Ukiudhika na kukasirika dunia haitakujua wala ukifurahi dunia haitakufahamu bali itaendelea na taratibu zake tu za kupuliza upepo kutoka mashariki kwenda magharibi ama kutoka kusini kwenda kaskazini. Mito yake na viumbe waliomo vitaendelea na ratiba zake zile zile za kila siku.
Dunia imejaa uchovu mkubwa. Ukikumbuka sheria na amri za Muumba wetu na ukikumbuka maisha yako yanavyokwenda kinyume na amri hizo nafsi yako inajihisi ni yenye hatia.
Unakumbuka kwamba tupo hapa duniani kwa kitambo tu? Unakumbuka kwamba yoyote uyafanyayo sasa hapa duniani yatasahaulika na mengine uyakusanyayo watayatawanya punde tu wewe ukiondoka? watagawana gawana wale ambao hawakutolea jasho kama wewe. Unakumbuka au umesahau hilo?
Kunawakati unatafakari lakini hupati majibu, saa nyingine usipoangalia unakata tamaa kabisa kwa jinsi
mauza uza ya hapa duniani yalivyo mengi.
Imetokea kipindi fulani katika mgodi wa Nyangarata wilayani Kahama, Tanzania watu watano walifukiwa na kifusi wakiwa ndani ya mgodi kwa siku 41, lakini, hatimaye waliokolewa siku ya 41. Walikuwa wakila kila aina ya wadudu kama vile mende na wengineo kwa muda wote wa siku arobaini na moja. Kama si Mungu wangevukaje masahibu hayo? .Pasipo Mungu tuzo ya tuyafanyayo kwa mikono yetu ni ipi? Kusoma kote huko na kuhangaika kote huko mwisho wake ni nini?. Maisha ni fumbo, fumbua!. Lakini usijali kuna njia nzuri ya kufuata.
Ikiwa Mambo Ndiyo Yako Hivyo Kuna Haja Gani Ya Kuhangaika?
Ndivyo ilivyo, ukifikiri sana unapata picha ngumu saa nyingine unaanza kujisemea kwanini nihangaike namna hii?. Wakati mwingine unawaza kwanini nihangaike kuwa tajiri wakati ninaweza kuwa masikini na nikaishi tu? Sikia, mimi nakushauri uweke msimamo wa aina moja tu; amua kuwa TAJIRI. Ndiyo amua kuwa tajiri. Haijalishi picha unayoipata iko je wewe weka msimamo wa aina moja tu wakuwa tajiri nitakueleza kwanini unatakiwa kuwa tajiri.
Fahari Ya Maisha Yako Iko Ndani Yako Nasio Nje Yako
Kumbe nimefahamu, tunakazi moja tu hapa duniani ambayo ni KUCHEZA KWA FURAHA. Maisha yote ni mchezo hakuna kazi nje ya kucheza. Ukiwa kiongozi unacheza, ukiwa Mwalimu unafundisha huo ni mchezo wa kufundisha, ukiwa mkulima unalima unacheza, kulima ni aina ya mchezo, ukiwa dereva unaendesha nao ni mchezo, ukiwa na mke/mume wako mnatengeneza mtoto nao ni mchezo, ukiwa wewe ni mchezaji wa masumbwi nao ni mchezo kama ilivyo michezo mingine nakadhalika. Bahati nzuri michezo yote ni raha, michezo yote ni furaha, michezo yote ni mitamu na kiwango cha utamu wa kila mchezo unafanana. Ukiwa wewe ni mwekezaji, kuwekeza ni mchezo. Kwahiyo kila jambo unalolifanya ni mchezo na hakuna mchezaji yoyote alliyeamua kucheza ambaye haufurahii mchezo wake. Wote wanafurahia sana kuwa wachezaji.
Ikiwa ndivyo hivyo, kuwa tajiri ni lazima uwe unapenda kucheza mchezo wa kutafuta pesa. Kuna michezo mingi ya kutafuta pesa, kwa mfano; Unaweza kuwa mfanya biashara, unaweza kuwa mkulima, unaweza kuwa mwekezaji, unaweza kuwa mchezaji wa aina yoyote lakini yote hiyo ni michezo ya kutafuta utajiri.
Siri hii imenifanya nibadilishe kabisa namna ya kufikiri kwangu. Nimeamua kuwa mchezaji wa kutafuta utajiri. Nacheza mchezo huu kwa furaha, pesa kwangu si kila kitu pesa kwangu, bali ni kichocheo cha kunifanya nizidi kucheza mchezo huu. Nacheza kwa furaha siku zote, hasara kwangu si kitu bali ni matokeo ya kucheza, kwahiyo nikipata hasara najua kunamahali nimecheza vibaya narekebisha makosa naendelea kucheza.
Najua wazi kwamba, nikiwa tajiri nitaweza kucheza michezo mingi zaidi hapa duniani. Kumbuka kadiri unavyocheza vizuri ndivyo unavyopata furaha moyoni mwako. Nikiwa tajiri nitaweza kucheza michezo mingi zaidi kama vile mchezo wa kutalii popote duniani, mchezo wa kuwekeza zaidi. Mchezo wa kusaidia watu wengine, na michezo mingine mingi nitaicheza kwa furaha. Kwa sababu hiyo lazima niwe tajiri ili furaha ya kucheza iongezeke ndani yangu. Sitakata tamaa kwa sababu changamoto za uhaba wa pesa kwa sasa si kitu kwangu bali ni kichocheo cha kunifanya nianze kucheza michezo mingi zaidi ili kukabili hali hiyo.
Nakupongeza Kwa Juhudi Zako Lakini Bado Jambo Moja Unatakiwa Kulifanya
Ikiwa mpaka umefika siku ya leo uko namna hii, mimi nakupongeza kwa hatua hiyo lakini pia wewe mwenyewe unatakiwa ujipongeze kwa kufika hapo ulipo fikia. Tatizo lako wewe unaangalia magumu tu yanayokupata huangalii mazuri mengi uliyoyafanya.
Sasa, kuna kitu kimoja ambacho leo nakushauri uanze kukifanya kuanzia leo, ikiwa unataka kufanikiwa na kufikia utajiri ambao ni kiwango cha juu cha uchezaji wa michezo mingi. Kitu hiki ni KUTHUBUTU.
Nasema ni lazima uanze kuthubutu. Kuthubutu maana yake nini? Ni kufanya jambo ambalo kwa muda mrefu au kwa maoni ya wengine linaonekana ni gumu au haliwezekani kufanyika. Wewe unatakiwa uibuke na kulifanya hata kama utalianza vibaya itakuwa heri kwako.
Kwa mfano mimi mwaka 2007 niliweza kuthubutu kusafiri kutoka Tabora kwenda Sumbawanga kwa shilingi miambili tu (200/=) na nilifika sumbawanga bila shida. Kwa akili ya kawaida tu haiwezekani kusafiri umbali huo kwa shilingi 200/= lakini mimi nilithubutu na nikaweza japo kila mtu niliyemwambia kuhusu safari alisema hutaweza lakini niliweza.
Soma makala hii ukitaka kufahamu nilifanyaje. Nguvu Iliyomfanya Daudi Ampige Goliath Inaweza Kukusaidia Na Wewe Umpige Goliath Wako
Uthubutu unakupa uhakika wa kufanikiwa maishani mwako. Mara nyingi sana wasiwasi hutufanya tushindwe kufikia mafanikio yetu. Jiulize ni mara ngapi umeshindwa kufanya biashara kwa kisingizio cha kukosa mtaji? Mimi nasema hukukosa mtaji ni kisingizio tu, pesa zipo nyingi sana kama sio za kwako tumia za wengine.
Majumuisho Ya Somo La Leo
Kama wewe sio mchezaji hapa duniani, ni mtazamaji tu, kazi yako ni kutazama wale wanaocheza, basi fahamu kwamba kila siku dunia utaiona ni mahali pachungu.
Nasema hivyo kwa sababu ukiwasha luninga yako au redio yako jambo la kwanza utasikia watu 20 wameuawa huko Syria na wengine 200 wamepata ajali na wengine 150 wameuawa kwa shambulio la kujitoa mhanga na wengine 1000 wamekumbwa na kimbunga na wengine 2000 wamelipukiwa na vinu vya nyukilia nakadhalika na kadhalika.
Hayo yote yatakufanya ukate tamaa na saa nyingine ujilaumu kuzaliwa au ujione mnyonge au ujione huna thamani hapa duniani, unajisikia mwenye hatia. Lakini ukweli ni kwamba tumeumbwa ili tucheze michezo kwa furaha kubwa. Hakuna mchezaji anayecheza amenuna, wachezaji wote wanacheza kwa furaha siku zote. Anza kucheza leo kwa furaha.
“Tafakari, jitume, Jibidishe Sana Lakini Mwisho wa Siku Kumbuka Kuna Kitu Muhimu Unahitaji ili Ufanikiwe...Kitu hiki ni KUTHUBUTU!! Ndiyo, Nasema ni lazima uanze kuthubutu”
0 comments:
Chapisha Maoni