Jumatano, 30 Machi 2016

Kutafuta Pesa Ni Kama Mchezo, Cheza Ufurahie Maisha



Ndugu na rafiki yangu, sina hakika na hali yako kiuchumi kwa sasa iko je, unaweza kuwa na hali nzuri kiuchumi au hali inaweza kuwa sio ya kuridhisha au unaweza kuwa na hali mbaya kabisa. 
Watu wengi hapa Tanzania wamekuwa wakilalamika kuwa maisha ni magumu. Sikubaliani moja kwa moja na maneno hayo labda kwa shingo upande hivi naweza kukubaliana na maneno hayo. Ninachokijua mimi ni kwamba maisha ni mazuri sana tena ni marahisi sana. Mtu akisema  maisha ni magumu, ugumu  wake unasababishwa na kutokujua cha kufanya ambacho kinaweza kukuletea pesa. 
Ziko mbinu lukuki za kukuletea pesa, zina hitaji mtaji kidogo tu wakati mwingine bila hata mtaji. Kinachotakiwa ni kupata ufahamu kidogo tu wa namna ya kufanya na ukitekeleza, tayari unaanza kubadilisha maisha yako. Unaanza kuvuna pesa.
Kuna dunia mbili japo watu wote tunaishi kwenye dunia hii hii moja. Wewe unapolalamika pesa hakuna, mtu mwingine ,tena anaweza kuwa jirani yako anashangaa kuona jinsi pesa zilivyo nyingi. Kwahiyo, wewe unaiona dunia haina pesa, jirani yako anaona dunia imejaa mapesa mengi.

Kutafuta Pesa Ni Mchezo
Usitafute pesa kama unatafuta maisha. Tunajua mtu anapokuwa anaumwa huwa tuko makini kuhakikisha anapona haraka, lengo la kupona ni
ili awe na maisha yake maana asipopona anapoteza maisha yake.
Unapotafuta pesa, usitafute kama unatafuta maisha. 
Tafuta kama unacheza mchezo. 
 Kama umeshawahi kucheza mchezo wowote katika maisha yako utakuwa unafahamu hiki ninachosema. Lengo la mchezo wowote ni kufurahisha, kuburudisha, kujenga afya na kushinda. 
Unapokuwa unacheza uwanjani unajisikia raha, unajisikia amani na hata ukitoka uwanjani bado unajisikia vizuri kwa sababu mchezo unafurahisha, unaburudisha na unajenga afya, lakini pia unaleta ushindi.
Kuna aina nyingi sana za michezo duniani. Kuna mchezo wa mpira wa miguu, kuna mpira wa pete, kuna golf, kuna mpira wa wavu, kuna mchezo wa magari, kuna mchezo wa ngumi nakadhalika. Pia, kuna mchezo wa kutafuta pesa.
Kutafuta pesa ni mchezo sawa na michezo mingine, huwezi kushinda mchezo wowote bila kufanya mazoezi, huwezi kupata pesa bila kufanya moja wapo  ya njia za kupata pesa. Katika maisha yako usiangalie tu kazi moja ya kufanya yenye kukuletea pesa unatakiwa kungalia kila kona kama vile mchezaji wa mpira wa miguu, uwanja wote ni wa kwake. 
Kama vile unavyocheza kwa furaha, tafuta pesa kwa furaha hata pale unapokosa usihuzunike, jifunze, kisha songa mbele.  Ukitafuta pesa kwa jaziba huipati ng’o au unapata kiduchu halafu unaweza kupunguza hata siku zako za kuishi kwa sababu ya mawazo.
 
Lakini ukitafuta pesa kama mchezaji, kwanza utaufurahia mchezo, utaburudika moyoni mwako, utafarijika na bado utakuwa na afya njema na kadri unavyocheza ipo siku utakuwa mshindi, hapo ndipo raha ya kucheza itakapo kamilika.

0 comments: