Zipo sababu nyingi na ushahidi mwingi wa kisayansi, unaonyesha kuwa,
ndoa na mimba katika umri mdogo wa msichana chini ya umri wa miaka 18 ni
hatari kwa afya na mstakabali wa maisha yake na mtoto wake.Wasichana
wengi wakati huu licha ya kuanza kupevuka wanakuwa hawajakomaa kiakili
na uwezo wao ni duni katika maamuzi juu ya kufaa kwa mtu atakayekuwa
mwenzi sahihi wa maisha.
Kimwili pia wasichana katika umri huu wanakuwa hawajawa tayari
kuyakabili majukumu ya uzazi na unyumba, nyonga za wasichana
wanaoendelea kukuwa mara nyingi huwa changa na finyu kiasi kwamba
husababisha matatizo mengi ya uzazi wakati wa kujifungua kwa njia ya
kawaida.
Wasichana wengi huchelewa kujifungua au huchukuwa saa nyingi za uchungu
kabla ya kujifungua, hali hii inaweza kusababisha kifo cha mama au mtoto
au wote wawili kama matibabu ya dharura ya upasuaji kwa ajili ya uzazi
hayakufanyika. Idadi kubwa ya akina mama wanaojifungua kwa njia ya
upasuji ni wale walio na umri mdogo.
Wasichana wanaopata ujauzito na kujifungua katika umri mdogo wengi wao
pia hupata tatizo la fisitula - Vescovaginal fistula (VVF) au
Rectovaginal fistula (RVF). Fisitula husababisha msichana kutokwa na
haja ndogo au kubwa bila kujizuia. Haja kubwa pia inaweza kumtoka
msichana kwa kupitia tupu ya mbele. Tatizo la fistula huharibu sana afya
ya mwili na hisia za msichana.
Tatizo jingine linaloambatana na mimba katika umri mdogo ni pamoja na
kutokwa na damu nyingi pale mimba inapoharibika au wakati wa kujifungua.
Wasichana wengi hukabiliwa na tatizo hili ikiwa ni pamoja na kupata
uambukizo wa bakteria katika njia ya kizazi pamoja na kupata kifafa cha
mimba.
Wasichana wadogo mara nyingi huzaa watoto wenye uzito pungufu au njiti,
watoto namna hii hukabiliwa na na hatari pamoja na changamoto nyingi za
kiafya katika umri wao chini ya miaka mitano. Watoto wengi hupata
matatizo ya mtindio wa ubongo na taahira ya akili. Wasichana wengi
wanaozaa katika umri mdogo hupata hali ya aibu na hisia ya kudharauliwa
mambo ambayo huongeza mzigo kwa wote mama na mtoto.
Wasichana wanaoolewa au kupata mimba za utotoni hupeteza fursa na haki
ya elimu. Wengi wao hufukuzwa shuleni au wazazi wao hupoteza imani kwao
kiasi kwamba, husita kuwaendeleza kimaisha hata baada ya kujifungua,
hali hii hufungua mlango kwa msichana kuingia katika umaskini na kuzaa
ovyo bila mpangilio. Mzigo huongezeka pale msichana anapolea watoto peke
yake kama hakubahatika kuolewa au kama ataachika baada ya kuolewa.
Wasichana wanaoolewa kutokanan na kukosa uwezo wa kukabili matakwa ya
unyumba na majukumu yake, wengi hukabiliwa na unyanyasaji, ukatili
pamoja na udhalilishaji wa kijinsia ndani ya ndoa. Wengi hupata vipigo
vinavyo wasababishia ulemavu wa maisha au vifo.Wengi hutukanwa na
kubezwa.Wengi hulazimishwa kuolewa na watu wenye umri mkubwa bila hata
kupima damu kwa ajili ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kabla ya ndoa.
Hali hii huwafanya wasichana wanaoolewa katika umri mdogo kukabiliwa na
hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI na wengi huwa wajane kabla ya
kuwa watu wazima. Wale wanaoachika huwa na uwezekana mkubwa wa kuachika
tena pale wanapoolewa kwa mara nyingine. Hii hutokana na athari za
kisaikolojia zinazowajengea wasichana hawa doa la kitabia katika jamii
na kuwafanya wasione umuhimu wa kudumisha mahusiano ya ndoa kutokana na
uzoefu mbaya walioupata katika ndoa za awali.
Mimba zisizotarajiwa na zisizotakiwa
Mara nyingi wasichana wadogo hawana elimu ya kutosha kuhusu muda wa
vipindi ambavyo wanaweza kupata ujauzito. Wengi hujiona kuwa ni wajanja
kiasi cha kutokupata madhila ya mimba lakini husahau kuwa ndege mjanja
hunaswa na tundu bovu. Wengi wao pia kutokana na sababu mbalimbali za
kibinafsi na za kijamii, hawapati fursa za kutumia huduma za afya ya
uzazi wa mpango.
Wasichana wengi wanaojihusisha na ngono kabla ya ndoa hupata mimba
zisizopangwa, zisizotakiwa na zisizotarajiwa. Jambo hili huleta mzigo
mkubwa wa kihisia kwa msichana hasa pale anapokuwa mwanafunzi. Wasichana
wengi wanaojikuta katika hali hii hufikiria kutoa mimba kama njia pekee
ya ufumbuzi wa tatizo.
Wengi hutoa mimba katika mazingira hatarishi na
kwa njia zisizozingatia afya na usalama. Hii hutokana na ukweli kuwa,
utoaji mimba ni kosa la kisheria na kimaadili katika nchi nyingi.
Wasichana wanaopata mimba hutangaza hadharani kuwa wao ni washiriki wa
ngono hatarishi ambayo inaweza kumsababishia mtu maambukizi ya virusi
vya UKIMWI na magonjwa mengine hatari.
Hivyo basi kutoa mimba
hakumhakikishii msichana usalama maana wakati wa ngono zembe anaweza
kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI pia ambavyo huwa havitoki kwa
njia ya kutoa mimba.
Utoaji mimba hata hivyo huambatana na hatari nyingi kwa afya na maisha
kwa ujumla wake kwani unaweza kusababisha hali ya kutokwa na
damu nyingi kiasi cha kupoteza maisha, kutoboa mfuko wa mji wa mimba,
uambukizo hatari wa mji wa mimba, ugumba, matatizo ya kisaikolojia na
migogoro ya kisheria.
Kutoa mimba pia huambatana na matumizi ya rasilimali za mtu binafsi na
zile za umma kwa namna ambayo huchangia kuongezeka kwa umaskini, vile vile gharama
za kuhudumia msichana aliyepata athari za utoaji mimba ni kubwa na
huduma hizi hutumia muda na rasilimali nyingine ambazo zingetumika
kuhudumia wangonjwa wengine.
Watoto wanaozaliwa na watoto wenzao
Wasichana wengi wanaopata watoto katika umri mdogo, hukabiliwa na tatizo
la kulea watoto peke yao kwa vile wengi huwa hawajaolewa na hata kama
wataolewa, wengi huachika mapema.
Wengi wao hawana maandalizi kwa ajili
ya ndoa na majukumu ya kutunza watoto hivyo watoto wengi wa akina mama hawa
hupata matatizo ya kihisia hasa pale wasipowaona baba zao pale nyumbani
kama ilivyo kwa watoto wenzao.
Jambo hili huwasababishia athari
ziambatanazo na huzuni, fedheha, msongo wa mawazo, kuumwa mara kwa mara,
kutofanya vizuri katika masomo yao, kukosa usingizi mara kwa mara na
kukosa mapenzi ya baba.
Watoto wasiopata mfano mzuri wa kuiga toka kwa wazazi wote wawili (baba na mama)
mara nyingi huchagua kuiga mambo mabaya kama vile uhalifu, uhuni na
matumizi ya dawa za kulevya kama mbadala wa mambo sahihi waliyotakiwa
kuyaiga kwa wazazi wao.
Wengi wa watoto waliozaliwa na kulelewa na akina mama wenye umri mdogo
hukabiliwa na hatari nyingi na tabia zao hudhoofika. Wengi huwa wavivu,
hukosa nidhamu na kukosa heshima hasa kwa wanawake. Watoto wa kike
wanaozaliwa na akina mama wenye umri mdogo wao mara nyingi nao huzaa
katika umri mdogo kama mama zao.
Watoto hawa mara nyingi hupenda kuwa na mahusiano na wanaume kama
mbadala wa baba zao lakini pia wanaweza kuchukia wanaume na kutoona
umuhimu wa kuolewa kwa namna ya kujiheshimu.Wengi wa watoto hawa hujenga
chuki dhidi ya wazazi wao kutokana na kutotimiziwa mahitaji yao kama
watoto wanaozaliwa na kulelewa ndani ya ndoa zenye upendo amani na
utulivu.
Jinsi ya kuepuka mimba na ndoa za utotoni
- Kujinyima ngono ili kupata afya na usalama kabla ya ndoa, ndiyo njia salama na yenye uhakika zaidi kuliko njia nyingine yeyote inayomsaidia msichana kuepuka na kuzuia mimba za utotoni. Njia hii ilitumiwa na wasichana wengi wa vizazi vilivyopita na kuwaletea mafanikio mengi tena makubwa.
- Wasichana ni lazima wawe na stadi za maisha zinazowawezesha kufanya maamuzi bora na sahihi, wajiamini na kuachana na ngono hadi watakapokuwa wamekomaa kwa ajili ya kukabiliana na majukumu ya unyumba. Balehe ya wasichana hufananishwa na kukomaa kwa tunda ambalo halijaiva tayari kwa kuliwa. Balehe ni maandalizi ya awali ya kuwa mwanamke.
- Ni haki ya msingi ya mwanamke kufanya ngono ndani ya ndoa yake katika kipindi chote cha maisha yake. Hivyo hakuna haja ya wasichana kuwa na haraka, kila jambo lina wakati wake, kuna wakati wa tunda kupevuka lakini likiendelea kuwa bichi na kunawakati tunda hukomaa na kuiva tayari kwa kuliwa bila kuleta madhara.
- Ingawa kuachana na ngono kabisa ni jambo zito kwa wasichana wengi wa kizazi kipya kutokana na shinikizo la utandawazi, lakini bado inawezekana. Kinachohitajika ni kuwa na sababu za msingi za kuacha na kusubiri pamoja na kujizoeza kusema hapana. Kwa wasichana wengi ni vigumu kukabiliana na msukumo wa marika wao wa kuwa na maamuzi yanayotofautiana na wasichana wengine wengi, lakini ni muhumu kufanya maamuzi ya kibinafsi yatakayo kufaidia wewe mwenyewe.
- Ipo haja ya kuwajulisha wenzako msimamo wako hata kama utaonekana mshamba. Ni bora kuwa mshamba ukiwa salama kuliko kuwa jogoo wa mjini bila manyoa wakati wa baridi. Msichana anatakiwa kutumia kichwa chake badala ya vichwa vya wasichana wengine, ni busara kukumbuka kuwa, msingi wa maisha mazuri ya kesho hujengwa leo.
- Kila msichana anao uwezo wa kuamua kwa uhuru ili apate mtoto kwa wakati ufaao. Kinachotakiwa ni kuwa na msimamo na uelewa wa umuhimu wa kupata mimba kwa wakati unaofaa na salama.
1 comments:
safi sana kaka unaweza kutusaidia wadau kupata info zaid big up
Chapisha Maoni