Leo katika makala yetu tunakwenda kuangalia dhana muhimu sana ambayo wote tunatakiwa kuielewa kuhusu maisha yetu ya kila siku. Japokuwa tunaijua dhana hii, lakini bado hatujaielewa kwa undani na hivyo kushindwa kuwa na maisha bora na yenye furaha.
Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna kisichokuwa na mwisho kwenye maisha yetu. Tukianza na maisha yetu yenyewe, yana mwanzo ambapo ni siku tunayozaliwa na yana mwisho ambapo ni siku tunayokufa. Hiki ni kitu ambacho kila mmoja wetu anajua. Lakini kujua tu hivyo haitoshi, bali kuna mengi ya kujifunza hapo ili kuwa na maisha bora na yenye furaha.
JAMBO LA KWANZA; Furaha haipo
mwishoni.
Kwa kuwa kila kitu kina mwanzo na mwisho, basi tumejijengea fikra kwamba tutakapofika mwishoni ndiyo tutakuwa na furaha sana. Kwamba tukishapita yote na kufikia mwisho, tutafurahia sana.
Hivi ndivyo tunavyofikiri kwenye elimu, kwamba siku unayohitimu masomo yako basi unakuwa na furaha sana. Na tunafikiri hivyo kwenye kazi pia, kwamba siku unayostaafu kazi basi utakuwa na furaha isiyo na kifani.
Lakini baada ya kufikia mwisho ndiyo tunagundua ya kwamba furaha haikuwa mwishoni bali ilikuwa kwenye mchakato mzima.
Siku utakapofikia mwisho wa maisha yako, siyo siku ambayo utakuwa na furaha, bali itakuwa siku ambayo unayaangalia maisha yako yote, jinsi ulivyoyaishi na ndio utagundua kama ulikuwa na maisha ya furaha au la.
Kuliko kusubiri mpaka siku ya mwisho ndiyo uje ugundue kama ulikuwa na furaha au la, kwa nini usianze leo, kwa nini usichague leo kuishi maisha yenye maana kwako ambayo ndiyo yatakayokuletea furaha. Kwa sababu kusubiri mpaka siku ya mwisho utapoteza sehemu kubwa ya maisha yako.
JAMBO LA PILI; Changamoto zina mwisho, lakini somo halipo mwishoni.
Kwenye maisha yetu tutakutana na changamoto mbalimbali. Lakini uzuri wa kila changamoto ni huu, kila changamoto ina mwisho wake. Hakuna changamoto itakayodumu na wewe milele, labda wewe mwenyewe uamue kuiganda changamoto hiyo.
Kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha ina mwisho wake. Hata kama ni kubwa na ngumu kiasi gani, itafika wakati changamoto hiyo itakwisha. Iwe utaifanyia kazi au hutaifanyia kazi, itafika mwishoni.
Kitu kingine muhimu sana kujua kwenye changamoto ni kwamba tunajifunza wakati wa changamoto na siyo mwisho wa changamoto. Ule wakati ambao tunapitia changamoto ndiyo wakati ambao tunajifunza mambo mengi sana. Tunajifunza kuhusu changamoto zenyewe za maisha, na pia tunajifunza kuhusu sisi wenyewe. Ni kwa kiasi gani tunaweza kuhimili changamoto, ni maeneo gani tupo imara na yapi tupo dhaifu. Tunajifunza pia kujijengea uvumilivu na kutokukata tamaa.
Hujifunzi mwishoni mwa changamoto, bali unajifunza wakati unaipitia changamoto hiyo.
JAMBO LA TATU; Maumivu yana mwisho.
Hakuna maisha ambayo hayapitii maumivu, lakini kitu kizuri sana ni kwamba hakuna maumivu yasiyokuwa na mwisho. Kwa asili kila maumivu yana mwisho, na maumivu makali yanadumu muda mfupi huku maumivu yanayodumu muda mrefu yanaweza kuvumilika.
Hivyo haijalishi ni maumivu gani ambayo unapitia kwenye maisha, yana mwisho wake, hayataendelea kuwa na wewe milele. Hivyo kikubwa ni kutokukata tamaa na kuendelea kufanyia kazi kile ambacho kinakuletea maumivu.
Usione maumivu yoyote unayopitia kama ndiyo mwisho wa dunia kwako, bali jua ya kwamba ni sehemu ya maisha na haitachukua muda mrefu kabla hayajafikia mwishoni. Na pia wakati unapitia maumivu ni wakati ambapo unajifunza mengi sana kuhusu maisha.
Kitu chochote unachopitia kwenye maisha, kiwe kizuri au kibaya hakitadumu milele, kwa sababu hata maisha yako yenyewe hayatadumu milele. Hivyo ni vyema ukatumia vizuri kila kitu unachopitia, kama ni kufurahia ukifurahie na kama ni kujifunza ujifunze. Uzuri wa maisha haupatikani mwishoni, bali vile tunavyoishi kila siku ya maisha yetu.
Mkusanyiko wa siku zetu ndiyo maisha yetu, hivyo usisubiri mpaka mwisho ndiyo ufurahie, bali anza kufurahia sasa na unapofika mwishoni tayari unakuwa umeyafaidi maisha.
Nakutakia kila la kheri katika kutengeneza falsafa mpya ya maisha, ambayo itakujengea maisha bora na yenye furaha na mafanikio.
0 comments:
Chapisha Maoni