Jumanne, 21 Agosti 2018

Waomba wasaidiwe umeme wa REA

WANANCHI wa Jimbo la Kondoa Mjini mkoani hapa, wamemwomba mbunge wao, Edwin Sannda awasaidie wapate umeme wa Mradi wa Nishati Vijijini (REA) unaopita katika maeneo yao ili kuboresha maisha yao.
Maombi hayo waliyatoa mwishoni mwa wiki katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika maeneo mbalimbali wakati wa ziara ya mbunge kukagua miradi hiyo na kuelezea namna Ilani ya CCM inavyotekelezwa. Wananchi wa mitaa ya Bolisa, Ukunku na Mulua, walimwomba mbunge wa Kondoa Mjini, Sannda kuwasaidia kupata huduma ya umeme katika mitaa yao ambayo imepitiwa na nguzo za umeme wa REA na haijapewa umeme.
Akijibu maombi hayo, mbunge huyo alisema, serikali imepanga kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya umeme katika jimbo hilo. Sannda alisema, mkandarasi wa kusambaza umeme katika mitaa mbalimbali katika wilaya ya Kondoa tayari amepatikana, kinachosubiriwa sasa ni kuanza kazi baada ya kumaliza kazi katika wilaya ya Chamwino na Bahi. Sannda alisema serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutoa huduma hii na ndio maana inafanya kazi kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza kuna maeneo yalipata huduma ya umeme mengine hayakumalizika.
Alisema ilianza awamu ya pili ambayo ilikamilisha sehemu iliyobakia katika awamu ya kwanza na kuanzisha miradi mipya. Aidha aliwasihi wananchi hao kuendelea kutunza vigingi vilivyowekwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kama alama za kuweka nguzo kwani maeneo mengine wananchi wamekuwa wakiviharibu na kuwapa kazi wakandarasi wanapoanza kazi. Sannda aliwataka wananchi kuendelea kufanya maandalizi ya kusuka nyaya za umeme katika nyumba zao na kuajiandaa kuweka fedha za kulipia huduma ya kuingiza umeme katika nyumba zao.
Ziara ya Sannda ilifanyika katika kata zote nane za Halmashauri ya Mji Kondoa ambapo alifanya ukaguzi wa miradi mbalimbali na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi wa maeneo hayo. Katika mikutano hiyo ya hadhara, wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miaka miwili. Katika ziara hiyo pia aliongozana na viongozi mbalimbali wa CCM katika Wilaya ya Kondoa na wataalamu mbalimbali kutoka katika Halmashauri ya Mji Kondoa.

0 comments: