"Mbio za sakafuni huishia ukingoni", huu ni usemi wa wahenga ambao una ukweli halisi. Kwa sababu kila sakafu ina ukingo, unapokimbia kwenye sakafu ukifika kwenye ukingo wa sakafu mbio zimeishia pale.
Maisha yetu ni mbio za sakafuni, kwa sababu kila mmoja wetu anajua kwamba hatoishi milele, siku moja wote tutakufa, na wala siyo mbali kama tunavyofikiri. Miaka 100 ijayo wote tunaosoma hapa sasa hivi tutakuwa tumeshakufa, mbio zetu zitakuwa zimefika ukingo wa sakafu yake.
Sasa swali moja muhimu sana kujiuliza ni je mbio za sakafu yetu zitaishia kwenye ukingo wa sakafu au zitaendelea? Hili ndiyo tutakalojadili kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha.
Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Ni imani yangu kwamba uko vizuri na una
endelea kuyaendesha maisha yako kwa falsafa mpya, na pia unapata matokeo bora kulingana na falsafa yako hiyo. Ni muhimu kuyajenga maisha yetu kwenye falsafa, ili kuwa na kitu tunachosimamia kwenye maisha yetu.
Kumbuka mtu ambaye hana cha kusimamia ataangushwa na kitu chochote.
Mbio za sakafuni huishia ukingoni, lakini sisi ndiyo tunaweza kuchagua kama mbio zetu ziwe na ukomo pale tunapofika mwisho wa sakafu au mbio hizo ziendelee hata baada ya ukingo wa sakafu.
Kama tukiyachukulia maisha yetu kama mbio na muda wetu wa kuishi kama sakafu, tunapofika mwisho wa muda wetu wa kuishi, mbio zetu zinakuwa zimeishia pale. Hii ina maana kwamba unapokufa maisha yako yanakuwa yamefika mwisho wake. Lakini siyo watu wote ambao maisha yao yanakuwa yameishia pale, wapo ambao wameendelea kuishi hata baada ya maisha yao kufika ukingoni.
Hawa ni watu ambao walifanya mambo makubwa kwenye maisha yao na siyo tu kusukuma siku. Hawa ni watu ambao walikuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine na hivyo kuacha alama ambayo wengine waliendelea kuikumbuka hata bila ya wao kuwepo.
Je wewe unataka nini? Unataka maisha ambayo yataishia ukingoni au ambayo yataendelea kuwepo hata baada ya wewe kuondoka duniani?
Uzuri ni kwamba uchaguzi upo mikononi mwetu, tunayo nguvu ya kuchagua mbio zetu ziishie wapi, japo siyo rahisi lakini inawezekana.
Wengi wetu tumechagua sakafu ambayo tunaikimbilia humo kila siku, sakafu hii tumeikariri na hatujawahi kupiga hatua ya ziada kuondoka kwenye sakafu hii.
Kuna wengi ambao wanafanya shughuli zao kwa mazoea, wakiamka wanakwenda kwenye kazi zao, wanazifanya kama walivyofanya jana, wakisubiri muda uishe na waondoke kwenye kazi hizo. Muda ukiisha wanakwenda kufanya kile walichozoea kufanya huku wakisubiri siku nyingine kuanza tena mzunguko. Wakati mwingine watu wamekuwa wakisema wazi kabisa ya kwamba tunapoteza poteza muda hapa.
Kuna wale wachache ambao wanaelewa kwamba maisha ni zaidi ya wao kupata kile wanachotaka, maisha yanahusisha wale wanaowazunguka na jamii kwa ujumla. Watu hawa huenda hatua ya ziada na kufanya mambo ambayo yatawawezesha wengine kuwa na maisha bora zaidi. Watu hawa huchukua hatua hizi hata kama wao haziwanufaishi lakini zinawanufaisha wengine.
Unaweza kuishi maisha ya kujiangalia wewe mwenyewe tu, au wewe na wale wa karibu kwako. Na maisha yako yakaenda vizuri sana, bila ya shida yoyote. Lakini safari yako hapa duniani itakapofikia tamati, hutaacha alama kubwa. Unaweza kuishi maisha ya kuangalia ni namna gani jamii inayokuzunguka inaweza kunufaika kupitia wewe, na ukawa na maana kubwa ya maisha yako pia kuacha alama kubwa unapoondoka.
Kila mmoja wetu ana nafasi ya kugusa maisha ya wengine, kuwafanyia wengine kitu ambacho hawawezi kuwalipa, kwenda hatua ya ziada katika kuhakikisha maisha ya wengine yanakuwa bora zaidi. Haya ndiyo yanayowatofautisha wale wanaoishi milele na wale wanaosahaulika haraka sana baada ya kuondoka duniani.
Muda wetu wa kuishi hapa duniani ni mfupi sana ukilinganisha na umri ambao dunia imekuwepo. Tukiweza kutumia muda huu vizuri tunaweza kufanya mambo makubwa kwetu na kwa wale wote wanaotuzunguka.
Watu wengi wamekuwa waifikiri labda wakipata madaraka au fedha ndiyo wanaweza kugusa maisha ya wengine. Lakini nikuambie ukweli kwamba kama wakati huna madaraka au fedha huna msukumo wa kugusa maisha ya wengine, madaraka au fedha haviwezi kukufanya wewe uguse maisha ya wengine. Fedha na madaraka yanaonesha kile kilichopo ndani yako, havikubadilishi.
Amua sasa kuishi maisha ambayo yanagusa maisha ya wengine, na huhitaji kuanzia mbali, bali anza kwenye kile unachofanya ili kujipatia kipato, anza kuwajali zaidi wale ambao unawahudumia, wape huduma bora, jiweke kwenye viatu vyao na jiulize ni kipi ambacho ungependa ufanyiwe kwa kuwa kwenye hali kama zao.
Tusikubali kuishi maisha mafupi ambayo yatasahaulika pale tu tunapoondoka duniani, badala yake tuguse maisha ya wengine, na maisha yetu yaendelezwe hata pale tunapoondoka duniani. Kila unachofanya, kuna ambao unawahamasisha kuchukua hatua, hivyo unapoishi maisha ya kuwajali wengine, kuna watu unawahamasisha nao kuwajali wengine.
Tuishi maisha yenye maana kwetu na kwa wengine pia. Tuguse maisha ya wengine kupitia kile tunachofanya.
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea falsafa mpya ya maisha yako, usikubali kuishi maisha yasiyoongozwa na falsafa.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.
0 comments:
Chapisha Maoni