JINSI CD4 INAVYOFANYA KAZI MWILINI

CD ni kifupi cha maneno ya kitaalam, yaani Cluster of Differentiation.
Hii ni aina mojawapo ya kiasili kilichoundwa kwa protini na mafuta (yaani glycoprotein) ambacho kinapatikana juu ya uso wa seli nyeupe za damu zijulikanazo kama Thelper Cells, Regulatory T-Cells, Monocytes, Macrophages na Dendritic Cells ambazo kazi yake kubwa ni kupambana na maradhi mbalimbali.

Zimepewa jina la CD4 kuonesha kuwa ni aina ya nne katika kundi la viasili vya CD. Kazi zake kubwa ni kusaidia baadhi ya chembe nyeupe za damu kupambana na wadudu waenezao maradhi mbambali katika mwili wa binadamu.

CD4 husaidia kukuza na kupitisha taarifa kutoka kwenye vipokeo vilivyopo kwenye T-Cells. Taarifa hii huzitahadharisha chembechembe nyeupe za damu kujiandaa kupambana na vidudu vilivyovamia mwili kwa kutumia njia mbalimbali. Aina hii ya chembechembe nyeupe za damu inayopambana na uvamizi wa mwili huitwa T-Lymphocytes.

CD4 ni aina ya protini inayopatikana katika ukuta wa seli zinazojulikana kama T-Helper Cells (pia hujulikana kama CD + Lymphocyte).

Virusi vya Ukimwi (VVU) hushambulia na kujishikiza kwenye protini hii kabla ya kupata uwezo wa kuathiri seli za T-Helper.
Seli hizi za T-Helper ndizo hulinda mwili dhidi ya maambukizi mbalimbali na hivyo kuchangia katika kustawi kwa kinga ya mwili.
Kupungua kwa seli hizi mwilini husababisha kupungua kwa kinga ya mwili na hivyo mtu kupata magonjwa nyemelezi.

Baadhi ya magonjwa nyemelezi yanayoweza kumpata mtu mwenye ugonjwa (VVU/Ukimwi) ni pamoja na magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vile ugonjwa wa Homa ya Mapafu (Pneumocyctic Carinii Pneumonia), Kifua Kikuu (TB) na Saratani.

Mengine ni magonjwa ya mfumo wa chakula kama vile Cryptosporidiosis, Candida (fangasi), Cytomegolavirus na kadhalika.
Lakini pia mgonjwa akipungukiwa CD4 huweza kupata magonjwa ya mfumo wa fahamu yaani Central/Peripheral Nervous System kama vile Cytomegolavirus, Toxoplasmosis, Cryptococcosis, Mkanda wa Jeshi na Saratani.
Mengine ni magonjwa mbalimbali ya ngozi (Skin Diseases) hasa Saratani ya Ngozi.

VIPIMO
Kutokana na uhaba wa vifaa vya kupimia kiwango cha seli aina ya CD4 katika nchi mbalimbali, Shirika la Afya Duniani (WHO), limetengeza mwongozo mwingine ambao utamsaidia mhudumu wa afya kutambua kama mgonjwa amefikia hatua ya ugonjwa wa Ukimwi na anastahili kuanza tiba au la.


Mgonjwa wa Ukimwi hupitia hatua zifuatazo kabla daktari hajaamua kumuanzishia tiba, yaani dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi na kurefusha maisha (ARV’S).
Hatua ya kwanza kitaalam huitwa Clinical Stage I ambapo mgonjwa kwa kawaida anakuwa hana dalili zozote za ugonjwa (Asymptomatic).

Lakini mgonjwa anaweza kuwa na uvimbe katika tezi ambao hauondoki, kitaalam huitwa Persistant lymphadenopathy. Hatua ya pili au kitaalam Cilinical Stage II ni pale mgonjwa anapopungua uzito chini ya asilimia 10 ya uzito wa mwili bila sababu maalum.
Lakini mgonjwa aliye na maambukizi akifikia hatua hii hujikuta akiwa na magonjwa ya mara kwa mara kwenye mfumo wa upumuaji kama vile kuumwa masikio, kinywa, tezi la koo yaani Tonsillitis, Otitis media na Pharyngitis, wengine huita magonjwa nyemelezi.

Mgonjwa pia anaweza kukumbwa na mkanda wa jeshi (Herpes zoster) au kuwa na vidonda pembezoni mwa mdomo au kwenye kinywa (Recurrent oral ulceration).
Anaweza pia kutokwa na vipele mwilini yaani kuwa na ugonjwa wa ngozi ambao kitaalam huitwa Seborrhoeic Dermatitis pia kuwa na maambukizi ya fangasi katika kucha.

Hatua ya tatu huitwa Clinical Stage III ambapo mgonjwa sasa hupungua uzito kupita kiasi kwa kuwa atakuwa anaharisha zaidi ya mwezi mmoja na atakuwa na homa inayojirudiarudia kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Lakini mgonjwa huyo akifikia hatua hii atakuwa na maambukizi ya fangasi kwenye kinywa na anaweza kujikuta akiugua kifua kikuu kwenye mapafu, au kupata maambukizi hatari ya vimelea vya bakteria hivyo kujikuta akiugua homa ya mapafu au ugonjwa wa uti wa mgongo.

Hatua hii ni mbaya kwa muathirika wa Ukimwi kwani anapata maambukizi katika mifupa na viungo vya mifupa yaani jointi, pia huwa na upungufu wa damu mwilini.

Hatua ya nne ya mgonjwa wa Ukimwi huitwa Clinical Stage IV ambapo mgonjwa hudhoofika mwili na kupata homa kali sana ya mapafu (Pneumocystis pneumonia) inayojirudia na hujikuta akipata saratani ya shingo ya kizazi.

Mgonjwa hupata maradhi kwenye mfumo wa figo au moyo yanayochangiwa na VVU na hukumbwa na maambukizi ya fangasi katika mishipa ya kupitisha chakula mpaka kwenye mapafu na mishipa yake ya kupitisha/kusambaza hewa mwilini.

Mgonjwa anaweza kupata ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na fangasi, mgonjwa pia hupata saratani ya kwenye tishu za mwili na maambukizi kwenye mishipa ya fahamu yanayosababishwa na vimelea aina ya Toxoplasma gondii. Mbaya zaidi hujikuta akipata maambukizi ya VVU kwenye ubongo. 

Mgonjwa akifikia hatua hiyo akapimwa na kuonekana ana upungufu wa CD4 daktari atamuanzishia dawa za ARV’S.

0 comments: