Habari yako ndugu na rafiki;
Leo ni siku nyingine nzuri, yenye kila Neema na Rehema.
Najisikia furaha pale ninapokuona tunaendelea pamoja kwenye juhudi zetu za
kuboresha maisha yetu. Leo nimekuletea makala hii nzuri ndani yake ikiwa imebeba
ujumbe muhimu kwako kwa wakati huu.
Ndugu, maisha yapo, yataendelea kuwepo hata kama mimi
na wewe hatutakuwepo. Mimi na wewe
na yule na watu wengine wote unaowaona tumepewa fursa moja kubwa ya kuishi. Wote
tumezaliwa na tumekua kila mmoja kwa jinsi yake, wote tunapumua na kutumia hewa
hii hii ya aina moja. Wote tunapata mwanga huu huu wa jua. Na mambo mengine
mengi tunashirikiana sawa kwa wote.
Pamoja na kwamba tuna shirikiana mambo mengi, kuna
tofauti zinajitokeza miongoni mwetu. Moja ya tofauti hizo ni mafanikio. Kuna wengine
japo umri na mambo mengi tunafanana lakini wanatuzidi kimafanikio. Kunasababu nyingi
ambazo tunaweza kuzitumia kama ndizo zinazosababisha tutofautiane kimafanikio. Hilo
lisikutishe, hebu tujifunze kwa viumbe wengine.
Ndege
Wajenzi Na Wasio Wajenzi
Kama ilivyo kwa binadamu, ndivyo ilivyo kwa viumbe
wengine kama ndege. Wote wanazaliwa, wanakua na hatimaye wanakuwa ndege wakubwa
kwa jinsi
yake.
yake.
Bila shaka utakuwa umeshapita hapa na pale ukakuta kiota au
viota vya ndege. Kuna baadhi ya ndege wao wamebobea kujenga viota. Hawawezi kuishi
bila kuwa na kiota, lakini kuna ndege wengine
hawawezi kujenga kiota wala hawajathubutu kujenga hata kimoja. Unafikiri
tofauti ya ndege wanaojenga kiota na wasiojenga kiota ni nini?.
Usiseme ni
mazingira wanayoishi ndiyo yanayowatofautisha hilo sio kweli kwa sababu
utawakuta wanaishi eneo moja tena huwa wanawaona wenzao jinsi wanavyojenga lakini
bado hawajengi vya kwao. Usiniambie tofauti yao ni umbo kwamba wengine ni
wakubwa na wengine ni wadogo kwa umbo, hilo sio kweli mbona tai ni ndege mkubwa
lakini anajenga kiota chake na njiwa pori ni wadogo nao wanajenga kiota chao. Kwanini
baadhi ya ndege wanamaumbo makubwa kwa madogo lakini hawajengi viota vyao?
Sababu
Sita Kwa Nini Baadhi Ya Ndege Hawajengi Kiota Chao.
Sababu
ya kwanza: Hawajawahi kuona ndege wa jamii yao wanajenga
Kiota.
Ndege ambao hawajengi kiota sio kwamba hawawezi kujenga ile tu kwamba
hata wazazi wao tangu wazaliwe hawajawaona wanajenga kiota, na wakiangalia
kwenye ukoo wao hakuna hata mmoja aliyewahi kujenga kiota, basi inawapa imani
kwamba hata wao hawawezi kujenga, au wanaamini kwamba kujenga kiota sio
utamaduni wao.
Kwa sababu ya imani hiyo wala hawahangaiki kujifunza jinsi ndege
wengine wanavyojenga. Zaidi zaidi wanavizia pale ndege wajenzi wanapohama na
wao wanaenda kuingia kwenye viota vya wenzao halafu wanajisikia vizuri tu na wanataga
na kutaga mayai humo.
Sababu
ya pili: Wanaamini kujenga kiota ni taabu Sana.
“Kwa nini
kuhangaika kutafuta majani ya miti ya kujengea kiota wakati naweza kutembeatembea
nikakuta kiota kimejengwa na mwenyenacho hayupo halafu nikaishi humo kiulaini”,
hayo ni mawazo ya ndege wasiojenga viota vyao. Kwa sababu ya mawazo hayo na
imani hiyo hawahangaiki hata kujifunza namna ya kujenga viota vyao.
Sababu
ya tatu: Kwao shida na dhiki watavumilia tu.
Ndivyo wanavyofanya
hata leo. Ikinyesha mvua kubwa wanavumilia kwa kujibanza kwenye matawi ya miti
na kwenye mapango. Jua likiwaka sana wanafanya vile vile wanavumilia tu, wakati
wa kulala usiku watatafuta tafuta sehemu watajibana usiku utapita. Wao hiyo
dhiki ni kawaida wala hawajiulizi njia za kutatua dhiki hizo.
Sababu
ya nne: Wanaamini kiota sio muhimu kwao.
Ingawaje wakitaka
kutaga wanavamia viota vya wengine. Kwa lugha nyingine wanajitekenya halafu
wanajicheka wao wenyewe. Mimi nawaonea huruma ndege hawa, kwanini wasijenge
kiota chao tu halafu wendelee kufurahia maisha?
Sababu
ya tano: Mabingwa wa kuongea, kukosoa na kudharau viota vya
wengine.
Ndege hawa ni waajabu sana, saa za kufanya kazi utawakuta wanaimba
nyimbo nzuri wakijinadi kwamba wao ndo wababe wa pori. Wanapowaona wengine wanaojenga viota, wanawakosoa
kwa maneno ya dharau na kashifa. Ni mabingwa wa kulinganisha viota vya wenzao
huku wao hawajajenga hata kimoja. Ni aibu kuwa na ndege kama hawa.
Sababu
ya sita: Mungu amewaruhusu wawe hivyo ili watufundishe.
Mimi namshukuru
Mungu kwa kuwaacha ndege hao katika hali
hiyo japo inauma kuwaona wakiteseka. Alitaka nipate kuona na kuelewa kwamba
unaweza kuishi katikati ya fursa zote lakini usijenge kiota chako japo wenzako
wanaokuzunguka kila siku wanajenga viota vyao. Baada ya kuligundua somo hili nimedhamiria
kujenga kiota changu. Anza kujenga na wewe cha kwako.
Mfano
Huu Wa Ndege Unakuhusu Kwa Namna Hii
Nimesikia mara nyingi watu wakilalamika kuwa mazingira
ni magumu ndiyo maana hawajafanikiwa mpaka sasa. Wanatolea mifano ya watu
waliofanikiwa wanasema, fulani alifanikiwa kwa sababu baba yake alikuwa tajiri,
amempa mtaji mkubwa ndiyo maana sasa hivi amefanikiwa na kutajirika.
Uwezo wa
kufikiri wa watu wanaosema hivyo unaishia hapo. Kinachobaki ni kulalamika na
kuilaumu Serikali eti haiwajali, ndivyo wanavyofanya ndege ambao hawajengi
viota vyao.
Kama unajenga kiota chako utaupata wapi muda wa kulalamika?. Mimi sijui
kama Serikali haitujali ninachojua, kama Serikali haitujali mbona kunawatu
wanatajirika wala hawako kwenye Serikali!, si kwa mali ya wizi bali kwa juhudi
zao na maarifa yao?.
Iache Serikali ifanye ya kwake wewe fanya ya kwako, ukiona
Serikali inakubana au haikuungi mkono kwenye njia fulani badilisha njia tafuta
njia ambayo utafanikiwa.
Jifunze kujenga kiota chako. Nenda porini au sehemu
walipo ndege wanaojenga kiota. Kaa mahali wanapojenga waangalie kwa muda jinsi
wanavyojenga kiota chao jifunze kitu harafu rudi kaanze kujenga kiota chako. Ukisahau
rudi tena kwenye kiota wanachojenga ndege jifunze kitu halafu rudi ukaendelee
kujenga kiota chako. Usiweke visingizio kama wanavyoweka wale ndege wasiojenga
viota vyao.
Tumia
Udhaifu Ulionao Kufanikiwa
Tunaweza kujifunza kupitia kwa mwanamama mmoja mfadhili wa chuo cha
SEKOMU kilichopo mkoani Tanga.
Mama huyu Lena Maria hana mikono tangu kuzaliwa
kwake, pia mguu mmoja hauko vizuri, pamoja na ulemavu huo amesafiri dunia nzima
akitoa matumaini kwa watu waliokata tamaa,
kwa sababu pamoja na ulemavu huo ameweza kushinda medali ya dhahabu mwaka 1989
kwenye mashindano ya kuogelea ya Olympic. Sio hilo tu anaweza kuendesha gari
kwenye majiji makubwa kama vile Tokyo kwa kutumia miguu yake.
Kwa sasa ni
tajiri mkubwa ndiye miongioni wa watu waliokifadhili chuo kikuu cha SEKOMU.
Je, ningekuwa mimi au ungekuwa wewe ungeweza
kufanya nini ukiwa katika hali hiyo? Acha kuwa ndege asiyejenga kiota anza
kujenga kiota chako, nakushauri anza leo kwa kuchukua maamuzi sahihi. Udhaifu ulionao
ubadilishe ukutie nguvu ya kufanikiwa zaidi.
Unaanzi
Wapi Sasa.
Kwanza jifunze kutengeneza pesa, ongeza ufahamu na
maarifa akilini, usianze kwa kutumia nguvu anza kwa kuongeza ufahamu.Ufahamu
utaupata kwa kusoma vitabu na kuongea na watu walioanza kujenga viota vyao.
0 comments:
Chapisha Maoni