“Hakuna
mtu badala yako, pambana kwa ajili ya maisha yako. Fahamu kuwa hakuna mtu
yeyote duniani atakayebeba maisha yako. Mtu anayekuchukia na kukufanyia mambo
mabaya analengo la kukuchelewesha kwenye safari yako ya mafanikio”
Wakati fulani, nilikutana na rafiki
yangu mmoja, anaishi na mke wake na wanamtoto mmoja. Mwaka mmoja uliopita
alifiwa na wazazi wake wote hivyo akabaki yeye na mke wake kwenye familia hiyo,
na akateuliwa na wanandugu awe msimamizi mkuu wa mali za wazazi wake yakiwemo
mashamba na mali nyingine.
Mara baada ya kupewa jukumu hilo, kuna baadhi ya
wanandugu hawakufurahishwa na madaraka aliyopewa ikizingatiwa kwamba yeye ni
mdogo kuliko wote, wakati huo alikuwa anaumri wa miaka 26. Matokeo ya kupewa madaraka hayo
yamewafanya baadhi ya wanandugu wamchukie, hata kufika hapo nyumbani hawafiki au wakija
wanaishia kwa majirani huku wakimsema kwa kila neno baya. Ingekuwa heri kama
wangeishia kumsema kwa maneno tu lakini kuna wengine wanaenda mbali zaidi kwa kumtafutia
dawa za kumloga ili wamharibie kabisa mambo yake.
Jumapili moja nilimtembelea nyumbani
kwake, nikamkuta anahali mbaya kimawazo huku hajui afanye nini. Kibaya zaidi
yeye na mke wake hawakuwa na matumaini ya kusonga mbele kiuchumi.
Je,
Wewe unahali Kama Hiyo Au Inafanana Na Hiyo?
Huenda wewe ndugu umekumbana na mkasa wa namna hiyo wa
ndugu kukuchukia kwa sababu mbalimbali.
Wanaweza kuwa ni ndugu zako wa ukoo au
wanafunzi wenzako au wafanyakazi wenzako au jamaa zako wa karibu wanakuchukia, hata ukisema chochote hawakuelewi zaidi ni
kukutukana au kukunenea mabaya.
Anaweza kuwa ni mtu mmoja anakuchukia na
anakutesa kwa mateso mengi kiasi kwamba unashindwa namna ya kufanya. Wakati mwingine
umekuwa na wasi wasi na maisha yako. Je, katika mazingira kama hayo utafanya
nini?
Fanya
Mambo Haya Kuvuka Mahali Hapo.
Jambo
la kwanza: Hakuna mtu badala yako, pambana kwa ajili
ya maisha yako.
Fahamu kuwa hakuna mtu yeyote duniani atakayebeba maisha yako. Mtu
anayekuchukia na kukufanyia mambo mabaya analengo la kukuchelewesha kwenye
safari yako ya mafanikio. Kama utaendelea kujibizana naye au kumnunia
unachelewa kwenye mafanikio, halafu unapoteza njia yako.
Unachotakiwa kufanya
ni kusonga mbele usikubali maneno ya mtu yakujeruhi moyoni mwako nakukutoa
kwenye mstari wa mafanikio.
Endelea na juhudi zako za kutafuta mafanikio waache
waseme, waache waongee kila neno wanalojua, wewe usiwajibu kaa kimya halafu
usiruhusu neno lolote likuumize moyoni mwako.
Kila unaposikia neno au matusi
achana nayo wewe jifanye hujasikia songa mbele. Kumbuka adui anambinu nyingi za kukuharibia maisha yako usimpe nafasi
akuharibu kwa maneno yake.
Ukianza kujibizana naye unawasha moto wa hasira kiasi kwamba hutaweza
kufanya mambo yako ya msingi. Kwahiyo
jifunze kukaa kimya na kupotezea kila neno kisha songa mbele kuelekea mafanikio
yako.(Fight for your own life)
Jambo
la pili: Tumia maneno mabaya kama kichocheo cha kufanikiwa zaidi.
Hii ni mbinu nzuri sana ya kushinda hila na mbinu za adui wa mafanikio. Ukisikia
neno baya likinenwa juu yako, usichukie furahi zaidi halafu yageuze maneno hayo
yawe hamasa ya kufanya bidii zaidi kwenye mafanikio yako.
Ili kuitumia mbinu hii
vizuri, unatakiwa uandae taswira yako ya mafanikio ambayo mara kwa mara utakuwa
unaiangalia na kupata nguvu ya kuifuta hadi uipate. Kwahiyo kila mtu
anapokutukana humwangalii aliyekutukana unaangalia ile taswira ya mafanikio
yako, kwahiyo hayo maneno aliyokutukana yanakutia uchungu wa kuifuata taswira
hiyo.
Fanya hivyo kwa furaha huku ukitiwa nguvu na maneno ya wanaokuchukia. Ili
kuipata taswira ya mafanikio yako andaa malengo yako.
Jambo
la tatu: Watu wote ni wagonjwa wa akili, kwahiyo jifunze kufurahi
na kupenda kila wakati.
Don Miguel Ruiz anasema watu wote hapa duniani
wanamajeraha akilini mwao, kwahiyo kila mara utawakuta wanawaka hasira na
kuumia moyoni mwao halafu wanatafuta mahali pa kupumzisha machungu ya kuumwa
kwao.
Akikupata mtu kama wewe atakuchukia na kukulaumu kwa kila jambo. Usishangae,
kwa sababu anaumwa ugonjwa wa akili. Tatizo
na wewe unaumwa ugonjwa wa akili ndio maana akikutukana unachukia na kuumia
moyoni mwako kwa sababu amegusa jeraha lililoko akilini mwako.
Ili kushinda
maumivu ya kuguswa kwa majeraha yako akilini, unatakiwa ujifunze kuwapenda watu
wote hata maadui zako. Jifunze kufurahi kila mara kila neno unalolisikia
ligeuze liwe furaha halafu mpende anayekunenea mabaya.
Ukiweza kuitumia mbinu
hii, ugonjwa wa akili yako utapona haraka halafu kila neno na chuki na lawama
zitakazoletwa kwako hazitakuumiza hata kidogo badala yake utajaa upendo na furaha
katikati ya chuki za wanadamu.
Jambo
la nne: Kila mtu atakufa. Hii ni mbinu nyingine nzuri ya
kutumia kushinda chuki na lawama za wanadamu.
Kama kuna mtu atakuja kwako
akaanza kukunenea kila neno baya na matusi na chuki juu yako, unatakiwa
umshangae halafu waza moyoni mwako hakuna atakayeishi milele. Ukiwa makini na
mbinu hii moyoni mwako, utajaa furaha kila wakati hata wakati mtu anapokuchukia
na kukununia bado utakuwa na furaha na utaanza kumhurumia kwa maneno yake
yasiyo na maana.
Don Miguel Ruiz katika kitabu chake The
Four Agreement anatuhimiza tujifunze kutoka kwa malaika wa kifo. Malaika
wa kifo anatufundisha kuishi maisha ya furaha na utakatifu kila siku na
kujiweka tayari kwa maana muda wowote tunaweza kufa. Tumia mbinu hii kumpuuzia
kila mtu anayekulaani huku ukijua hataishi milele.
Jambo
la tano: Angalia Fursa Nyingine. Kama kuna uwezekano wa kukaa
mbali na watu wanaokuchukia, basi fanya hivyo. Mfano, mtu anaweza kuwa
anakuchukia kwa sababu anakuona kama mzigo kwa kuwa unaishi nyumbani wake. Ukiona
sababu ya kukuchukia ni hiyo, jaribu kuangalia uwezekano wa kuondoka mahali
hapo. Tafuta chumba chako uanze maisha yako utajifunza mengi na mbinu za kupata
pesa utazipata nyingi.
Wakati mwingine sio lazima uondoke nyumbani unaweza
kutafuta biashara yoyote ili uwe unaingiza pesa kidogo kidogo kuliko kukaa bure
tu.
Jambo
la sita: Andaa
kitengo maalum kwa ajili ya mtu anayekuchukia. Tunaona katika ulinzi na usalama
wa nchi yetu, kama kuna eneo lina migogoro mingi sana ya uvunjifu wa amani,
jeshi la polisi huwa linaandaa kanda maalumu kwa ajili ya kusogeza huduma
karibu kwenye eneo hilo na kutatua migogoro iliyopo.
Fanya vivyo hivyo kwa mtu
anayekuchukia mwandalie kitengo maalumu ili usogeze huduma karibu yake zaidi
kiasi kwamba ataondoa chuki yake na kukuona wa thamani kwake. Kwenye kuandaa
kitengo maalumu unatakiwa umpende na
umpatie mahitaji yoyote unayoweza kumpa.
Unaweza kuwandalia zawadi au unaweza
kumfanyia jambo lolote jema. Mfanyie mambo mema mengi uwezavyo hatimaye
utaubadili moyo wake. Usiwe mtu wa kulipiza kisasi bali uwe mtu wa upendo na
kusonga mbele kwenye mafanikio yako.
Hata kama ataendelea kukuchukia ipo siku
ataujua ukweli halafu atakuomba msamaha mwenyewe.
Jambo
la saba: Fanya vizuri zaidi. Kama mtu anakuchukia kwa kuwa
unafanya vibaya kwenye jambo fulani, unatakiwa udhamirie kufanya vizuri zaidi. Anza
kufanya vizuri zaidi mfano; darasani, kazini kwako, kwenye biashara, kwenye kilimo,
kanisani, msikitini n.k. Unapofanya vizuri zaidi humridhishi mtu yule anayekuchukia bali pia inakusaidia wewe kupata
uzoefu na kuboresha maisha yako.
Jambo
la nane: Usipambane kwa
nguvu za giza, kaa vizuri na Mungu wako. Kama mtu anayekuchukia anatumia nguvu
za giza kukudhuru, usihangaike kutafuta nguvu za giza ili upambane naye. Unatakiwa
kukaa vizuri na Mungu wako maana tunajua kwamba ulozi na uchawi hauwezi
kumdhuru mtu aliye kaa vizuri na Mungu wake. Tena ukikaa vizuri na Mungu wako,
halafu mtu mwingine atumie nguvu za giza kukudhuru, hajui anachokifanya maana
Mungu atamjibu kwa mapigo makali.
Unayo
Safari Ndefu
Kumbuka nilivyokwambia, hakuna mbadala wa maisha yako,
maisha yako ni yako wewe mwenyewe, kama utabaki unakatishwa tamaa na mtu kiasi
kwamba unaacha kusonga mbele kwenye mafanikio yako, ujue kabisa unajiandalia
maisha magumu.
Usikubali mtu yeyote kwa namna yoyote ile akurudishe nyuma
kwenye safari yako ya mafanikio. Ukikwama kwenye maisha yako hakuna
atakayekusaidia zaidi zaidi watakucheka na kukuona huna lolote.
Kama ni hivyo
kwanini ukatishwe tamaa na mtu. Usikubali, pambana hadi kieleweke na unatakiwa
kuweka msimamo wa maisha yako. Unatakiwa kusema “kila jambo acha litokee tu
lakini kufanikiwa lazima”.
0 comments:
Chapisha Maoni