Jumamosi, 2 Aprili 2016

Tupaze Sauti Dhidi Ya Ukatili Kwa Watu Wenye Ualbinism, Ni Unyama Usiovumilika!!


Matendo ya Ukatili na Unyama wanavyofanyiwa Watu wenye Albinism, kumeichafua sana nchi yetu!

Vitendo vya kukata viungo vyao na hata kuwaua kabisa kumewafanya nduguzetu hawa kuishi kwa mashaka makubwa kana kwamba hawafai kuishi katika nchi yao wenyewe.

Hakuna amani kwa wat wenye albinism hata katika kile kinachoitwa nchi zenye amani katika Bara la Afrika, na Tanzania ikiwemo, ambako wanazaliwa, wanakua, wanaishi na kufanya kazi! Hata baada ya kufariki dunia, bado ndugu zetu hawa hawapumziki kwa amani kwani makaburi yao hukuliwa na viungo vyao  kuibwa.

Kati ya mwaka 1998 na 2015 Jumla ya matukio 413 ya Mauaji, ukataji wa viungo, kubakwa, utekaji nyara, majaribio ya utekaji nyara, makaburi kufukuliwa na kupotea kwa watu wenye Albinism yalilipotiwa katika nchi 25 za Afrik
a.


Tabora ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania ambayo imekumbwa na unyama huu kwa kiwango kikubwa na chenyekuleta fadhaa kubwa, na hivyo kuwa ni miongoni mwa maeneo hatarishi kwa nduguzetu hawa wenye Albinism.

Vitendo hivi vinafanywa na watu wavivu ambao wanaaminishwa na waganga wa kienyeji kwamba kwa kutumia viungo vya watu wenye albinism watakuwa matajiri, na pia kumekuwapo madai kuwa baadhi ya wanasiasa wanahusika katika Unyama huu kwa imani kuwa wakitumia viungo hivyo wataibuka na ushindi katika chaguzi mbalimbali.

Mimi hainiingii akilini hata kidogo kwamba viungo vya watu wenye Albinism vinauwezo wa kumfanya mtu kuwa Tajiri au kushinda kwenye uchaguzi, badala yake ninaamini katika uwezo binafsi wa mtu mwenyewe kujiletea mafanikio hayo. Kwa nini?

 Albinism sio jambo la miujiza, na watu wenye Abinism wanazaliwa, hawatokei kimiujiza!!! Mtu anazaliwa akiwa na Albinism kutokana na wazazi wake kubeba vinasaba vya Abinism. Ukweli ni kwamba watu wenye albinism wako duniani kote, wote wana sifa sawa, hali sawa na wanafanana kwasababu wote wanakosa Melanin kwenye ngozi, macho na nywele. Ingwa rangi za ngozi zao pengine hutofautiana, lakini wote wana uoni hafifu!!

Ingawa albinism ni hali ya nadra sana ya nasaba, lakini tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 19 nchini Tanzania amebeba vinasaba hivyo!! Hii inamaanisha kuwa ingawa mimi na wewe hatuna albinism haimaanishi kuwa hatuna vinasaba hivyo!

Kwa mujibu wa taarifa za mwanasayansi kutoka Marekani, DKT Murray Brilliant Mtaalamu wa elimu ya nasaba ya Albinism, kuna aina tofauti za vinasaba vya Albinism ambapo kuna Oculocutaneous Albinism 2 (OCA2) ambayo imezoeleka sana katika nchi za Afrika huku sehemu nyingine za dunia kukiwa na OCA1, OCA3 na OCA4, vilevile kuna Ocular Albinism (OA) ambayo ni ukosefu wa melanin machoni pekee na hii mara nyingi huonekana kwa wanaume.

 Sasa hebu niambie hiyo miujiza ya utajiri kwenye viungo vya watu wenye Albinism inatokea wapi?

Kutokana na taarifa hizo za kisayansi, inawezekana kabisa kuwa kama sio sisi basi hata ndugu zetu wanaweza kupata watoto au wajukuu wenye Albinism! Hivyo basi vita hii dhidi ya Unyama wanaofanyiwa ndugu na rafiki zetu wenye Albinism ni yetu sote.

Naamini wanaofanya hivi wanatoka katika jamii zetu na inawezekana tunawajua au tunazo taarifa zao, kukaa kimya huku tunajua habari kuhusu wahalifu hawa na kuamua kukaa kimya, kunatufanya kuwa tunashiriki katika ukatili huu.

PAZA SAUTI YAKO KUPINGA UKATILI HUU WA KISHETANI kwa kuwafichua wote wanaohusika, Usikubali kuwalinda!!!!

0 comments: