Jumatatu, 28 Machi 2016

Unapotaka Kuoa Au Kuolewa Je nini cha kuangalia. Sura Au Tabia?



  
Kuna msemo maarufu sana usemao "NI HERI UKOSEE KUJENGA NYUMBA LAKINI USIKOSEE KUOA AU KUOLEWA"


Karibu katika mada hii, imenibidi nikuletee mada hii kwa sababu kumekuwa na maswali mengi sana, vijana wanaotaka au waliokaribia kuoa au kuolewa kutaka kujua mke au mume wa kuoa wanatakiwa waangalie nini.

Ndoa ni taasisi nyeti sana, Taasisi hii ikiyumba basi jamii pia itayumba. tunashuhudia mambo mengi sana ambayo yanatokea kwenye jamii ambayo ni matokeo ya kuyumba kwa taasisi hii:

watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi, mmomonyoko wa maadili, umasikini, nk. Haya ni baadhi tu ya matokeo ya kuyumba kwa taasisi nyeti ya ndoa.

maranyingi kuyumba, na kuvunjika kwa ndoa hua kunahusiana sana
na mwanzo wa mahusiano ya kuelekea kwenye ndoa, yaani namna ya kuchagua yupi wa kuoa au kuolewa naye. 

  
Kabla hatujaaza kuangalia mada hii naomba nikupe kisa kimoja kilichotokea kwangu kipindi bado nikiwa mtoto. 

Kipindi hicho nilikuwa nikiugua mama alikuwa ananipa dawa ya miti shamba, alikuwa anaenda porini anachimba mizizi ya miti au majani halafu anakuja anaiponda ponda anailoweka kwenye maji au anaikausha anaisaga saga inakuwa unga. Kisha baada ya hapo alikuwa ananipa ninywe. Chakushangaza dawa hizo mara nyingi zilikuwa chungu sana halafu nikimwambia mama mbona dawa chungu hivi? Mama alikuwa anasema “Fumba macho tu mwanangu kunywa ili upone”. Nilikuwa nikifanya hivyo mara nyingi.

Kisa hicho ni mfano halisi wa vijana wengi wanapoingia kwenye swala la kuoa au kuolewa. Nimewasikia vijana wengi wakisema heri nioe mwanamke wa aina hii kwa sababu nikioa wa aina hii watakuwa wananiibia watu wengine. Utakuta kijana kaoa au kaolewa na mtu ambaye mara nyingi kwenye mambo yao “anafumba macho tu ili apone”. Mimi nauliza kwanini uishi maisha hayo? Wakati kunauwezekano wa kupata mke au mume mzuri unayempenda?

Je, Wazee wa zamani walikuwa wanaangalia sura au tabia?
Tunatakiwa kujifunza kutoka kwa wazee wetu, maana wahenga wanasema ya kale dhahabu.
Tukianza kwa mfano Ibrahimu alimwoa Sara, Sara alikuwa mwanamke mzuri sana wa sura na umbo na mcha Mungu, ndio maana Farao alimtamani ingawaje Sara alikuwa mzee wa zaidi ya miaka 75.
Vivyo hivyo Isaka alimwoa Rebeka maandiko yanasema alikuwa mzuri wa sura na umbo na mcha Mungu.
Yakobo alimwoa Raheli maandiko yanasema alikuwa mzuri wa sura na umbo na mcha Mungu.
Mfalme wa Wakaldayo Ahasuero alimwaoa Esta maandiko yanasema alikuwa mzuri wa sura na umbo na mcha Mungu.
Yoakimu alimwoa Suzana maandiko yanasema alikuwa mzuri wa sura na umbo na mcha Mungu.
Wazee wa makabila mengi hapa nchini walikuwa wanawashauri vijana wao wa kiume kuoa msichana mwenye sura nzuri na tabia nzuri.

Msichana au mvulana mwenye sura nzuri ni yupi?
Binadamu wote tumeumbwa kwa umbo linalofanana, ingawaje mwonekano wa mtu mmoja na mwingine hutofautiana. Tofauti hii ya mwokenano ndiyo imebatizwa kwa majina ya sura nzuri na sura mbaya lakini wote ni binadamu wale wale. Kwahiyo kwenye swala la kuoa au kuolewa mtu huchagua mtu wa kumwoa au kuolewa naye mwenye sifa anazozitaka yeye na kwa sababu alizonazo yeye. Kwenye swala la kuangalia sura nzuri au mbaya hiyo ni mitazamo tu (perception) ya binafsi. 

Nasema ni mitazamo ya binafsi kwa sababu mtu unayemwona wewe ni mzuri wa sura, mtu huyo huyo anaonekana kwa mwingine sio mzuri kama unavyomwona wewe. Ingawaje kuna mtu anaweza kuwa ni “popular” yaani anakubalika na wengi kwamba anasura nzuri lakini sio watu wote watakao kubali kuwa anasura nzuri.
Kwa kifupi sura nzuri au sura mbaya ni mtazamo wa binafsi, yaani ni hivi watu wote wanaweza wakasema huyu anasura mbaya lakini ukimwamgalia wewe unamwona anag’aa kama malaika utabaki unawashangaa tu wanaosema anasura mbaya.

Unapotaka kuangalia tabia ya mtu angalia mambo yafuatayo
Naomba tuangalie baadhi ya mambo yanayoonesha tabia ya mtu.

Jinsi anavyo vaa.
Mavazi ya mtu na namna anavyoyavaa unapata kumfahamu moja kwa moja jinsi alivyo mtu huyo. Sina haja ya kueleza sana namna uvaaji na aina za  mavazi jinsi yanavohusiana na tabia ya mtu husika, ukweli ni kwamba mavazi na uvaaji wa mtu unaonesha tabia ya mtu huyo. Kwako wewe unayeoa au kuolewa chunguza mavazi anayovaa mtu unayetaka kuwa na mahusiano naye halafu utaamua sasa uoe au uolewe naye.

Jinsi anavyoongea
Maneno ya mtu huakisi kile kilichomo moyoni mwake. Huhitaji kuhangaika wewe msikilize tu anapenda kuongelea mambo gani, basi, utapata kumfahamu moja kwa moja. Mfano unaweza kumwuliza unapenda miziki gani atakwambia halafu chunguza kama hiyo miziki na wewe unaipenda kama huipendi maana yake hayuko upande wako. Jinsi mtu anavyoongea sauti yake na maneno yanayotoka moyoni mwake ndivyo alivyo mtu huyo. Sikiliza sana maneno anayoongea utaupata ukweli wote wa mtu huyo.

Jinsi anavyoonekana.
Tabia ya mtu imefichwa kwenye sura ya mtu. Mfano mara nyingi watu utawakuta wanasema huyu ni jambazi ukiwauliza kwanini watakwambia huoni hata sura yake?. Mwonekano wa sura ya mtu mara nyingi ndivyo alivyo mtu huyo. Chunguza sana sura ya mtu unayetaka kuwa nae kwenye mahusiano yako utapata kufahamu vyema jinsi alivyo mtu huyo.

Jinsi anavyotembea.
Kutembea kwa mtu kunamwonesha jinsi mtu huyo alivyo. Kama mtu anatembea kwa madaha mengi, mwendo wa kubinuka binuka, mikono yake haitulii mara huku mara huko kusiko kawaida unapata kujua kichwani mwa mtu huyo kuna nini. Tembea ya mtu inawonyesha jinsi alivyo.

Jinsi anavyotabasamu na kucheka.
Tabasamu la mtu na kucheka kwake kunamwonyesha jinsi alivyo. Mfano kuna mtu mwingine ili atabasamu au acheke ni mpaka umempa noti, au utakuta mtu anatabasamu lakini unagundua kabisa anafanya unafiki. Chunguza tabasamu na kicheko cha mtu unayetaka kuingia naye kwenye mahusiano.

Sasa uoe au uolewe kwa kuangalia sura au tabia?
Mimi nakushauri uoe au uolewe na yule mnayependana. Sura na umbo zuri sio cha lazima ingawaje ni kitu muhimu kukiangalia na kukizingatia. Nasema hivyo kwa sababu usifanye kama mama alivyokuwa ananiambia “Fumba tu macho kunywa”. 

Kama wewe ni mwanaume na huwa unapendelea wasichana wa aina fulani hivi, basi tafuta msichana wa aina hiyo hiyo  halafu uoe. Usikubali kumwoa yule usiyempenda maana siku za baadaye utatamani kutafuta mwingine.  

Mfalme Ahasuero alikuwa na uwezo wa kuoa msichana yeyote aliyekuwa anataka lakini aliwakusanya wasichana wote wazuri halafu akamchagua Esta msichana bikira, mzuri wa sura na umbo zuri. Huyo ndiye aliyempenda. 

Inawezekana ningekuwa mimi au ungekuwa wewe usingempenda Esta. Ndivyo ilivyo kwenye swala la kuoa au kuolewa, chagua unayempenda.

Tabia ni kitu kingine cha muhimu sana kwa sababu unaweza ukangalia sura ukasahau tabia, utajuta. Ndiyo maana vijana wengi huwa wanasema sitaki kuolewa au kuoa na mvulana au msichana mzuri maana nitakuwa nagawana na wengine. Mimi hiyo naiita imani potofu. Wapo wasichana wazuri na wavulana wazuri wenye tabia nzuri labda sema ni uvivu wako tu wa kutafuta.

Kumbuka, ni afadhali umwoe mtu unayempenda na anayekupenda. Kama mmoja atapenda na mwingine hapendi,  hiyo nayo ni shida itawasumbua sana.
 


0 comments: