Usipokuwa makini siku yako nzima inaweza kuharibiwa na watu. Au hata kazi yako au biashara yako ikaharibiwa na watu wengine. Japo ni jambo ambalo ni la kizembe, kwa wewe kukubali mtu mwingine akuharibie chochote ambacho ni chako, lakini imekuwa inatokea.
Ni mara ngapi umekuwa ukilaumu watu kwamba wamekuharibia siku yako, wamekuharibia maisha yako, wamekuharibia kazi au biashara yako na mengine mengi.
Kuna dawa nzuri sana ya kuepuka watu kukuharibia vitu
vyako, vitu ambavyo umeweka juhudi kubwa sana kujijengea kwenye maisha yako. Na dawa hiyo ni kuwaelewa watu. Kwa kuwaelewa watu wanaokuzunguka au unaokutana nao kwenye maisha yako ya kila siku, kutakusaidia usiharibu siku yako au maisha yako.
Nina uhakika hakuna mtu anayeamka asubuhi na kusema leo nakwenda kuharibu siku ya mtu fulani, hakuna mwenye akili timamu anaweza kuamka na lengo la aina hii. Na kama wapo basi ni wachache sana. Hii ina maana kwamba wengi unaowalaumu wameharibu siku zako au maisha yako halikuwa lengo lao kuu kwenye maisha yao kwa siku hiyo.
Na hii inaonesha kwamba kuna kitu kimetokea katikati ambacho kimefanya mtu afanye kitendo ambacho wewe umetafsiri kama kukuharibia wewe. Ndiyo maana ni muhimu sana uwaelewe watu vizuri, ili hali zao zisiingilie maisha yako.
Kwa mfano kuwa watu ambao wao wameshindwa na hivyo wanaamini kila mtu ni wa kushindwa, kuna watu ambao hawajawahi kujaribu mambo makubwa na hivyo wanaamini kila anayejaribu atashindwa, kuna watu wana hasira na maisha yao na hivyo kila wanayemwona mbele yao wanaona ndiye chanzo cha maisha yao kuwa hovyo.
Unapowajua watu inakuwa rahisi kwako kuona sababu za wao kufanya yale wanayofanya na kuhakikisha hayaingilii maisha yako.
Wewe ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya maisha yako, usikubali mtu yeyote aje ayaingilie maisha yako na kuyavuruga kwa njia yoyote ile. Jua wengi wanaojaribu kufanya hivyo siyo malengo yao bali inaweza kutokana na hali ambazo wao pia wanapitia. Epuka kuchochea chochote hasi ambacho mtu anacho ndani yake, na maisha yako yatakuwa bora.
UKWELI NI KWAMBA hakuna mtu anayepanga kuharibu siku yako au maisha yako kwa makusudi. Bali watu wana changamoto zao ambazo zinawafanya wanafanya maamuzi ambayo yanaweza yasiwe bora sana kwako. Tambua ya kwamba wewe ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya maisha yako, usiruhusu mtu yeyote kuyaharibu. Waelewe vyema wale wanaokuzunguka ili uweze kuepuka matendo yao yanayoweza kuharibu siku yako.
CHUKUA HII.
“Do not allow the opinions of others deter you. Be yourself and have faith in your abilities.” ― Lailah Gifty Akita
“Do not allow the opinions of others deter you. Be yourself and have faith in your abilities.” ― Lailah Gifty Akita
(Usiruhusu maoni ya wengine kukuzuia wewe kufanya kile unachotaka. Kuwa wewe na amini kwenye uwezo mkubwa uliopo ndani yako).
Usikubali mtu yeyote akuharibie siku yako au maisha yako, waelewe watu na epuka kuwa kichocheo cha hali zao hasi.
0 comments:
Chapisha Maoni