Mashaka Maziku (60) mkazi wa kata ya Mbugani manispaa ya Tabora ambaye alimkata mkewe sehemu za siri kwa imani za kishirikina ili aweze kujipatia mali amehukumiwa kwenda jela miaka saba.
Mbali ya Maziku mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo Kahele Paul aliyekuwa ni mganga wa kienyeji amehukumiwa kwenda jela miaka mitano baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kula njama kwa nia ya kutenda kosa.
Adhabu hizo zimetolewa jana na hakimu mkazi wa mhakama ya mkoa wa Tabora Jackton Rushwela baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka uliokuwa unaongozwa na wakili wa serikali Idd Mgeni.
Hakimu Rushwela alisema anatoa adhabu hiyo ili liwefundisho kwa wananchi wengine wanaokuwa na tamaa ya kujipatia mali kwa njia za kishirikina huku wakiwasababishia madhara watu wengine.
Awali wakili wa serikali aliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo kati ya oktoba 29 na novemba 2/2014 katika eneo la Kazaroho kata ya mbugani mjini Tabora.
Wakati wa tukio hilo ilidaiwa kuwa Maziku aliambiwa na mganga wa kienyeji ambaye ni mshitakiwa wa pili katika shauri hilo kwamba akipeleka sehemu za siri za mkewe atapata shilingi milioni tano.
Maziku baada ya ushauri huo huku akiwa na tamaa ya kujipatia mali alinchukua mkewe (jina linahifadhiwa) na kwenda kunnywesha pombe ili aweze kutimiza ukatili huo wa kijinsia ambao unapigwa vita na dunia nzima.
Upande wa mashitaka ambao ulileta mashahidi wanne waliiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa baada ya kumnywesha pombe nyingi mkewe alichukua kishu na kumkata sehemu za siri na kuzihifadhi kwenye mfuko wa suruali yake na akatoweka.
Walibainisha kuwa mama huyo alikuwa akipiga kelele kutokana na maumivu makali aliyopata huku akivuja damu nyingi na aliokolewa na majirani na kumpeleka hospitali ya mkoa kwa matibabu.
Maziku baada ya kukamatwa na kuhojiwa alikana akidai kwamba yeye aliondoka na kumwacha mkewe akiwa ni mzima lakini ulipofanyika upekuzi nyama ya nyeti hizo zilikutwa kwenye mfuko wa suruali yake.
Upande wa mashitaka uliiomba mahaka itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwani vitendo vya ukatili vya aina hiyo kwa ajili ya kujipatia mali vimekuwa vinawasababishia madhara watu wasiokuwa na hatia.
**************
0 comments:
Chapisha Maoni