Jumamosi, 2 Aprili 2016

Kukosea Ni Kawaida, Kubali na Ujifunze!


 
Unajisikiaje pale mtu mwingine anapokuambia neno hilo? Kwamba wewe umekosea?
Mara nyingi watu wanapoambiwa hivyo kwa haraka sana huanza kupinga, huanza kutafuta kitu cha kujitetea.
 
Kukosea kunauma na hivyo wengi hawapendi kuonekana wamekosea, hata kama ni kweli wamekosea. Badala yake hutafuta kila njia ya kujitetea na kujiondoa kwenye kile ambacho wamekosea.
 
Sasa wewe rafiki yangu usiingie kwenye mkumbo huu, usitake kukimbia kosa lolote ulilofanya, kwa
sababu haitakusaidia, badala yake itakuumiza zaidi.
Kama mtu anakuambia umekosea, badala ya kukimbilia kukataa au kujitetea, mwombe akupe ufafanuzi ni wapi ambapo umekosea. Na weka mawazo yako huru kusikiliza. Usisikilize huku unajiandaa kupinga au kujitetea, bali sikiliza ili kuelewa ni wapi umekosea kweli au ni wapi ambapo watu hawakuelewa vizuri na hivyo kuona wewe ndiye uliyekosea.
 
Kama ni kweli umekosea basi kubali na ahidi kutorudia tena kile ulichokosea. Na kama watu walielewa vibaya basi unaweza kuwaelewesha vizuri ili muweze kwenda sawa. Kwa kufanya hivi utaondokana na ubishani usio wa msingi na pia kujifunza zaidi na hivyo kutokurudia kosa, au kuhakikisha unawaelewesha watu vizuri ili wasikuelewe tofauti.
 
Kukosea siyo mwisho wa dunia, bali ni njia ya kujifunza na kuwa bora zaidi. Na sio mara zote watu watakuelewa kwa kile ulichosema au kufanya.
Hivyo kuwa tayari kujifunza kutokana na makosa yako na kutoa ufafanuzi sahihi kwa wengine.
 

UKWELI NI KWAMBA ni vigumu sana mtu kukubali makosa yake hasa pale anapoambiwa na wengine
kwamba amekosea. Achana na hili na badala yake wasikilizE kwa makini wale wanaokuambia umekosea, nfahamu kuwa kuna mengi sana utajifunza kutoka kwao, iwe umekosea kweli au la.
 
CHUKUA HII
Mistakes are always forgivable, if one has the courage to admit them. - Bruce Lee
 
(Makosa mara zote huwa yanasamehewa kama mtu ana ujasiri wa kuyakubali).
 
Unapokosea usitafute njia ya kutoroka, Kubali makosa yako, jifunze kupitia makosa yako na hakikisha huyarudii tena.

0 comments: