Ijumaa, 8 Aprili 2016

Wafalme Hupigana Kwa Ajili Ya Himaya, Vichaa Hupigana Kwa Ajili Ya Sifa


 
Umekwisha wahi kuona? Mtu anag’ang’ana kufukazana na vijimambo vidogo vidogo tu mtaani wala hakuna kinachoeleweka. Ndio! watu hao wapo wengi tu,  wao ni wachambuzi wa kila neno litokalo vinywani mwa wengine. 
Ni wataalamu waliobobea kuhakikisha hawakosi sifa mtaani, kijiweni, ofisini, shuleni, chuoni, gengeni na kila sehemu walipo. Ingekuwa heri kama sifa hizo ni za mambo mema , rakini mara nyingi ni yale yasiyofaa hata kutamkwa.  Wanaweka sifa pasipohitaji sifa.

Ukitambua Chagua Njia Yako
Nataka nikuhimize uchague njia yako mwenyewe ya maisha, jiamulie wewe mwenyewe njia utakayopitia. 
Usiige mtu fanya kile ukipendacho. Nikijichukulia kwa mfano mimi, kufundisha ni kitu ninachokipenda sana. Sipendi kuajiriwa kama mwalimu wa shule lakini napenda
kufundisha kwa namna yoyote ile. Najisikia raha sana ninavyoandika makala hizi za kuwahamasisha watu wachukue hatua kuelekea mafanikio yao. Hii ni njia niliyoichagua mimi. 
Usijaribu kuniiga ikiwa siyo njia yako vinginevyo iwe ni moja ya njia ulizokuwa umezichagua kufuata.

Kichwa Cha Habari
Wafalme Hupigana Kwa Ajili Ya Himaya, Vichaa Hupigana Kwa Ajili Ya Sifa. hayo ni maneno ya mwandishi mashuhuri wa mashairi kutoka Uingereza anaitwa John Dryden. Anatupatia picha halisi ya kile kinachoendelea katika jamii yetu. 
Nimekutana na baadhi ya watu ambao kutokana na fursa walizozipata, huwezi kumwambia chochote. Utakuta mtu sio kwamba hapambani bali  anapambana sana kwa ajili ya maisha yake yamkini na kwaajili ya maisha ya watu wengine wanaomzunguka. 
Tatizo ni njia ipi anayotumia kupambana huko?. Zamani ilionekana ukiwa mwalimu kila mtu mjini na kijijini atakusalimia kwa heshima “shikamoo mwalimu”; lakini siku hizi ukiwa mwalimu unaogopa hata kusema kama wewe ni mwalimu. Unafikiri ni kwanini? 
Sio kwa sababu ualimu hauna heshima wala sio kwa sababu kuwa mwalimu sio njia sahihi ya kupambana! Hapana bali kinachotokea akilini mwa watu wengi kulingana na maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa fursa duniani, watu wengi wameanza kubadili mawazo yao na kuanza kuona kwamba kuajiriwa ni njia mojawapo ya kuanzia maisha nasio njia ya kukufanya uwe tajiri.
Ninachotaka kusema ni kwamba, kuajiriwa tu halafu ukabaki unajisifia kwamba wewe ni mtumishi wa Serikali na unacheo kikubwa na kwahiyo yoyote na yeyote anayekushauri wa chini yako unaona kama anakushauri upuuzi na unapotezea halafu unakomaa kusubiri “Pension yako” na unajiona uko sahihi kabisa, hiyo ndiyo aliyoisema John Dryden kwamba “Wafalme Hupigana Kwa Ajili Ya Himaya, Vichaa Hupigana Kwa Ajili Ya Sifa”.

Unahitaji Neno Moja Tu
Imewahi kutokea kwako?  
Siku moja ukaamka unahuzuni moyoni na hupati picha jinsi utakavyo vuka changamoto za maisha zinazokukabili. Ukafanya kila njia ya kukufariji na kukufanya upate ahueni lakini hukupata ahueni hata kidogo. 
Ukawasha mziki wa kila aina uupendao lakini mziki unaonekana kama mziki wa “waswezi”(hawa ni watu wanaofanya sherehe za matambiko huko Unyamwezini na usukumani),yaani kwa kifupi mziki haupandi. 
Je haijahi tokea wakati ukiwa katikati ya mawazo magumu namna ile halafu ukasikia sauti au neno  moja  au ukasoma sehemu halafu gafla kila kitu kimefunguka, furaha inarudi unapata nguvu japo shida iliyokuwa inakusumbua bado haijaisha? Je, hali hiyo haijawahi kutokea kwako? Kwanini ulipata furaha katikati ya shida nyingi zikiwa bado zinakukabili?

Kwanini Unaenda Kusali?
Sijui kwa upande wako lakini mimi imetokea mara nyingi kama sio kila siku, nikienda Kanisani kusali kuna neno moja hunigusa kuliko maneno mengine na kunifanya nifikiri upya juu ya msimamo wangu wa maisha. Kuna maneno mengi sana huzungumzwa Kanisani au Msikitini lakini katika yote hayo neno moja tu ndilo litakalokugusa na kukufanya uanze kuishi maisha mapya ndani ya nuru uliyoipata kwenye ibada. Kama unafikiri nasema uongo nisamehe bure.
Kwanini usingekuwa unabaki nyumbani tu ukachukua kitabu chako cha dini ukajisomea?. Jibu ni rahisi sana kitu kipya husisimua ubongo wako na kuongeza umakini. Unahitaji mtu mwingine aseme kwa ajili yako ili kuamsha akili na ari ndani yako. Ukitaka kuwa kichaa kama alivyosema bwana John Dryden funga mlango wako wa ndani wa kusikia. Maneno yote mzuri yatakuja lakini yatakuta mlango umefungwa hayataingia moyoni mwako na matokeo yake utakuwa unajiona uko vizuri kumbe ni kichaa.

Tunafahamu Unajua Mambo Mengi Lakini….
Hatutaacha kusema na wewe na wala hatutaacha kukuandikia makala au hatuaacha kuwasiliana na wewe kwa njia yoyote ile. Kwanini tuwasiliane na wewe mara kwa mara kwa njia ya makala, semina, simu au hata ana kwa ana?
JIBU: Tunafahamu kwamba unahitaji neno moja tu ili likutie nguvu kuelekea mafanikio yako. Maadamu umeamua kufikia mafanikio makubwa ya kiuchumi  neno letu moja litakusaidia sana. Tunafahamu kunachangamoto nyingi za kimaisha,  huenda kuna kitu kimekutoa kwenye mstari wa kuelekea mafanikio makubwa, kwa kupitia makala zetu huenda kuna neno litakugusa na kufungua upya nia ya kusonga mbele kuelekea mafanikio yako.
Usiache kusoma makala hata kama ina kichwa cha habari kisichobeba mvuto kwako mimi nakushauri jilazimishe uisome makala yote huenda kuna neno moja au ushauri utakugusa sana halafu utapata wazo jipya au mbinu mpya ya kusonga mbele. We need to be rich”

Glasi Iliyojaa Maji Inahitaji Kuongezwa Ukubwa Ili Ibebe Maji Mengi
Kwa kujifunza kutoka kwa watu mbalimbali hasa waliofanikiwa duniani nimepata kuelewa kwamba, unaweza kujiona uko vizuri kumbe wewe ni glasi iliyojaa maji. Hata tone moja likiongezwa kwenye glasi hiyo,  matone mwili au matatu yatamwagika chini. Maana yake kuna mahali akili zetu na mioyo yetu inakuwa glasi iliyojaa maji. Hata aje mtu wa aina gani akwambie kuna fursa nzuri ya kufanya wala hushituki wala hakuna hamu ya kumsikiliza wala hujali kabisa,  wakati maisha magumu yanakugonga. Hii ni dalili kwamba wewe ni glasi iliyojaa maji. Huhitaji kujua jambo jipya umeridhika na mbinu unazotumia au unazofikiria huhitaji kujua mbinu nyingine. Mimi nasema kufanikiwa kwako kutakuwa kwa shida sana.

Baada ya kugundua kwamba kumbe mtu anaweza kuwa glasi iliyojaa maji, mimi nilikataa katu katu,  kwamba sitaki kuwa glasi iliyojaa maji. Kwa sababu hiyo nikaifundisha akili na moyo wangu lazima utengeneze glasi kubwa ambayo haitajaa maji. Ndivyo nilivyo mpaka sasa,  kwangu kujifunza sifikirii kama nitamaliza kesho au mwaka kesho au miaka kumi ijayo sifikirii hivyo hata kidogo, kujifunza kwangu ni siku zote na wakati wote maadamu niko hai.

Kwa kujizoeza hivyo akili na moyo wangu siku zote usiku na mchana unahamu ya kujua mambo ambayo siyajui. Nikisikia kesho kuna semina ya ujasiriamali moyo unatamani na  akili inakusanya akili zake ili iweze kusikia kwa makini na kuengeneza taswirw ya kile ninachokisikia pia inaandaa umakini wa kusikiliza maana nahitaji neno moja tu nisonge mbele. 

Sijafika mbali lakini kasi ni nzuri sana,  imani yangu siku moja nitafika mbali. Sijaamua kusafiri pekee yangu tu kuelekea mafanikio makubwa nataka kwenda na kila mtu aliye na mzigo ndani yake wa kufikia mafanikio makubwa. Ndio maana nakutumia makala hizi ili tusonge mbele.

Kanuni Ya 20% Kwa 80%
Hii ni kanuni ya ulimwenguni kote kwamba 20% wa watu katika idadi ya watu fulani ni matajiri na 80% ya watu katika idadi hiyo hiyo ya watu ni maskini. Wewe ungependa kubaki kwenye 80%? Kama unabaki huko endelea kubaki mimi nimeshagoma. Ukiweza na wewe kugoma, goma na weka msimamo wa kuhamia kwenye 20%. Imetosha kwa leo.

0 comments: