Alhamisi, 23 Agosti 2018

Kilimo Cha Nyanya



Biashara Itakayokupatia Milioni Tano Baada Ya Miezi Mitatu

KILIMO CHA NYANYA
Ndio, kilimo cha nyanya. Tembea kila kona ya Tanzania, nyanya inaliwa kila mahali, kwa hiyo kulima nyanya utakuwa na uhakika wa kupata soko. Nyanya inastawi katika maeneo mengi nchini hivyo ukilima katika eneo ulilopo unaweza kupata mavuno mengi. Kilimo cha nyanya kinawatajirisha watu wengi, hilo nimejiridhisha nalo sina wasiwasi.
Nakushauri uanze kulima nyanya mwezi huu wa Septemba ili kufikia mwezi wa kumi na mbili uanze kuvuna na upate million tano yako.
Mimi nimeamua kulima nyanya; maandalizi ya awali yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuandaa shamba la ekari moja, kusia mbegu za nyanya na kutafuta mbolea ya samadi, yote hayo tayari nimeyafanya; sasa  naenedela kuandaa shamba wakati mbegu zinakua.

Tukutane Mwezi Disemba Nikuonyeshe Milioni Tano Yangu
Sikutanii wala sijisifii, nataka nikuone na wewe unachukua hatua uanze kucheza mchezo wa kutafuta pesa. Sipendi kukuona ulalamika na kunyong’onyea kisa huna pesa, nataka nikuone unafanikiwa, ndiyo furaha yangu ndiyo maana nakueleza mambo kama haya ambayo kwa kawaida ni siri yangu.  Lakini kwa vile nataka nikuone unaanza kucheza mchezo huu hata kama ni kidogo itakuwa vizuri, ukirudia tena utafanya makubwa zaidi.

Sitaki kusema maneno mengi, ufuatao ni mchanganuo wa kilimo cha nyanya ninacholima mimi. Unaweza kuandaa wa kwako utakapo anza kulima.

 KILIMO CHA NYANYA
Awamu ya Kwanza: Septemba 2015
S/No      Mahitaji          Idadi/Kiasi  Gharama        Jumla
1.          Kulima shamba       Ekari 1         40,000/=
2.          Kuandaa matuta     Ekari 1         50,000/=
       Jumla ya gharama zote za kuandaa shamba 90,000/=
3.         Kununua mbegu      Packet 4       28,000/=
4.         Kuandaa kitalu cha kusia
        mbegu na kumwagilia
        mbegu                     5m           10,000/=
  Jumla ya maandalizi ya mbegu                        28,000/= 
5.         Kupanda miche shambani   Ekari 1     50,000/=
6.         Mbolea ya samadi              Trip 5         25,000/=
7.         Kununua jenereta                    1       500,000/=
8.         Kumwagilia (mafuta)         Mara 10     250,000/=
9.         Kupalilia                            Mara 2       20,000/=
   Jumla ndogo                                                    845,000/=
10.     Mbolea ya kuzalishia (CAN) Kilo 10     50,000/=
11.     Madawa ya kutibu magonjwa ya nyanya  40,000/=
12.     Kuvuna                              mara 4        100,000/=
Jumla     ndogo                                              190,000/=
JUMLA YA GHARAMA ZOTE                          1,163,000/=
Mavuno ya nyanya kwa ekari moja ikitunzwa vizuri yanaweza kufikia tani arobaini (40) sawa na madebe 2,200 ya lita ishirini. Lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, magonjwa na sababu nyingine, kiwango cha chini cha kuvuna nimeweka tani kumi na nane (18) sawa na madebe 1000 ya lita ishirini.
Debe moja la nyanya hapa Bariadi linauzwa kwa Tsh 10,000/=.  Labda kutokana na mabadiliko ya bei sokoni, bei ya chini ninayoweza kuuzia iwe Tsh 8,000/= kwa debe.
Nitavuna jumla ya madebe 1,000 na kila debe nitauza kwa Tsh 8,000/=, nitapata jumla ya Tsh milioni nane 8,000,000/=.
Jumla ya mauzo yote                      8,000,000/=
Jumla ya gharama zote                   1,163,000/=
Jumla Ya Faida nitakayopata      6,837,000/=
JUMLA YA FAIDA NITAKAYOPATA KWENYE MRADI HUU AWAMU YA KWANZA NI TSH 6,837,000/=
Huna Milioni Moja, Utafanyaje Kupata Mtaji Wa Kuanzia?
Naomba nikutoe hofu juu ya hilo, ukiangalia kwa makini kwenye jedwali la mchanganuo hapo juu, utagundua kuwa gharama nyingi nilizozitaja ni za vibarua ukitoa gharama za jenereta, kununua mbegu, mbolea ya kuzalishia na dawa za kutibu magojwa. Gharama zingine unaweza kuziepuka kama utashiriki wewe mwenyewe kwenye shughuli hiyo bila kutegemea vibarua.
Njia Nzuri Ya Kupata Shamba Na Mahitaji Mengine
Mimi wakati naamua kulima nyanya sikuwa na shamba la kulima, nilizunguka zunguka huko kijijini nafuta shamba la kulima angalau ekari moja. Haikuwa kazi rahisi wala sikufanikiwa kupata shamba kabisa. Baadaye nilimkuta mzee mmoja anashamba zuri sana lenye rutuba na liko karibu na bwawa la maji. Nikaongea na mzee huyo na kumwomba kama ataniruhusu niungane naye kulima nyanya, tuupanue mradi uwe mkubwa zaidi. Nikampa maelezo mengine mengi nikamweleza faida atakazo pata, hatimaye mzee akakubali. Kwa njia hiyo nikawa nimepata shamba  bure na mbolea ya samadi ya bure maana mzee anafuga ng’ombe. Gharama pekee ni kuisafirisha mbolea kuipeleka shambani. Kupitia ushirika huo nilioupata japo sikuwa na mwenyeji hata mmoja, sasa ninauhakika kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa.
Njia Hii Aliitumia Rafiki Yangu Na Akafanikiwa.
Kuna rafiki yangu mmoja tumesoma naye kidato cha tano na sita pale Milambo High School, kwa sasa yuko Mwanza amehitimu chuo cha SAUTI mwaka jana. Baada ya kumaliza masomo, hakuwa ana fahamiana na mtu yeyote pale jijini Mwanza zaidi ya marafiki zake tu aliosoma nao chuoni. Siku moja akaanza kutembea mjini akitafuta fursa, akafika sehemu fulani hivi akamkuta mzee mmoja anafuga kuku wachache wa kienyeji , rafiki yangu alipowaona hao kuku alifurahi sana. Akamtafuta yule mzee akafanya nae mazungumzo ya kuupanua mradi akamwambia faida atakazo zipata baada ya mwaka mmoja. Yule mzee alifurahi kweli akamkubalia rafiki yangu, kazi ikaanza. Nakawambia mpaka sasa wanafuga kuku zaidi ya elfu nne ndani ya miezi minnne tu, na wanatarajia kuwa na kuku elfu kumi na mbili ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Tumia Njia Hiyo Utafanikiwa Tu
Kama mimi nimetumia njia hiyo na nimefanikiwa, kama rafiki yangu alitumia njia hiyo na akafanikiwa na wewe tumia njia hiyo upate mahali pa kuanzia nina uhakika utafanikiwa. Kumbuka kutafuta pesa ni mchezo, cheza kwa furaha,  bila hofu moyoni mwako hakika utashinda na kufanikiwa.
Mbegu Gani Ya Nyanya Nzuri?
Baada ya kuuliza uliza watu wengi na wataalamu wa kilimo, wamenishauri nilime aina ya Mwanga.  Wanasema ina mavuno mengi na ganda lake ni gumu na inavumilia magojwa mengi. Mahali unapoishi ulizia nyanya aina gani inakubalika sokoni, utapata jibu. Mbegu zingine nilizozikuta madukani ni Tanya, Cal J, Tengeru 97, Iffa, Mkulima, Maoney maker na nyingine nyingi. Fanya utafiti wako ujue ni ipi inafaa.
Tulime Pamoja
Nachukua nafasi hii kukukaribisha uambatane nami kwenye kilimo hiki cha nyanya. Unaweza ukawa na uzoefu mkubwa wa kilimo hiki tafadhali weka maoni yako hapa chini kwenye kibox cha comment ili utusaidie na sisi ambao ndio tunaianza kazi hii au unaweza kuniandikia kupitia email yangu morningtanzaniasite@gmail.com. Pia wale watakao kuwa na maswali yoyote wanaweza kuniuliza kwa email hiyo au kwa kuandika kwenye kibox cha comment.
“Kama mimi nimetumia njia hiyo na nimefanikiwa, kama rafiki yangu alitumia njia hiyo na akafanikiwa na wewe tumia njia hiyo upate mahali pa kuanzia nina uhakika utafanikiwa”

0 comments: