Jumamosi, 16 Aprili 2016

Mambo 3 Ya Kuanzia Ili Ufikie Mafanikio Ya Juu Zaidi.

 
Wakati natafakari maisha jinsi yalivyo na wakati natafakari ufahari wa mwanadamu hapa duniani, ndipo nilipopata kuelewa kwamba maisha ni kama maigizo ni kama uchekeshaji vile. Kwanini nasema hivyo? 
 
Nasema hivyo kwa sababu usipoangalia kwa makini unaweza kuishi kwa kujisahau jinsi ulivyo badala yake ukaishi kwa taswira ya dunia ambayo taswira ya dunia sio kitu halisi bali ni taswira tu au mtazamo tu. Ndiyo maana nikapata kanuni rahisi ya maisha kwamba maisha yote hapa duniani is a game yaani ni mchezo kama  ilivyo michezo tunayoifahamu hivi sasa.

Najua hujaelewa ninachosema, ngoja nikupe mfano; kuna wakati nilipokuwa ndogo nilikuwa naishi kwa taabu sana kwa sababu nilikuwa najiona mimi ni mfupi na mwembemba zaidi kuliko wenzangu,  kila siku nilikuwa najilinganisha na wenzangu na nilijiona mimi ni mdogo zaidi. Niliishi kwa unyonge sana kipindi hicho sikuwana uhuru wa kusimama na kujidai mbele ya wenzangu.

Iko mifano ya namna hiyo mingi;  nimekutana na watu wanajiita wazuri wa sura au walembo, mara nyingi hujivunia sura yao nzuri na jinsi wanavyofuatwafuatwa na watu maarufu kwahiyo watu hao huringia uzuri wa sura zao nzuri. 
 
Baadaye nikagundua kuwa kumbe mtu anayeringia na kujivunia uzuri wa sura au urembo mpe muda, ndiyo mtu yeyote anayeringia uzuri wa sura yake au maumbile yake mpe muda,  anza kumpa miaka 5  kisha njoo umtazame uone uzuri wake ulivyo  kisha mwongezee  miaka mingine 5 halafu njoo tena umtazame uzuri wake, utagundua kuwa kumbe uzuri wa sura na umbo zuri ni taswira ya dunia hii taswira yenyewe si kweli bali ni uongo. 
 
Tangu kipindi hicho nilipogundua falsafa hii sihangaiki tena na maumbile yangu wala sithubutu kujilinganisha na mtu yeyote,  jinsi nilivyo najifurahia sana.

Kilichonishangaza Zaidi
Katika pita pita yangu nimekuja kuona mambo ya kushangaza, mtu mzuri wa umbo na sura nzuri lakini eti ni kichaa au ni mwizi au akili zake zimeshft kidogo au ana hali ngumu isiyoelezeka au sio maarufu kama watu wengine.  Jumla ya yote hayo ni kwamba sura au umbile la mtu halina nafasi katika mafanikio yake hata siku moja. Kwa maana nyingine kufanikiwa kwako hakutegemei mwonekano wako kunategemea mambo haya matatu tunayoenda kuyaangalia hapa chini ambayo ni LAZIMA uwe nayo ili uweze kufanikiwa kwa kiwango cha juu zaidi.

Jambo La 1: Wekeza Kwenye Viungo Vyako
Mwl Nyerere tunamshukuru na kumuenzi vizazi na vizazi si kwa sababu alikuwa handsome au kwa sababu alikuwa baunsa ni kwa sababu aliwekeza kwenye KINYWA CHAKE. Tofauti ya Mwl Nyerere na mimi iko katika maneno yetu. Alitumia muda mwingi kukifundisha kinywa chake kijue namna ya kuongea na akafanikiwa,  sasa amekuwa akisema na sisi Watanzania kwenye kila hatua ya maamuzi ya kitaifa. Wanasiasa wote wanawekeza katika vinywa vyao. Wanamuziki wanawekeza katika vivywa vyao wahubiri na watumishi wa Mungu wanawekeza katika vivywa vyao. 
 
Bahati nzuri huhitaji mtaji mkubwa kuwekeza katika kinywa chako kinachotakiwa ni wewe kuamua na iwe sehemu ya shauku (Passion) au Hobby yako. Kwa kufanya hivyo tu mafanikio  unayavutia kwako. Kuwekeza katika kinywa kuna muunganiko wa viungo vingine baadhi ya viungo hivyo ni kichwa na moyo.

Watu wengi zaidi maarufu na waliofanikiwa duniani wamejifunza kuwekeza katika viungo vyao pekee. Wapo waliowekeza katika miguu yao sasa ni wachezaji maarufu na wanamafanikio makubwa. Je, wewe ndugu yangu unayesoma makala hii umewekeza katika kiungo gani cha mwili wako? Ukiniuliza mimi hilo swali nitakujibu kwamba mimi nawekeza katika kinywa na mikono yangu. 
 
Ili niwekeze katika kinywa,  mara nyingi sana nasimama mbele ya watu na kuzungumza na watu, kila jukwaa ninalopata nafasi nalitumia kuongea ni matumaini yangu kwamba baada ya muda si mrefu nitafanya mambo makubwa kwa ajili yangu na taifa langu kwa ujumla. Natumia mikono yangu iniletee faida. Ngoja tuliagalie hili kwenye jambo ya pili hapa chini.

Jambo La 2: Jiweke Mwenyewe Kwenye Historia Kwa Faida Yako Na Vizazi Vijavyo.
Moja ya mambo yananyonishangaza ni pale ninapoenda kwenye maduka ya vitabu au maktaba ya vitabu. Asilimia 80% ya vitabu vimeandikwa na watu wa mataifa mengine. Vitabu vichache sana vimeandikwa na watanzania. Natafakari sana je sisi Watanzania hatuna cha kuandika? Kwanini wao tu ndio wawe wanaandika wakati mimi na wewe tupo tu. Nataka nikwambie mikono yako unaweza kuitumia kukuingiza kwenye historia. 
 
Vitabu tunavyofurahia vya neno la Mungu vimeandikwa na watu kama mimi na wewe walipopata uvuvio wa Mungu wakaandika vitabu hivyo, kwani wewe na mimi hatupati uvuvio wa Mungu? Kwanini usitumie maisha yako hapa duniani kuacha nyayo za kuwafundisha wengine jinsi ya kuishi? Kwanini watu wengi zaidi wasibarikiwe kwa kuwepo kwako hapa duniani? Kwanini mikono yako usiitumie kama silaha ya kukuletea mafanikio yako  kwa vizazi vyako?. 
 
Unahitaji mtaji kiasi gani ili uanze kuandika vitabu vya kuufundisha ulimwengu?. Ni dhahiri kwamba hujaamua au huoni umuhimu wake. Ni nia yangu kukujengea ari na kiu uanze kubadili fikira zako kisha ujiweke kwenye historia wewe mwenyewe.

Jambo La 3: Ongeza Kipato Chako Kwa Kuanzia Kanuni Rahisi Hadi Ngumu.
Pesa inawafurukutisha watu ulimwenguni kote. Mimi na wewe tunatamani tuwe na pesa nyingi iwezekanavyo. Kibaya zaidi badala ya kutafuta pesa kwa kutumia mbegu iliyoweka ndani yetu ya kutuletea pesa, watu wengi wamekuwa wanaruka ruka huku na huku ili tu wapate pesa. Lakini kwa umri wangu nilioishi hapa duniani nimeanza kugundua kwamba kupata pesa ni rahisi sana ukitumia hobby na passion yako. 
 
Mtu anayekwepa kutafuta pesa kwa kutumia hobby na passion yake maisha yake huwa magumu zaidi. Kuna dada mmoja kutoka Uganda anaitwa KANSIIME yeye ni comedian amenivutia sana kwa kazi yake hiyo ya kuigiza. Hakuanza na mtaji bali anachotumia ni kinywa chake tu kutengeneza pesa. Maisha kwake ni rahisi anafurahia jinsi alivyo,  pesa anaivuna kwa njia naweza kuisema nyepesi ukilinganisha na njia nyingine. Hobby yake ameibadilisha kuwa pesa. Kwani wewe unashindwa kuibadilisha hobby yako iwe pesa?

Chukulia kwa mfano unapenda kuangalia mpira wa miguu. Hiyo ni hobby yako kwanini usiibadilishe iwe pesa?. Unachotakiwa kufanya  ni kujenga ukumbi tu tena hata kama ni wa maturubai kisha nunua luninga yako kubwa weka na bechi anza kuonyesha mpira. Ukiandaa mazingira vizuri utapata wateja wengi sana kisha utapata pesa nyingi. Kingilio kinakuwa ni kinywaji unachouza. Mfano unakuwa unauza soda au vinywaji vingine kwahiyo kila mtu anayekuja kuangalia mpira sharti anunue kinywaji na aingie kuangalia. Utapata wateja wengi watakaokuja kwako maana mtu ataona ni bora aje kwako anunue kinywaji badala ya kuilipia hilo pesa kama kiingilio.

0 comments: