Nakuchukua nafasi hii
kukukaribisha kwenye ulingo huu wa kujifunza maana kujifunza hakuzeeki, unatakiwa
kujifunza siku zote katika maisha yako. Kila kitu unachokiona kinakufundisha
jambo fulani, kama hujui kinakufundisha nini ni kwa sababu macho yako
hayajafumbuliwa upate kufahamu unachojifunza kutoka kwenye vitu hivyo.
Leo nakuletea makala hii kwa lengo la kukufumbua macho
yako na akili yako ili uweze kugundua kitu gani kinakukwamisha ili uchukue
hatua haraka kulitatua tatizo hilo na hatimaye uendelee vema na safari yako ya
kuelekea mafanikio makubwa.
Majaribu
ni nini?
Neno majaribu mara nyingi hutumiwa sana kwenye upande
wa dini, kuelezea hali ngumu inayompata mtu agharabu kwa lengo la kumjaribu
uimara wa imani yake. Kwa kifupi majaribu ni hali au kitu ambacho huwa mzigo
mzito unaomwandama mwanadamu. Huko kwenye dini tunaambiwa mtu anapojaribiwa na
akalishinda jaribu linalomsumbua hupewa thawabu na Mwenyezi Mungu kama tuzo ya
kufuzu mafunzo anayotaka Mungu amfundishe mtu huyo.
Katika makala hii, nataka tulizumgumzie neno majaribu
kuelezea magumu yote unayokumbana nayo wakati unapotaka kuelekea mafanikio yako
makubwa.
Kwa mfano, unataka uanzishe biashara yako lakini huna mtaji, umefanya
kila njia kutafuta mtaji lakini umekosa hilo ni jaribu moja wapo. Mfano mwingine
unasoma shuleni au chuoni lakini kadri
siku zinavyokwenda hufanyi vizuri darasani umejaribu kila mbinu lakini bado
huoni matumaini, hilo limeshageuka kuwa
jaribu lako.
Unaweza kuwa unafamilia yako lakini kutokana na hali ngumu ya maisha,
huna pesa na familia hiyo inahitaji pesa kwa kiwango kikubwa lakini bado huoni
mahali pa kutokea, hilo nalo limeshakuwa jaribu lako. Sio hayo tu na mengine
mengi magumu unayoyapitia labda kwenye swala la mahusiano na mwenzi wako,
uhusiano wenu umelegalega kwa siku nyingi uaminifu kati yenu umepungua na kuna
kila dalili za kusalitiana, nalo hilo limekuwa jaribu kwako.
Kama unamazingira kama hayo au yanakaribiana na hayo
basi somo hili ni lakwako. Tuendelee kujifunza na baada ya somo hili unaweza
kupata nguvu mpya ya kushinda majaribu yako.
Usipogundua
kama Tatizo Ulilonalo Ni Jaribu Huwezi Kushinda.
Wataalamu wa afya, kwa maana ya madaktari na wahudumu
wengine wa afya hawawezi kumpa dawa mgonjwa bila kujiridhisha ugonjwa anaoumwa
mgonjwa yule.
Mambo hayo hayaishii huko tu hospitalini lakini hata katika
maisha yetu ya kawaida bila kufahamu tatizo linalokusumbua sio rahisi
kulishinda tatizo hilo. Kwa kuongezea zaidi bila kugundua kama changamoto
uliyonayo ni jaribu huwezi kuishinda changamoto hiyo.
Dalili
Hizi Zinakusaidia Kutambua kama Changamoto Uliyonayo Ni Jaribu
Kwa kawaida sio rahisi kugundua changamoto uliyonayo
kama ni jaribu. Lakini ukitulia na kutafakari unaweza kufahamu kwamba
changamoto inayokubili ni jaribu. Dalili
tatu zifuatazo zinaweza kutumika kukukufahamisha kwamba changamoto
uliyonayo ni jaribu.
Dalili
ya kwanza: Kubwa mno huoni mahali pa kutokea, hakuna mtu wa
kukusaidia unakata tamaa na kunyong’onyea. Hii ni moja ya dalili kwamba
changamoto inayokukabili ni jaribu.
Dalili
ya pili: Umesumbuka kwa muda mrefu huitaki hali ile au swala
hilo lakini kila unapotaka kuishinda hali hiyo huwezi. Hii nayo ni moja ya
dalili kwamba changamoto inayokusumbua ni jaribu. Mfano inaweza kuwa ni tabia Fulani
mbaya kila unapojaribu kuiacha unajikuta umerudia tena na tena mpaka inafikia
hatua umekosa raha na hujui utatokaje.
Dalili
ya tatu: Chanzo chake sio wewe ni watu wengine, ndugu na jamaa
zako wa karibu ndio wanaokutesa kwa aina
moja au nyingine tena kwa muda mrefu. Ukiona hivyo ujue hilo linaweza kuwa jaribu
lako.
Umegundua
Jaribu Lako? Jiandae
Kama nilivyoanza kukueleza hapo juu, mgonjwa akienda
hospitali jambo la kwanza ni kujua ugonjwa anaoumwa ndipo apewe dawa sahihi ya
kutibu ugonjwa huo. Tukirudi kwenye somo letu, unapogundua kwamba changamoto
inayokukabili ni jaribu unatakiwa ujiandae. Ujiandae kufanya nini?, ujiandae kushinda
jaribu hilo.
Binadamu tumeumbwa kwa namna ya ajabu sana, unapogundua
tatizo linalokusumbua mara nyingi huwa tunapata nguvu na ujasiri wa kukabiliana
na tatizo hilo, tunapataje nguvu?, “ Tunapata nguvu kutoka kwenye kitu
kinachoitwa kujitambua “awareness” .
Don Miguel Ruiz anasema
katika kitabu chake The Mastery of Love , kujitambua “awareness” ni silaha ya
kwanza kushinda kila aina ya uongo na hisia mbaya.
Mfano ukiwa na “awareness” kama kuna mtu anakutukana ukitaka
kumrudishia kwa matusi hutaweza maana utakumbuka nikimrudishia kwa matusi kuna
kupigana au kujenga uhasama. Badala yake utakaa kimya. Lakini bila “awareness” lazima utamrudishia matusi na
maneno mengine mengi.
Umakini (awareness), ni silaha kubwa sana ya
kukupa uvumilivu na hekima ya kuamua vema kwa sababu ukiwa na “awareness” hutataka umkwaze mtu.
Lazima Ushinde Jaribu Lako.
Weka nia ya dhati ya
kushinda jaribu lako. Tumia “Umakini”ili usimkwaze mtu. Kumbuka unaposhinda
jaribu lazima upate tuzo. Soma kitabu cha Ayubu jinsi alivyopambana na majaribu
yake hadi akashinda na hatimaye akapewa tuzo kubwa. Soma kitabu cha Ayubu kwenye
biblia sura ya 1,2 na sura ya 42.
Jaribu Linapokushinda Unapoteza Kila Kitu.
Hata kile kidogo
ulichonacho kitapotea kama jaribu utaliruhusu likushinde. Usikubali kushindwa
na jaribu, pambana ulishinde halafu baada ya ushindi lazima utapata tuzo kubwa.
Ndio maana wajasiriamali wanaoshinda majaribu yao wanapewa tuzo ya kufanikiwa
kimaisha. Tunawaona wakiishi maisha mazuri ya utajiri mwingi. Ni kwa sababu
wanashinda majaribu yao. Nakuhimiza tena unapogundua jaribu lako, jiandae
kushinda jaribu hilo.
0 comments:
Chapisha Maoni