Jumanne, 29 Machi 2016

Ubinafsi Unazuia Maisha Ya Furaha



UBINAFSI.
Ubinafsi hasa ule wa kujifikiria sisi wenyewe pekee ndio kikwazo kikubwa kwetu kuwa na maisha ya furaha. Na hapa hatuzungumzii ule ubinafsi wa mali pekee, maana hili tu ndilo tunaloelewa kuhusu ubinafsi.

Ubinafsi wa mali unatunyima furaha, ila kuna ule ubinafsi wa kujifikiria sisi wenyewe tu, ule wa kuona maisha yetu pekee ndiyo yenye umuhimu na kuona kile tunachotaka sisi ndiyo kinachotakiwa kuwa.

Ubinafsi huu ni ule wa kujiona kwamba wewe upo katikati ya dunia na kila kitu inabidi kiende kwa mapenzi yako wewe. Inapotokea kitu kinakwenda tofauti na ulivyopanga au ulivyotegemea basi unaumia sana na kuona maisha kama hayakufanyii usawa kwa upande wako.

Huu ni ubinafsi mgumu sana kuutambua kama hutaweza kuuchimba kwa ndani. Kwa sababu huu unakuwa umejengeka ndani kabisa na unaweza kuona ni maisha ya kawaida.
Kwa ubinafsi huu kitu pekee ambacho mtu anaona ni muhimu ni kile kinachomhusu yeye. Kile kinachohusu mwili wake, mawazo yake, mipango yake ni vingine vinavyomhusu yeye. Na hata katika mawazo au maongezi yanakuwa yametawaliwa na mimi.

Kwa ubinafsi huu, linapotokea jambo ambalo liko tofauti na mtu alivyotegemea, basi mtu huyu hutaka dunia nzima isimame ili tatizo lake litatuliwe kwanza.

Huyu ni yule mtu ambaye hajawahi kuwasiliana na wewe, ila anakupigia simu akiwa na shida na anataka wewe uache kila unachokifanya umtatulie tatizo lake. Hajali kwamba wewe ulikuwa na mambo yako mengine unafanya, anataka umtatulie tatizo lake sasa, na ukishindwa kufanya hivyo lawama zote analeta kwako. Au huenda wewe ndiye mtu wa aina hiyo, unakuwa na shida na unataka kila mtu aache kile anachofanya aje kwenye shida yako, hata kama hana msaada mkubwa anaoweza kutoa. Na wakati huo huo wewe sio msaada mzuri kwa watu wengine.

Ubinafsi wa aina hii umekuwa unawanyima furaha wale wenye nao. Kwa sababu kama wote tunavyojua, hakuna kitu kinachoweza kwenda kama wewe unavyotaka, kuna mambo mengi sana ambayo yanaingilia kati kati. Na hata unapokuwa kwenye matatizo, siyo kila unayemwomba msaada atakusaidia. Unatakiwa kuelewa hilo ili unapopata msaada ushukuru na unapokosa ujue ni jambo linaloweza kutokea pia. Kwa kuwa mbinafsi kwanza utaona lililotokea halikupaswa kutokea kwako, na hata baada ya kutokea basi walishindwa kukusaidia ni maadui kwako na hawakupendi, bila ya kujali na wao walikuwa wanapitia nini.

Kwa kujifikiria wewe pekee unakosa nafasi ya kipekee ya kujifunza kupitia changamoto zako mwenyewe na za wengine pia. Unapojiona wewe pekee ndiyo muhimu unakosa mahusiano mazuri na wengine, na haya yote yanapelekea maisha kuwa ya hovyo na kukosa furaha.

Ili kuondokana na ubinafsi huu unahitaji kuacha kujifikiria wewe mwenyewe tu, anza kuwaona na wengine pia ni muhimu, jua ya kwamba mambo mabaya yanatokea kwa kila mtu na siyo kwako tu. Na pia jua kila mtu anapitia mambo magumu kama unavyopitia wewe na hivyo siyo wote wanaweza kukusaidia unapokuwa kwenye mambo magumu.

Jua ya kwamba wewe ni sehemu ndogo ya umoja wa dunia ambao ni mkubwa sana. Wewe peke yako huwezi kuikamilisha dunia na hivyo unawahitaji wengine. Unapoacha kujijali wewe mwenyewe sana, utaanza kuona maisha ya wengine nayo ni muhimu na kuangalia mchango unaoweza kutoa kwenye maisha ya wengine. Kwa njia hii utakuwa na mchango bora kwa wengine na wao kuwa na mchango bora kwako na hatimaye wote kuwa na maisha bora.

Hakuna kitu chochote ambacho kinatokea kwako tu, vitu vinatokea kwa kila mtu, ukianza kuangalia maisha ya wengine pia utaona kile unachopitia ndicho ambacho kila mtu anapitia kwa wakati wake na namba yake.

Tufanyie kazi haya tunayojifunza kwenye falsafa mpya ya maisha ili tuweze kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa na yenye furaha.

Kila kitu kinaanza na sisi, lakini ni lazima tuepuke ubinafsi kutukosesha nafasi ya kuiona picha halisi ya dunia na maisha ambayo kila mmoja wetu anapitia.

0 comments: