Jumamosi, 9 Aprili 2016

Ipo Nguvu Ya Kuleta Mafanikio Kwako, Nayo Hufanya Kazi Kwa Mfumo Huu.

Rafiki Mpendwa, Bila shaka umewahi kupita sehemu mbalimbali za mjini, mfano sokoni na maeneo mengine. Katika kupita kwako kote huko, hujagundua kitu wala hujawazia kitu au bidhaa yoyote. 
 
Siku moja ukapata wazo la kununua jiko la mkaa. Ukaenda tena mjini kama kawaida yako, lakini leo hii unawazo la kununua jiko la mkaa. Ukafika sokoni ukashangaa kuona jinsi majiko ya mkaa yalivyo mengi lakini siku za nyuma ulikuwa unapita pale pale ila huyaoni au kama uliyaona hukuyafikiria. 
 
Unaamua kuangalia ili uchague jiko zuri unalolipenda, unajisemea ngoja nizunguke zunguke sokoni nikiulizia bei na pia nikitafuta jiko zuri nitakalolipenda. Unaanza kuzunguka sokoni unashangaa kuona kumbe soko limejaa majiko ya mkaa mengi namna ile, kila sehemu ni majiko ya mkaa hatimaye unaamua kununua moja unarudi nyumbani.
 
Siku nyingine kama kawaida yako unapita mjini katika tembea tembea yako, huoni kitu, kila jambo ni kawaida tu. 
 
Siku moja unaamua  ununue usafiri angalau uanze na pikipiki. Siku inafika unaenda mjini kama kawaida yako, lakini leo hii unawazo la kununua pikipiki. Unashangaa siku ile unaona vituo vingi sana vya kuuzia piki piki halafu unagundua kumbe mjini kuna pikipiki nyingi sana za kila aina. 
 
Siku hii unaanza kuona na kuelewa aina za pikipiki lakini siku zingine ulikuwa hujali sana kuangalia aina za piki piki. Unajisemea, ngoja nizunguke zunguke mjini nikitafuta pikipiki nzuri. Unaanza kuzunguka zunguka unashangaa kila mahali mjini kuna kituo cha kuuzia pikipiki. Hatimaye unachagua ya kwako unanunua unarudi nyumbani.

Nimekupa mifano hiyo miwili nikitaka kukueleza kwamba umezungukwa na fursa nyingi sana kila mahali zimezagaa. Tatizo huna macho ya kuziona fursa hizo, mpaka siku utakapo weka malengo ya kuona baadhi ya fursa hizo utashangaa kuziona zimetapakaa kila mahali.

Weka Malengo Yako Nikuonyeshe Jinsi Inavyokuwa
Unapoweka malengo maana yake unataka ufike sehemu fulani. Ni kama mtu anaposafiri kwenda mbali labda mkoa au nchi nyingine atahitaji ramani imwongoze ili afike huko salama. Malengo hayawekwi kichwani tu, malengo yanaandikwa. 
 
Ni lazima unapoweka malengo yaandike na ukisha yaandika yapitie mara kwa mara ikiwezekana kila siku na hata unapotembea unatakiwa uwe nayo kichwani na ufikiri namna ya kuyafanikisha.

Anga Lote Limejaa Mawazo Ya Kukusaidia Malengo Yako
Hii ni siri ya ajabu sana. Michal Miszcuk katika kitabu chake Be Happy then Live (unaweza kubonyeza jina la kitabu hapo juu kukidownload bure) anailezea siri hii kwa undani sana , anasema anga lote limejaa nguvu ya ajabu ambayo kazi yake ni kuwasaidia watu katika hisia zao. 
 
Kama wewe unahisia za woga, nguvu iliyopo angani itakuongezea woga mwingine ili uwe mwoga zaidi. Kama unawaza jambo fulani na unakiu ya kutaka kulipata, uwe na uhakika nguvu ya angani itakupa majibu haraka sana, ndio maana nimekupa hiyo mifano miwili hapo juu.
 
Kwahiyo, ukitaka kufanikiwa jambo lolote hata kama huna nyenzo za kulifanikisha jambo hilo, usiogope unachotakiwa wewe ni kuliandika liwe kama malengo yako halafu tumia  muda mwingi kuwaza na  kufikiri namna utakavyolipata. 
 
Kadri unavyo waza na kufikiri ndivyo nguvu iliyoko angani inazidi kukufumbua macho yako, utashangaa siku zote ulikuwa unapita sokoni huoni majiko ya mkaa lakini ukishawaza tu kununua jiko la mkaa  macho yako yanaanza kufumbuliwa taratibu unashangaa kuona soko zima limejaa majiko ya mkaa.
 
Ndiyo maana kama usipoweka malengo hakuna kitu utakachofanikiwa au hata kama utafanikiwa ni kwa kiwango kidogo sana, sisi hapa tunataka ufanikiwe kwa kiwango kikubwa.

Kichwa Chako Ni Kama Rada Hutuma Na Kupokea Mawimbi
Brian Tracy katika kitabu  chake “The Goal” anaelezea jambo hili, anasema ndani ya ubongo wa mwanadamu kuna sehemu ndogo inayofanya kazi ya kutuma na kudaka mawimbi kutoka angani. Sehemu hii ya ubongo hutuma na kudaka mawimbi yale tu akili ya mtu huyu inayawaza kwa hisia kali au kwa kiu kali. 
 
Kama unawaza kuwa mchawi na umedhamiria kabisa kuwa mchawi utashangaa siku moja moja unaota unaloga au unapaa na ungo, ni kwa sababu sehemu hii ya akili inadaka mawazo ya uchawi yanayoelea angani. 
 
Kama unawaza na unakiu ya kutengeneza ndege uruke angani, si ajabu unaweza kutengeneza ndege yako, kama walivyofanya wale vijana wawili wa Marekani waliotengeneza ndege ya kwanza, wanaitwa Wright Brothers.
Je, Wewe Unataka Nguvu Hii Ikusaidie Nini?
Chochote unachotaka ikusaidie itakusaidia. Lakini masharti ya nguvu hii ni lazima uweke malengo ya kile unachotaka ukusaidie, malengo yako yaandike halafu tumia muda mwingi ukiyafikiria na kutaka kufahamu namna ya kuyafanikisha. Utashangaa kufumba na kufumbua inakuletea jibu au njia. 
 
Kumbuka sio lazima ikuletee majibu moja kwa moja inaweza kukuletea mtu atakaye kupa mwongozo au inaweza kukuonyesha kitabu cha kusoma chenye majibu ya kile unachokitaka.
 
Si ajabu hata mimi, ninaweza kuwa nimesukumwa na nguvu hii ili nikusaidie wewe kwenye kitu unachokitamani na umekuwa unakitafuta muda mrefu. Sio ajabu, inaweza ikawa hivyo.

Kama Mawazo Yako Angani Yanaelea, Chagua Moja Ulifanyie Kazi.
Bila shaka, ulishawahi kufikiria kuanzisha biashara fulani hivi. Kabla hujaanzisha hiyo biashara unagundua kumbe kuna mtu mwingine ameianzisha tena inawezekana ni katika eneo hilo hilo ambalo na wewe ulikuwa unafikiria kuanzisha. 
 
Kwanini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu mawazo yote yapo angani yanaelea unapolidaka wewe kwa mfumo nilioueleza hapo juu, na mwingine analidaka kwa mfumo huo huo.
Unatakiwa kufanya nini basi?. 
 
Robert Kiyosaki anasema usihangaike kubuni au kugundua bidhaa mpya. Dunia imejaa bidhaa mpya nyingi sana lakini watu waliojidhatiti kufanya biashara ni wachache sana. Maana yake nini?. Maana yake, biashara hiyo hiyo uliyokuwa unaiwazia unaweza kuifanya lakini ukabuni mbinu ambayo wenzako hawana na ukauza sana. 
 
Kwa mfano, kuna rafiki yangu mmoja alikuwa anaelezea ubunifu alioufanya jamaa yake sehemu fulani hivi, anasema yule jamaa yake alifungua duka la bidhaa za umeme kama, luninga, suboofer, na vitu vingine vingi. Ili kuteka na kupata wateja wengi, yule jamaa alianzisha mtindo wa kukopesha, kama mtu akitaka kununua na hana hela ya kutosha au anayo kidogo alikuwa anamkopesha kwa makubaliano maalum na mwisho wa mwezi analipa deni. Kwa kufanya hivyo alipata wateja wengi sana na sasa ni tajiri mkubwa.

Anayefanya Vizuri Kuliko Wengine Ndiye Mshindi
Dhamiria kuwa mshindi, dhamiria kuuchukia na kuukataa umasikini. Fursa tunazo nyingi, uwezo wa kufanikiwa tunao, kilichobaki ni kuweka nia ya kufanikiwa. Weka nia, hakuna sababu ya kuwa masikini na tukiwa masikini ni kwa sababu hatutaki kufanikiwa, sio kwa sababu hatuna nyenzo. Nyenzo tunazo tuzitumie, nyenzo ya kwanza ni kuamua, nyenzo ya pili ni kupata maarifa na kutunza afya yako. 
 
Ukiyazingatia hayo kusanya nguvu nyingi kutoka angani halafu songa mbele. Usiangalie mtu yeyote jiangalie wewe na hatima ya maisha yako. Hapa sio swala la kumwangalia mume wako anasemaje wala sio swala la kumwangalia mke wako anasemaje, ingawaje ni vizuri kama mtavipigana vita hivi pamoja.  
 
Mimi nimeshachukua hatua, sitarudi nyuma, nakuhamasisha na wewe ujiunge kwenye safari hii ya mafanikio.
imeandikwa na


“Ndani ya ubongo wa mwanadamu kuna sehemu ndogo inayofanya kazi ya kutuma na kudaka mawimbi kutoka angani”

0 comments: