Makala hii ni tafakari huru kuhusu
mambo ya msingi katika mahusiano. Hapa
utapata tafakari ya maana ya maneno na imani ambazo zinatutatiza wengi wetu.
1. Mchanganyiko mkubwa kuhusu maana ya mahusiano, mapenzi na
ndoa:
Labda kipengele hiki tuanze kwa kueleza
kuwa kunaweza kuwepo ndoa, lakini yasiwepo mahusiano wala mapenzi. Inaweza
kuonekana kama inachanganya kidogo, lakini ndio ukweli wenyewe. Ndoa ni namna tuu ambayo
wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano.
wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano.
Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine
, na ni namna ya kutaka kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho
kitatokea kuvunjika, basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu
zilizopo za ndoa husika, ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi,
kugawana mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka
kiapo kwa Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua.
Hivyo basi, ndoa haijengi
mahusiano wala mapenzi. Kiuhalisi inabidi kwanza yawepo mahusiano na mapenzi
kisha ndio kiapo kifanyike, kwani kinyume cha hivyo ni kuwa unakula kiapo
‘feki’.
Ndio maana basi, ni muhimu kwa
wapenzi kutambua kweli kama wanahitajiana, kuwa kwenye mahusiano na kutafakari
kwa uhuru kama kweli wanataka kuweka kiapo rasmi cha kuwa pamoja.
Kutumia ndoa kama kinga ya
kuhakikisha mahusiano yako yanadumu ni maamuzi magumu ambayo pengine yanaweza
yasilete faida hapo baadae.
2.Mahusiano na ndoa nyingi huyumbishwa na Matarajio yasiyo
halisi
Kabla hata ya kuingia katika
mahusiano na hatimaye ndoa wengi wetu huwa na matarajio binafsi ya kimaisha.
Matarajio haya yanajumuisha vile tunavyotaka sie wenyewe kuwa hapo baadae,
pamoja na matarajio ya vile tunavyotaka wenza wetu wawe.
Hata hivyo katika hali halisi
tunajikuta sisi wenyewe hatuwezi kujibadilisha au kujiweka kwa usahihi vile
tunavyotamani kuwa (kwa sababu kwa kila tunachojaribu kufanya kuwa bora,
tunajikuta bado tuna madhaifu mawili matatu). Pamoja na ukweli huu, tunajikuta
tupo na matarajio ya kuwafanya wenza wetu wawe watu wa aina fulani. Kwakuwa
kiasili binadamu ni kiumbe huru, tunajikuta wenza wetu nao wakiwa ‘busy’
kutimiza ndoto za vile wanavyotamani kuwa iwe kimavazi, aina ya marafiki,
utafutaji wa kazi , kujiendeleza kimasomo, aina ya mali za kununua, hata
kufikiria tofauti aina ya maisha wanayotaka muishi.
Matokeo yake ukinzani huu wa
matarajio ni mkanganyiko wa mgongano wa mawazo kati ya wawili nyie, na mwanzo
wa vita ya chini kwa chini ya nguvu ya maamuzi katika mahusiano yenu.
3. Kuweza kumbadili tabia mwenza wako
Mojawapo ya jambo ambalo hufanywa na
wengi walio katika mahusiano ni kuwa na ‘tamaa’ ya kutaka kumbadili tabia
fulani mwenza wake. Hata hivyo ‘tamaa’ hii ni sehemu ya yale tunayoyaita
matarajio yasiyo halisi, kwani tabia ya mtu hujengwa na mambo mengi sana,
ikijumuisha aina ya makuzi, aina ya mfumo wa imani mtu anaouamini, aina ya
marafiki alio nao, uwezo wake wa kujiamini katika kubadili tabia kwani wengine
wameshakata tamaa kuwa hawawezi kukata tamaa, na zaidi sana, mabadiliko ya
tabia huhitaji mfumo endelevu na wenye kusoma vema asili ya tabia ili kuweza
kuirekebisha.
Hata hivyo wengi wetu kwenye
mahusiano, hutegemea ‘mapenzi’au vitisho tuu kama vile ‘nitakuacha mie ’, kama sababu ya kumfanya mtu abadilike
kitabia.Udhaifu wetu katika kutambua asili ya tabia ya mtu husika na mbinu za
kisayansi za kubadili tabia hufanya zoezi la kubadilishana tabia kuwa gumu na
pengine lisilowezakana.
4. Kuvumilia ndio kuonyesha upendo na ndio kudumisha
mahusiano
Hii ni aina nyingine ya matarajio
ambayo sio halisi kwani kiukweli kila mtu analo jukumu la kufanya bidii kuwa
mtu mwema, hivyo hauhitaji kubeba ‘uzembe’ wa mwingine kwa kisingizio tuu cha
kuwa unaonyesha upendo hususani pale ambapo ni kwa uzembe tuu au kutokujali
kwake mwenza husika amefanya jambo fulani.
Kwa jinsi kasumba hii ilivyo enea
sio ajabu kukuta mtu akifanya mambo mabaya kwa mwenza wake kwa makusudi ili tuu
eti apime kama kweli mwenza wake ni mvumilivu.
Kumbuka hapa hatumaanishi kuwa
kusamehe ni kosa. Hapana, kusameheana ni muhimu, lakini sio kwamba ni muhimu
tuu katika mapenzi. Kusameheana ni jambo la asili, na tunapaswa kusameheana kwa
mambo mengi nje hata ya mahusiano.
Tunachosema ni kuwa kuna kasumba ya baadhi yetu kuona kuwa wanayo
‘haki’ ya msingi ya kukosea eti tuu kwakuwa tuu mwenza wake analazimika
kusamehe ili kuonyesha kweli anao upendo wa dhati.
Amini usiamini, kasumba hii ya
kutarajia aina ya pekee ya kusamehewa na kuvumiliwa kwa kisingizio tuu cha kuwa
upo kwenye mapenzi na mwenza wako, hurudisha nyuma maendeleo ya mahusiano yenu
kwani mwenzi wako nae ni binadamu na kumbuka anayo matarajio mengine ya maisha,
isitoshe na yeye anahitaji upendo na kujaliwa na wewe, hivyo kutarajia kwako
kusamehewa na kuvumiliwa kuna mnyima haki mwenza wako. Hatimaye kutegema kwako
kusamehewa kila wakati, kunamfanya mwenza wako atilie mashaka upendo wako
kwake.
5. Uaminifu = Upendo= Kudumu kwa mahusiano
Pamoja na ukweli kuwa mwenza wako
anatarajia utakuwa muanifu kwake, elewa kuwa kuwa mwaminifu pekee katika
mahusiano yako sio tiketi ya kudumu kwa mahusiano yenu kwakuwa watu wanaingia
kwenye mahusiano sio tuu kwa kuwa wanataka kuwa na mtu mmoja muaminifu bali
wana mahitaji mengine wanayohitaji.
Zungumza na mwenza wako, fanya
utafiti wako binafsi kuhusu mpenzi wako ujue mambo mengine anayohitaji toka
kwako.
Pia msikilize anapokutaka urekebishe
mambo kadhaa au ufanye mambo fulani. Inapendeza pale unapomfanyia mtu mambo
yanayompendezesha kwa kuwa hivyo ndivyo anavyotaka, sio kwakuwa tuu wewe
unadhani kufanya hivyo kutampendezesha mhusika.
JITAFAKARI NA UTATHMINI MCHANGO WAKO KATIKA KUDOROLA AU KUVUNJIKA KWA MAHUSIANO NA NDOA YAKO .....
0 comments:
Chapisha Maoni