Jumatatu, 28 Machi 2016

Anga Ndiyo Ukomo wa Mafanikio Yako!

 
Hii ni Hadithi nzuri inayoweza kubadilisha siku yako
 
Kulikuwa na kijana mmoja mdogo mwenye umri wa miaka minane (8), alimwendea babu yake na kumwuliza; “Babu nataka nifanikiwe sana kwenye maisha yangu. Naomba unipe mbinu za kufanikiwa”. Babu akamwangalia mjukuu wake kwa muda kidogo bila kumjibu kitu, baadaye akamwambia “nifuate”; basi yule kijana mdogo akaongozana na babu yake kwenda kwenye kitalu cha miti.  Walipofika pale walinunua miche miwili ya miti kisha wakarudi nyumbani.

Walipofika nyumbani babu akachukua mche mmoja wa mti kati ya ile miwili waliyonunua akaupanda nje kidogo kwenye eneo la wazi karibu na nyumbani. Kwa kawaida eneo ambalo alikuwa anaishi babu huyo na mjukuu wake lilikuwa kame na linaupepo mkali sana ambao hutimua vumbi kubwa. Miti mingi mikubwa huvunjika matawi yake kutoka na upepo huo.

Mche wa pili, babu aliupanda kwenye chungu kilichojazwa udongo wenye unyevunyevu. Kisha hicho chungu akakiweka pembeni ya nyumba karibu na dirisha kwenye eneo lenye kivuli. Mara baada ya kupanda miche yote, babu akamwuliza mjukuu wake unafikiri ni mche upi utasitawi sana?. Bila kusita  kijana akasema nafikiri huu uliowekwa kwenye chungu utasitawi sana kwa sababu unaudongo wenye unyevunyeu lakini pia sio rahisi upepo au ukame kuuathiri mche huu.

Baada ya majibu hayo babu hakumjibu kitu mjukuu wake. Siku si nyingi yule kijana alianza masomo,  baada ya miaka mitatu akarudi nyumbani kwa babu yake wakati wa likizo. Siku ile walifurahi wote kuonana baada ya muda mrefu kupita, Siku hiyo waliendelea na mazungumzo yao. Yule kijana akamwuliza tena babu yake; “Babu nilikuuliza swali, mimi nataka kufanikiwa zaidi maishani mwangu nifanye nini? Kipindi kile nilikuuliza hukunijibu naomba unijibu leo basi;.

Babu akamwambia mjukuu wake twende tukaiangalie miti tuliyopanda siku zile. Wakaenda kuangalia, alichoshangaa yule kijana aliukuta ule mti walioupanda nje kwenye uwazi na kwenye eneo lenye upepo mwingi, ulikuwa umestawi sana na ulikuwa mrefu wenye afya kuliko ule mti waliopanda kwenye chungu. Uliopandwa kwenye chungu ulikuwa haujasitawi sana wala haukurefuka kama ule mwingine hata haukuwa na matawi mengi kama ule mwingine.

Kijana alishangaa sana maana alichokiona ni kinyume na jinsi alivyokuwa anafikiria. Kisha babu yake akamwambia;  “Kama unataka kufanikiwa sana ni lazima ukubali kupambana na changamoto wala usithitubutu kukimbilia kivulini. Unapokuwa kivulini anga halitakutuza tuzo bali litamtuza aliyejuu yako na wewe utabaki kwenye udongo wenye unyevunyevu lakini huna mizizi imara wala matawi yako hayatasitawi sana”.

Babu akaendelea kumwambia mjukuu wake; Umeuona ule mti tuliopanda kwenye eneo la wazi umestawi sana kwa sababu ulikumbana na changamoto nyingi sana za ukame na upepo mkali, changamoto hizo zimefanya mizizi ya mti huo izame chini sana ili kuyafikia maji mengi lakini pia ili kujilinda na upepo mkali.

Zaidi ya yote anga hukituza kitu chochote kinachosimama chenyewe kikaonekana. Kwahiyo na wewe ukitaka kufanikiwa mjukuu wangu ni lazima ujifunze kuonekana kama wewe wala usithubutu kuwa kivulini mwa mtu mwingine kwa sababu ukiwa kivulini mwa mtu mwingine atakayeonekana ni yule anayekupa kivuli na anga litampa tuzo huyo. wala sio wewe.

Kumbuka ule mti tulioupanda kwenye chungu, tuliweka udongo unaoweza kujaza chungu hicho, kwa maneno mengine tulipima udongo wenye kutosha kujaza chungu hicho lakini ule mti tulioupanda nje kwenye eneo la wazi haupimiwi udongo, udongo wote ni wake. Vivyo hivyo na wewe mjukuu wangu kama unataka kufanikiwa epuka mtu fulani kukupimia kiasi cha mafanikio yako. Mtu anayekupimia pesa anataka usisitawi sana. Kwanini usiwe huru kupata kiasi chochote cha mafanikio unayotaka bila kupimiwa? Jifunze mjukuu wangu kuwa huru kama vile mti tulioupanda kwenye eneo la wazi ulivyokuwa huru ndio maana ulistawi sana. 
 
Mjukuu wangu nataka kukuambia kwamba wanaofanikiwa zaidi ni wafanyabiashara na wajasiriamali kwa sababu hawapimiwi pesa bali wanakusanya bila kikomo. Fanya hivyo mjukuu wangu kisha utafanikiwa na siku zote ikumbuke mifano hii ya miti miwili itakusaidia sana kufanikiwa kwako. 

Yule kijana alifurahi sana majibu yenye busara ya babu yake na alimwahidi babu yake kwamba atayatenda kwa vitendo mafundisho yake.Mwisho wa hadithi.
 
Bila shaka umejifunza mengi kutokana na hadithi hii. Jitahidi uyafanyie kazi unayojifunza. 

Tunapenda kusikia kutoka kwako pia kupitia comment zako!

0 comments: