Jumamosi, 2 Aprili 2016

Mafanikio Hayaonekani Kwa Urahisi, Yatafute Kwa Umakini!!




Hebu Tujaribu Kuona Kama Tunaweza Kujifunza kutokana na Hadithi Ya Shamba La Ekari Tatu Za Dhahabu Barani Afrika

Miaka ya 1930 katika nchi ya Ghana kulikuwa na mzee mmoja alikuwa anashamba la ekari tatu. Bahati mbaya hakujua kama shamba lake limejaa dhahabu. 

Siku moja akaja mgeni kutoka Ubelgiji, alikuwa anazunguka katika nchi za Afrika kuangalia wapi kuna madini kwa ajili ya uwekezaji. Bahati nzuri mgeni huyu akafika kwenye shamba la mzee huyu wa Ghana, alipoliona tu lile shamba alishangaa kuona shamba zima la ekari tatu limejaa dhahabu.  

Kwa lugha ya upole mgeni akamsalimia yule mzee mwenye shamba, kisha mgeni akaanza kumwambia yule mzee, “Laiti ningepata shamba la dhahabu lenye ukubwa wa ekari tatu, ningeweza
kununua kila kitu hapa duniani.” Mzee aliposikia neno dhahabu hakuelewa mpaka alipoeleweshwa vizuri na mgeni wake. Basi mzee akamwuliza yule mgeni, “Hivi nawezaje sasa kulipata shamba kubwa la dhahabu namna ile?”. Mgeni akamwambia yule mzee inabidi kutafuta, mimi nimetoka Ubelgiji kuja kutafuta shamba kubwa la dhahabu. 

Mazungumzo yao yaliendelea lakini mwisho wa yote ilikuwa ni makubaliano ya kuendelea kutafuta shamba kubwa la dhahabu la ekari tatu. Mgeni alirudi kwao Ubelgiji kwenda kutoa taarifa kwamba amepata shamba kubwa la dhahabu nchini Ghana, hivyo ilitakiwa wajiandae timu kubwa kwenda kuanza uwekezaji. 

Yule mzee naye alifunga safari kuzunguka kila mahali Afrika na hata Ulaya alifika akitafuta shamba kubwa la dhahabu ili aweze kuwa tajiri. Akiwa nchini Uholanzi maisha yalikuwa magumu na alikuwa hajapata shamba kubwa la dhahabu na  hakuweza kurudi tena Ghana huenda alifia huko ughaibuni akiwa masikini huku akiliacha shamba lake limejaa dhahabu.

Hadithi Inatufundisha Mambo Kadhaa Hapa.

A.   Tumesikia habari ya shamba la dhahabu (mafanikio) mimi na wewe tunalitafuta. Kwenye kutafuta mafanikio yetu hapo ndipo inapokuja tofauti kubwa. Wapo wengine wanaamini mafanikio watayapata kwa kuajiriwa, Wapo wengine wanaamini mafanikio watayapata kwa kufanya biashara, wapo wengine wanaamini watapata mafanikio kwa bahati nasibu na wengine wanaamini vyovyote vile. 

      Kila  mtu anatafuta shamba la dhahabu anakokujua au anakoamini lipo. Nataka nikwambie kwa dunia ya sasa yenye maendeleo makubwa ya teknolojia shamba la dhahabu lipo kwenye Mtandao Wa Intanet. Unaweza kukubaliana na mimi au unaweza kukataa, lakini mimi nasema mtandao wa intanet ndiyo unaoogoza kwa sasa hapa duniani kuwapatia watu wengi zaidi mafanikio makubwa kuliko katika kipindi chochote kilichowahi kutokea. 
B.   Tunatafuta shamba la dhahabu bila kujua dhahabu ikoje au inaonekanaje. Kutafuta kitu huku hujui kikoje unaweza kukipita bila kujua kama ni chenyewe. Kutafuta mafanikio bila kuwa na maarifa ya kutosha kuhusu mafanikio ni dhahiri kwamba utapishana na fursa nyingi kwa sababu utakuwa unaziogopa kwamba huenda sio kweli. 

    Ni lazima uwekeze muda mwingi zaidi kwenye kutafuta maarifa ya kiuchumi. Sisemi uende chuoni ukasomee uchumi ninachosema unatakiwa upate muda mwingi zaidi wa kujifunza kuhusu uchumi na fedha. Kuna waalimu wengi sana siku hizi, google ni mwalimu wa kwanza anayeweza kukupatia maarifa mengi. 

Sipendi uwe kama yule mzee aliyeacha shamba la dhahabu akaenda mbali eti anatafuta dhahabu. Mzee yule hakuwa na maarifa ya kutosha kuhusu dhahabu.

0 comments: