Jumatano, 30 Machi 2016

Epuka Kuulisha Ubongo wako Mawazo Hasi!


Ni sheria ya asili kwamba chochote kinacholishwa kinakua, na chochote kinachokosa chakula kinadhoofu na kufa.
 
Wote tumewahi kuona watoto wadogo, kadiri anavyopata chakula kizuri, yaani mlo kamili anakua vizuri na kuwa na afya bora. Lakini anapokosa chakula kizuri afya yake inakuwa dhoofu na anaweza kufariki. Sasa mawazo hasi nayo huwa yana chakula chake, na yakipata chakula hiki ya akua na kustawi sana. Ila pia yakikosa chakula hiki yanadhoofu na kufa kabisa.
 
Kama unasoma hapa unajua lengo letu kubwa ni lipi, ambalo ni kudhoofisha kabisa mawazo hasi ambayo yanatujia. Na njia pekee ya kufanya hivyo ni kuhakikisha hatuyapi chakula chake.
 
Ukweli ni kwamba huwezi kuyazuia kabisa mawazo hasi kuingia kwenye akili yako, yatakuja tu. Ila wewe una uchaguzi wa kuyalisha ili yaendelee kukua na kukutawala, au kuyanyima chakula ili yadhoofu na kufa kabisa. Sasa je huoni ni vizuri sasa ukakijua chakula cha mawazo hasi ili uweze kuyanyima chakula hiko na yafe? 

Karibu sasa ukijue chakula hiko.
Chakula cha mawazo hasi, ni mlo kamili wenye virutubisho vitatu muhimu sana kwa ukuaji wa mawazo hasi;
 
Kirutubisho cha kwanza ni KULALAMIKA. 
Pale unapolalamika kwa nini iwe wewe, kwa nini itokee kwako na mengine, hapa unayalisha mawazo hasi
na yataendelea kustawi.
 
Kirutubisho cha pili ni KULAUMU WENGINE.
Unapolaumu wengine maana yake unajitua wewe mzigo kwa jambo lolote lile, lakini hii njia ya kukusaidia wewe, itazidi kuchochea mawazo hasi.
 
Kirutubisho cha tatu ni UMBEYA. 
Kadiri unavyoshiriki kufuatilia na kusambaza mambo ambayo hayakuhusu au huna uhakika nayo, ndivyo unavyozidi kuchochea mawazo hasi na kujiweka pabaya zaidi.
 
Epuka kulisha mawazo hasi yanayokujia kwa chakula hiko, na mawazo hasi yatapotea yenyewe.
Ila kama utashiriki kwenye kuyapa mawazo hasi virutubisho hivyo, umeyakaribisha yadumu kwako.

UKWELI NI KWAMBA chakula cha mawazo hasi ni mlo kamili wenye virutubisho vya kulalamika, kulaumu wengine na umbeya. Tambua kuwa kufanya mambo hayo matatu kwenye jambo lolote unalokutana nalo ni kuchochea mawazo hasi yaendelee kuwa na wewe. Epuka mambo hayo matatu kwa uwezo wako na nguvu zako zote.
 
CHUKUA HII:
Watch out for the joy-stealers: gossip, criticism, complaining, faultfinding, and a negative, judgmental attitude. - Joyce Meyer
 
(Kuwa makini na wezi hawa wa furaha; umbeya, kukosoa, kulalamika, kutafuta makosa na mtazamo hasi wa kuhukumu).

Chakula cha mawazo hasi ni kulalamika, kulaumu na umbeya, epuka sana vitu hivyo vitatu ili kuwa na maisha bora.

0 comments: