhoea)
- Chlamydia
- Kaswende (Syphillis)
- Trichomoniasis,
- Pangusa(Chancroid)
- genital herpes
- genital warts.
- nk.
KISONONO (Gonorrhoea) au "Gono" kama wengi wanavyopenda kuuita kwa kifupi. Kisono ni ugonjwa kati ya magonjwa ya zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Neisseria gonorrhoeae, bakteria ambao hukua na kuzaliana kwa haraka katika sehemu zenye unyevunyevu na joto mwilini kama kwenye shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mirija ya kupitisha mkojo au mbegu za kiume (urethra), mdomoni na kwenye puru au rectum. Maambukizi mengi kwa wanawake hutokea kwenye shingo ya kizazi
Ugonjwa huu huambukizwa kupitia vitendo vya ngono kutoka kwa mtu aliye na ugonjwa huu utakapojamiiana naye bila kutumia kondomu. Pia mama mjamzito mwenye kisonono anaweza kumuambukiza mwanaye wakati wa kujifungua.
Dalili za ugonjwa huo huanza kujitokeza kuanzia siku ya 2 hadi ya 7 baada ya mtu kupata maambukizi ya ugonjwa huo na huweza kuchelewa kuonyesha dalili hasa kwa wanawake. Dalili za ugonjwa huo ni kama zifuatazo:-
Kwa wanaume ugonjwa wa kisonono:-
- husababisha kuhisi kama kichomi wakati wa kukojoa (burning sensation).
- kutokwa na majimaji ya njano, meupe au ya kijani kwenye uume yanayoambatana na maumivu makali sana.
- wakati mwingine kuhisi maumivu au kuvimba kwa korodani (swollen testicles).
- kuhisi maumivu au kuhisi kichomi wakati wa kukojoa,
- kuongezeka kutokwa majimaji ukeni, majimaji ambayo ni ya njano au yaliyochanganyika na damu.
- kutokwa damu kabla ya hedhi kufikia wakati wake wa kawaida,
- kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa,
- kuhisi kichefuchefu,
- homa na kutapika.
Kumbuka
Kondomu au mipira ya kiume husaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama gono, chlamydia na kadhalika lakini sio kinga muafaka ya magonjwa ya zinaa kama vile kaswende, genital herpes na genital warts.
KASWENDE
Utangulizi.
Ugonjwa wa kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum. Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayoongoza kwa kusababisha madhara mengi. Maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito huleta madhara mengi sana kama vile kujifungua kiumbe ambacho kimeshakufa, mtoto kuathirika na ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa, mtoto kupata matatizo wakati wa ukuaji wake, degedege na kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga. Ugonjwa wa kaswende huathiri zaidi ya mimba milioni moja duniani kote kila mwaka na kuchangia theluthi mbili ya vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa tayari wameshakufa katika nchi za maeneo ya chini ya Jangwa la Sahara. Asilimia 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto kufariki wakati wa kuzaliwa. Pia asilimia nyingine 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende husababisha watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu kupata matatizo ya ukuaji, degedege na kuongezeka vifo vya watoto kwa asilimia 50.
Magonjwa ya Ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana pamoja ambapo pia ugonjwa wa zinaa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu kupata Ukimwi.
Je, ugonjwa wa kaswende huambukizwa kwa njia gani?
Kama tulivyosema
awali, kaswende husababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum.
Njia za maambukizi za ugonjwa huu ni kama zifuatavyo:1) Kupitia kujamiana bila kutumia kinga au ngono zembe na mtu aliyeambukizwa kaswende.
2) Mama aliyepata ugonjwa wa kaswende wakati wa ujauzito anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito.
3) Kuambukizwa kupitia michibuko au mipasuko kwenye ngozi wakati wa kujamiana au wakati mwingine pale mtu anapogusana na mtu mwenye kaswende ikiwa wote wawili wana mipasuko kwenye sehemu mbalimbali za ngozi zao.
Sio rahisi mtu kutambua kama ana michibuko au la kwenye ngozi kwani mingine huwa midogo sana isipokuwa ile inayoweza kuonekana kwa macho, lakini huweza kuwa njia ya maambukizo. Baada ya kujua visababishi vya ugonjwa huo sasa tuzibainishe pia dalili zake.
Dalili na viashiria vya ugonjwa wa kaswende hutegemea aina ya ugonjwa wa kaswende wenyewe. Kuna aina tano za ugonjwa wa kaswende ambazo ni;
- Ugonjwa wa kaswende wa awali (Primary syphilis)
- Ugonjwa wa kaswende wa pili (Secondary syphillis)
- Kaswende iliyojificha (Latent syphilis)
- Kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis)
- Kaswende ya kurithi (Congenital syphilis)
Dalili ya kwanza ya aina hii ya kaswende ni kutokea kwa kidonda kidogo cha mviringo (chancre kama kinavyojulikana kitaalamu) katika sehemu ambayo bakteria wameingilia na hutokea kati ya siku 10 hadi miezi mitatu (kwa kawaida kuanzia wiki 2 hadi 6) baada ya mtu kupata maambukizi. Kidonda hiki kinaweza kutokea kwenye sehemu ya haja kubwa, shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mdomoni, katika uume, ulimi, vulva, tupu ya mwanamke na sehemu nyinginezo mwilini. Tezi (lymph nodes) ambazo zipo karibu na sehemu iliyotokea kidonda hiki kawaida huwa zinavimba baada ya siku 7 hadi 10. Kidonda hiki hakiambatani na maumivu na kwa kuwa kinaweza kutokea katika sehemu zilizojificha kama kwenye shingo ya kizazi, sio rahisi mtu kutambua kama ana aina hii ya kaswende. Kidonda hiki kinaweza kuwepo kwa muda wa wiki 3 hadi 6 kama mtu hatapata matibabu na hutoweka chenyewe bila tiba au baada ya kupata tiba. Robo tatu ya wale ambao hawapati tiba huishia kuingia kwenye kundi la kaswende ya aina ya pili yaani.
Secondary syphilis.
Aina hii hutokea wiki 4 hadi 10 baada ya mtu kupata kaswende ya awali. Dalili za aina hii ya kaswende ni: vipele ambavyo haviwashi katika viganja vya mikono au nyayo za miguu. Vipele hivi pia vinaweza kutokea mwili mzima au sehemu mbalimbali za mwili. Pia muathirika huhisi uchovu, kuumwa kichwa, homa, kunyofoka nywele, vidonda vya koo, kuvimba kwa matezi mwili mzima, maumivu ya mifupa na kupungua uzito. Kaswende ya aina hii hujitokeza kwa wiki kadhaa na hutoweka hata bila kupata tiba kwa mtu aliyeathirika. Pia inaweza kujirudia rudia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili na mtu huingia kwenye kundi la aina ya tatu ya ugonjwa wa kaswende yaani (latent syphilis) baada ya miaka miwili.
Latent syphilis.
Aina hii inajulikana kama kaswende ambayo inaweza kuthibitika tu kwa kutumia vipimo vya maabara (serological test) na imegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni kaswende iliyojificha ya awali au (Early latent syphilis) kwa kimombo.
Early latent syphilis
Hii ni kaswende ambayo hutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya muathirika kuugua kaswende aina ya pili .Aina hii huwa na dalili zinazojirudia kama za kaswende ya pili. Kundi la pili ni kaswende iliyojificha ya kuchelewa au Late latent syphilis.
Late latent syphilis.
Hii hutokea baada ya mwaka mmoja wa kuugua kaswende ya aina ya pili (secondary syphilis). Wakati wa kuugua aina hii ya kaswende, muathirika huwa hana dalili wala viashiria vyovyote vile na uwezo wake wa kuambukiza mtu mwingine huwa chini au hawezi kabisa kumuambukiza ugonjwa huu mtu mwingine. Kaswende ya aina ya nne kama tulivyosema inaitwakaswende ya baadaye (Tertiary syphilis).
Tertiary syphilis
Asilimia 30 ya wagonjwa wa kaswende ambao hawakupata tiba hapo awali huingia kwenye kundi hili na hutokea miaka 15 hadi 30 baada ya maambukizi ya kaswende. Aina hii inaweza kuathiri viungo kama macho, ubongo, mishipa ya fahamu, viunganishi vya mifupa au joints, uti wa mgongo, moyo na mishipa ya damu. Kwa ajili hiyo aina hii ya kaswende ni yenye madhara makubwa kwani huweza kusababisha upofu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya akili na magonjwa ya mishipa ya fahamu. Huweza kumfanya mtu kuwa kiziwi na kupungukiwa na kumbukumbu na hata kumsababishia kifo. Pia aina hii ya kaswende inaweza kuathiri mfumo wa chakula, mfumo wa kupumua na mfumo wa uzazi. Aina ya mwisho ni ya kurithi (Congenital syphilis).
Congenital syphilis
Aina hii ya kaswende hutokea wakati wa ujauzito au baada ya mtoto kuzaliwa. Nusu ya wototo wanaozaliwa huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huu. Nusu ya watoto wenye maambukizi ya kaswende hufariki dunia muda mfupi kabla ya kuzaliwa au baada ya kuzaliwa. Dalili za aina hii ya kaswende kwa mtoto mchanga zinaweza kutokea baada ya kuzaliwa au wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa. Dalili hizo ni, kutoongezeka uzito au kushindwa kukua, homa, kukasirika haraka, kutochongoka kwa pua yaani pua linakuwa bapa, vipele kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo ambavyo huwa ni vipele vya rangi ya madini ya shaba kwenye uso, viganja vya mikono na nyayo na vipele kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa. Dalili nyingine ni kutokwa na majimaji puani, kuongezeka ukubwa wa ini na bandama, ngozi kuwa ya njano, na upungufu wa damu mwilini (anemia).
TRICHOMONASI
Trichomonasi husababishwa na
maambukizi ya protozoa anayefahamika kisayansi kama Trichomonas vaginalis.
Ugonjwa huu husababisha muwasho na karaha katika uke kwa wanawake na katika
mfereji wa mkojo kwa wanaume. Trichomonasi huweza kutibiwa kwa urahisi na
antibiotiki.
MALENGELENGE
(genital herpes)
Ugonjwa wa malemgelenge katika
sehemu za siri husababishwa na maambukizi ya herpes simplex virus(HSV).
Aina nyingi za malengelenge huwa ni kutokana na aina ya pili ya HSV (HSV
type 2). hata hivyo, maambukizi kutokana na aina ya kwanza ya HSV (HSV
type 1) nayo yapo. Malengelenge katika sehemu za siri husababisha vivimbe
vinavyouma vinavyojirudia kila mara, ingawa mara nyingi ugonjwa huwa hauonyeshi
dalili kwa muda mrefu. Upimaji wa damu huweza kuonyesha uwepo wa maambukizi ya
HSV, hata kama mtu bado hajaanza kuonyesha dalili. Dalili za HSV zinaweza
kutibika kwa kutumia madawa yanayopambana na virusi kama vile acyclovir,
lakini HSV hawawezi kutoka katika mwili - hawatibiki.
DUTU
(genital warts)
Dutu huota katika uume na
katika eneo la kuzunguka uke na mkunduni. Husababishwa na kundi la virusi
lifahamikalo kama human papillomavirus (HPV) ambao husambazwa wakati wa
kujamiiana. Dutu zinaweza kutibiwa na kuondolewa kwa upasuaji mdogo. Aina
fulani ya HPV ambao husababisha maambukizi katika sehemu za siri wanaweza pia
kusababisha kansa ya mlango wa uzazi (cervical cancer)
Kuzuia
na kudhibiti maambukizi
Tofauti na magonjwa mengine hatari,
hatua rahisi zinaweza kutumika kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa.
Hatua ambaYo ni madhubuti kuliko
zote ni kuepuka ngono kabisa. Bila ya kukutana kimwili hakuna uwezekano wa
kupata maambukizi ya zinaa.
Kuwa na mwenzi mmoja tu katika ndoa
na kwa wale wanaojiingiza katika mahusiano pia husaidia kupunguza hatari ya
maambukizi.
Kondomu inakinga dhidi ya maambukizi
hayo lakini si kinga kamili kwa asilimia mia moja. Kondomu huvaliwa kwenye uume
au kwenye uke na huwa kama kizuizi kwa vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya
zinaa. Hata hivyo kondomu huwa haifuniki sehemu yote ya siri ambayo hukutana
wakati wa kufanya ngono, na uwezekano wa kupata maambukizi ya zinaa bado upo,
hasa malengelenge.
Uchunguzi wa awali na matibabu
kamili huzuia madhara zaidi ya maambukizi ya zinaa; wakati huohuo huzuia
uambukizaji kati ya mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hii ni muhimu sana kwa
magonjwa ya zinaa ambayo huwa hayaonyeshi dalili, kwa sababu wale
walioambukizwa huwa hawajui kuwa wana hatari ya kuwaambukiza wenzi wao.
Matibabu yote lazima yafuatwe hata
kama matumizi ya awali ya dawa yalipelekea dalili zote kutoweka. Maambukizi
yanaweza kuendelea bila ya kuwa na dalili na hivyo kupelekea aliyeambukizwa
bila kujua kusambaza ugonjwa.
Chanzo: Maarifa Ya Jamii
0 comments:
Chapisha Maoni