Ijumaa, 8 Aprili 2016

Tumia Kipaji Chako Kwa Faida Yako Na Ya Wengine


Lena Maria akiwaonesha wanachuo wa chuo cha SEKOMU jinsi anavyoandika kwa kutumia miguu yake.

Habari yako ndugu na rafiki yangu msomaji wa ukurasa huu, Hivi karibuni nimepokea jumbe nyingi kutoka kwa wasomaji wa ukurasa huu haswa wakitaka kumtambua zaidi mwanamama Lena Maria ambaye nilimtolea mfano kwenye Chapisho la 'Maisha Ni Kama Ujenzi Wa Kiota, Umejenga Chako?' kama bado hujaisoma basi bofya HAPA ili uisome.

Kutokana na hitajio hilo nimeona niweke Makala hii ili pia tujifunze namna ya kutambua na kutumia kipaji chako kwa kumuangazia mwanamama Lena, karibu,

Tatizo la wazazi wengi wanawasaidia kupita kiasi watoto wao.” Ni maneno ya mwanamama Lena Maria Klingvall kutoka Sweden, ambaye ni miongoni mwa waanzilishi na mfadhili wa chuo kikuu cha SEKOMU hapo nyuma kilikuwa kinaitwa SEKUKO kinachopatikana
Lushoto mkoani Tanga. 

Lena Maria ni mtu wa ajabu kwa sababu ameweza kuuonyesha ulimwengu kuwa hakuna binadamu aliye hai ambaye hana kipaji tena cha kipekee. Mama huyu hana mikono kabisa toka kuzaliwa kwake, zaidi ya hilo mama huyu ni mlemavu wa miguu ingawaje anaweza kutembea kwa kuchechemea.

Ulemavu wa Lena Maria haukumzuia hata kidogo kufanya kile kila binadamu mwenye viungo vyote anaweza kufanya. Anaweza kuendesha gari kwa kutumia miguu yake tena anaweza kuendesha gari kwenye majiji makubwa duniani kama vile Tokyo, mfano; ameweza kufanya ziara zaidi ya arobaini nchini Japan. 

Anaweza kuandika kwa kutumia miguu, anakula bila shida kwa kutumia miguu yake. Kama hiyo haitoshi Lena Maria ni mwimbaji mzuri sana na mwandishi wa vitabu. 

Hakuna kitu asichokiweza Lena Maria, aliwahi kuolewa ingawaje kwa sasa waliachana na mume wake kwa maswala mengine wala sio kwa sababu ya ulemavu wake.

Lena Maria ni mwogeleaji mashuhuri na ameshahi kushiriki kwenye mashindano ya Olympic huko korea ya kusini na alishinda medali mbili za dhahabu mwaka 1986.

Dunia Inahitaji Msaada Na Mchango Wako.
Lena maria amezunguka dunia nzima akiustajabisha ulimwengu kwa jinsi alivyoumbwa na kwa jinsi ambavyo udhaifu wake wa viungo haumzuii kabisa kufanya kila jambo ambalo watu wenye viungo vyote wanafanya. 

Amekuwa msaada mkubwa sana wa kuwahamasisha watu wote wajikubali na watumie fursa hii ya kuishi kufanya kazi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya ulimwengu. 

Hakuna mtu aliyemwona Lena Maria akajidharau tena au akajiona hafai. Wengi waliomwona Lena maria hutoka na ndoto mpya maishani mwao maana hakuna aliyewahi kuamini kuwa mwanamama huyu anaweza kufanya maajabu yote hayo.

Mwaka 2010 alitembelea chuo cha SEKOMU kilichopo wilayani Lushoto mkoani Tanga, alipata fursa ya kuongea na wanachuo aliwaonesha kila jambo analoweza kulifanya kwenye maisha yake akianza na kuimba, kuandika na kila neno aliloona vema kulisema alilisema. 

Dunia ya chuo cha SEKOMU haikuamini maajabu ya mtu huyu kila mtu alitoka ana nguvu mpya na kila mtu alimshukuru Mungu kwa kuwa yeye ni mzima namna ile. 

Baadhi ya wanachuo walikimbia kanisani kwenda kutubu kwa sababu waligundua kuwa kumbe wanakila kitu halafu wanasingizia na  hawatumii zawadi ya kuwa na viungo vyote  ipasavyo..


Kipato Cha Lena Maria
Ulemavu wake ndio mtaji mkubwa na ndio fursa pekee inayomfanya Lena maria azidi kuwa tajiri. Mfano alipokuwa Japani alialikwa kwenye matamasha zaidi ya miamoja na kila alipokuwa anaalikwa alikuwa analipwa. 

Kule Korea aliweza kuhojiwa na watu wengi kwenye vituo mbalimbali vya redio, magazeti na luninga. Kote huko amejipatia fedha nyingi na anaendelea kujipatia fedha nyingi kila siku.

Mama huyu alipotambua kuwa ulemavu wake ni fursa inayoweza kuwatia nguvu wale waliokata tamaa, tangu hapo akaanza kuzunguka dunia nzima akitoa misaada kwa watu mbalimbali na hatimaye alipata nafasi ya kufika chuo kikuu cha SEKOMU ambapo alichangia maendeleo ya chuo hiki kwa fedha nyingi.  

Tunadeni kubwa la kulipa sisi tuliojaliwa viungo vyote kwa ajili yetu wenyewe na kwa ajili ya kuwasaidia watu wengine.

Kipaji chako na thamani yake iko katika mambo yafuatayo;-
    a)  Kipaji chako kimefichwa katika udhaifu wako.
Ni hivi, udhaifu (kupungukiwa) kwako ndipo kipaji chako kilipo. Maana yake ni hii mtu anapokuwa anahisi kupungukiwa kitu fulani ndipo anapata hamu au kiu ya kutaka kukipata kitu hicho na kadri anapojitahidi kukipata kitu anachokitaka, watu huku nje tunaona halafu tunaanza kusema aisee fulani ana kipaji kizuri sana cha kucheza mpira au kuimba au kuchora na kadharika. 

Mwl Nyerere anapata sifa kila kona kwamba alikuwa kiongozi shupavu na mwenye maono hii ni kwa sababu alikuwa na mapungufu (udhaifu) mwingi ambao kila siku alikuwa akiamka anajisikia hana amani anajiona amepungukiwa vitu vingi kwahiyo akawa anajitahidi kupata kila anachokitaka, matokeo yake sisi tunamwona anakipaji cha kuongea na kuongoza.

Jichunguze unaudhaifu (mapungufu)  gani kisha fahamu kuwa upungufu ulionao ndimo kipaji chako kimefichwa. Tumeona Lena Maria kwa kutokuwa na mikono na ulemavu wa miguu ndimo kulimo fichwa kipaji chake sasa dunia inamshuhudia mwanamama huyu kama mtu wa ajabu. Tumia udhaifu wako kusonga mbele.

b) Kinachowafanya watu wengine wapate nguvu na wafurahi ndicho kipaji chako.
Kipaji cha mtu hakijifichi, huonekana mapema sana na wewe mwenyewe ni rahisi kujua kipaji ulichonacho. 

Kitu kinachowafanya watu wafurahie uwepo wako au/na wapate nguvu na kuhamasika zaidi unapokuwa kati yao hicho ndicho kipaji chako. Kinachotakiwa sasa jifunze namna ya kutumia kipaji hicho na ukiendeleze zaidi kwa faida yako na kwa faida ya watu wengine.

Mfano, kama wewe ni mwimbaji kila ukiimba watu wanafurahia zaidi na wanahamasika zaidi katika uimbaji wako hicho ndicho kipaji chako, unachotakiwa kufanya ni kukiboresha zaidi kipaji hicho. Kama wewe ni mwandishi kila unapoandika kitu watu wanaguswa zaidi na wanafurahi zaidi basi ujue kipaji chako ni kuandika jifunze mbinu zaidi za kuandika unaweza ukawa mwandishi mashuhuri na mhamasishaji mzuri.

         c) Udadisi kidogo tu na kujaribu kunaibua kipaji chako.
Wakati mwingine unaweza usiweze kugundua kipaji chako kwa kuangalia udhaifu wako na kwa kuangalia kile watu kinawapa nguvu au furaha kutoka kwako. Kuna njia kabambe ya kufahamu kipaji ulicho nacho. 

Njia hii ni kujidadisi wewe mwenyewe na kisha kujaribu kila jambo unaloweza kulifanya ili mradi tu usivunje sheria. 

Mfano kuna kipindi nikiwa nyumbani nilikuwa na kiu sana ya kulima mpunga lakini sikuwa na nyenzo za kulimia ikiwa ni pamoja na zana za kilimo. Niliwaza sana namna ya kuweza kupata zana hizo hatimaye nikaja na wazo la kutengeneza trekta dogo kwa kutumia gia za injini ya gari. Nilianza kuchonga mbao, gia nilileta kutoka Sumbawanga mpaka nyumbani Tabora.

Baada ya udadisi na kujaribu niliweza kufahamu kuwa kumbe ninakipaji fulani ambacho watu wengi walikuwa hawana. Kwahiyo hata na wewe ndugu unao uwezo wa kujidadisi na kujaribu, muda sio mrefu utajifahamu vizuri.

Lena Maria kilichomfanya afahamu kipaji chake na akakitumia vizuri ni kujaribu kwa kila jambo hakutaka kabisa kusaidiwa kila kitu maana alikuwa anafahamu kuwa wakati mwingine msaada unalemaza akili ya kufikiri.

Ni vizuri kwanza kujaribu kwa juhudi zako kabla hujakimbilia kupata msaada. Ndiyo maana kwa wenzetu huko katika nchi zilizoendelea watu wengi hawataki msaada maana wanaamini kusaidiwa ili hali unazo nguvu na akili timamu ni kudharirishwa. 

Sisemi kupewa msaada ni vibaya hapana maana kunategemea na aina ya msaada, kuna msaada wa ushauri, wa matibatu nk, lakini msaada wa kupewa kila kitu sio mzuri kwa sababu unalemaza akili na kubaki wategemezi.

 “Ni vizuri kwanza kujaribu kwa juhudi zako kabla hujakimbilia kupata msaada



0 comments: