Jumatatu, 4 Aprili 2016

Je Umejijengea Himaya Yako? Kama Bado Ijenge Sasa!


Neno Himaya linamaana zaidi ya moja lakini maana ninayozungumzia hapa ni biashara kubwa(extensive) inayoongozwa na mtu mmoja au kampuni. Mfano kwa Tanzania ni Himaya ya Said Salim Awadh Bakhresa.
 
Mpenzi msomaji wangu ninaamini kuwa makala hii itakusaidia kukutia hamasa ikiwa unandoto za kufika mbali kiuchumi. Hakuna kazi ngumu kama kujenga kitu kikubwa kisichokuwepo na ambacho wewe ndiye mwanzilishi wake. Inahitaji juhudi kubwa, maarifa mengi, uzoefu wa kutosha, ubunifu mwingi na zaidi ya hayo inahitaji maono dhahiri.

Dr.Laura Schlessinger, Mwandishi wa vitabu na mtoa maada wa vipindi vya redio huko Marekani aliwahi kusema “Usijaribu kufanya jambo lolote ikiwa haujajiandaa kukabiliana na changamoto zinazotokana na jambo hilo”.

Mimi nasema usijaribu kuanza  kujenga himaya yako ikiwa hauna kiu ya dhati ya kuwa na himaya. Ni gharama kubwa zinahitajika sio gharama za pesa tu bali na gharama ya muda, mawazo,elimu,na ushindani nk.
Elimu yako ya darasani inaweza kukusaidia kidogo
sana kwenye ujenzi wa himaya hiyo. Nasema hivyo kwa sababu huku mtaani watu wengi waliofanikiwa kujenga himaya zao wengi wao hawajasoma sana. Kama wewe umesoma hiyo ni msaada wa ziada utakusaidia kwa namna moja au nyingine. Nitakupa  mfano wa Said Awadh Bakhresa.

Mapitio ya Said Salim Awadh Bakhresa.
Bakhresa amezaliwa mwaka 1949 huko Zanzibar. Akiwa na miaka kumi na nne (14) tu aliacha shule na akaanza kukaanga chips na baadaye alifungua mgahawa wake maeneo ya kariakoo jijini Dar es Salaam. 
Miaka ya 1970 aliweza kufungua mashine ya kusaga unga na mpaka  sasa ana kiwanda kikubwa cha kusaga unga pale Kipawa, Dar es Salaam. Kiwanda hicho kinaitwa “Kipawa Flour Mill” ambacho kinasambaza unga wa ngano na mahindi Tanzania nzima na Afrika Mashariki kwa ujumla hasa katika nchi ya Rwanda na Burundi
 
Said Salim Bakhresa ametumia miaka 30 ( miongo mitatu) kujenga himaya yake ya biashara ambapo mpaka sasa kwa mujibu wa gazeti la Marekani la Forbes la mwaka jana 2014 limemtaja Bakhresa akiwa na utajiri wa zaidi ya dolla za kimarekani milioni 575, huku akiwa nafasi ya 44 kati ya matajiri 50 wa kwanza barani Afrika. Katika makampuni yake yote anaajiri zaidi ya wafanyakazi 2000.
 
Kwa sasa ana miliki makampuni mengi huku kampuni la azam, likifanya vizuri zaidi sokoni. Amejikita katika biashara ya kutengeneza vinywaji, chokoleti, na kutoa huduma ya vyombo vya usafiri kama vile meli na magari,pia akiwa amewekeza kwenye sekta ya habari akiwa anamiliki kituo cha luninga, na katika michezo hajabaki nyuma akiwa anamiliki timu ya mpira wa miguu ya Azam FC. Hayo ni machache tu kwa kuyataja.

Kujenga Himaya Yako Inawezekana.
Unaposema kujenga himaya, ni kitu kikubwa sana na ni watu wachache wenye uthubutu wa kuchukua hatua kuelekea huko. Lakini utashangaa watu wengi hata kule kuanzisha kile kidogo ni ngumu sana. Tatizo nini ni? Sio rahisi kulijibu swali hili lakini ninachotaka ufahamu kuwa jambo lolote linawezekana ikiwa kuna mambo haya mawili ya awali;  
Wazo (Idea) na Kiu (Desire). Mambo hayo mawili ndiyo chimbuko la mambo yote katika maisha ya mwanadamu. Ukikosa kimojawapo kati ya hivyo hakuna kipya utakachokifanya, mfano ukikosa Wazo hata kama una Kiu kiasi gani utashindwa ufanye kipi utatangatanga mara ujaribu hiki mara ujaribu hiki matokeo yake ilikuwa asubuhi hatimaye inafika jioni yaani unazeeka bila kitu kipya ulichofanya. Pia, ukiwa na wazo halafu ukakosa kiu ya kulitekeleza wazo hilo kwa vitendo utakuwa ukienda kwenye makundi ya watu wanaozungumzia mawazo yao unakuwa wa kwanza kuelezea aisee yaani mimi napanga kufanya hiki na hiki Mungu tu anisaidie ukitoka hapo hutekelezi hata kimoja.

Watu Wengine Waliofanya Maajabu Katikati Ya Mazingira Yalioonekana Haiwezekani.
David Ben- Gulion Waziri Mkuu wa kwanza wa Israel alitoa agizo kwamba kijengwe chuo kikuu katikati ya jangwa la Negev lililoko kusini mwa Israel. Wananchi wa nchi ile walilalamika na kunug’unika wakisema haiwezekani kujenga chuo kikuu jangwani hii haitawezekana kabisa, walisema hivyo; lakini yeye aliendelea na msimamo wake wa kujenga chuo kikuu hicho. 
Hivi sasa hicho chuo kimeshajengwa na kinaitwa Be-Gulion University ni miongoni mwa vyuo vikuu vichache duniani vinavyofundisha masomo na utafiti wa majangwa. Alifanikiwa kwa kuwa na kiu na wazo ambalo aliamua kulitekeleza kwa vitendo ndio maana  alichukua hatua na alifanikiwa.

Kule Uholanzi, waliweza kutengeneza nchi mpya kwa kile kinachoitwa Land Reclamation. Ni kitu cha ajabu kutengeneza nchi ndani ya bahari lakini walifanikiwa.

Thomas Edson aliweza kutengeneza bulb za umeme ingawaje alifeli mara elfu kumi (10,000) kabla ya kufanikiwa. 
Kilichowasaidia hao wote ni kiu na wazo kisha wakachukua hatua.
Mambo Haya Yatakusaidia Na Kukutia Moyo Wakati Unapoanza Safari Yako Ya Kujenga Himaya Yako.

Jambo la kwanza: Tafuta Sababu Ya Kuwa Na Himaya Yako.
Sababu ya wewe kuwa na himaya ni muhimu sana unapotaka kujenga himaya yako. Ndiyo itakuwa inakuchochea uwe na bidii ya kupiga hatua zaidi kuelekea kwenye himaya yako.Baadhi ya sababu unazoweza kuzitumia kama kigezo cha wewe kujenga himaya yako ni hizi zifuatazo; lakini unaweza kuweka za kwako.
  1. Kusaidia watu wengi zaidi. Mfano kuna rafiki yangu mmoja alisema yeye anatamani sana katika himaya yake anayoijenga aje aajiri angalau watu miatatu (300) kwa sasa amefikisha watu miamoja (100).
  2. Kufanya chochote unachokitaka. Mfano kusafiri kwenda popote duniani, kumiliki aina yoyoye ya gari unaoitaka, kujenga na kuishi kwenye aina yoyote ya nyumba unayoitaka n.k
  3. Kwanini wawe wao na sio mimi?.hii ni sababu tosha ya kukufanya ujenge himaya yako. Kwanini wao tu waitwe matajiri halafu mimi niitwe masikini?. Nguvu ninazo, uwezo ninao fursa ninazo sasa kwanini wawe wao nasio mimi?
  4. Iwe ndo “hobby” yako. Ndiyo, ukiwa na himaya yako na ukaijenga vizuri inakuwa kama hobby fulani hivi. Kila unapotembea kutoka sehemu moja ya himaya yako kwenda sehemu nyingine unajisikia kuburudika zaidi au una “enjoy life”
  5. Njia mojawapo ya kumshukuru na kumtukuza Mungu. Unajenga himaya yako kwa lengo la kumpa sifa na utukufu Mungu wako. Ndivyo walivyofanya matajiri wa zamani kama Ibrahimu na Mfalme Sulemani.
Jambo la Pili: Weka Kwenye Maandishi Na Kisha Andaa Ramani Yake.
Huwezi kujenga himaya bila mwongozo wa maadishi. Unatakiwa uandike kila hatua utakayopitia. Kwa jina jingine inaitwa “Financial Plan”.  
Kama hufahamu namna ya kuandika financial plan tafuta mtu mwenye uelewa akusaidie kuandika. Financial plan inakupa dira au mwelekeo wa namna ya kujenga himaya yako. Pia jambo kubwa kabisa, inakuonyesha muda utakao tumia hadi kujenga himaya yenye nguvu. Kama vile mtu anayejenga nyumba huandaa ramani, ramani hiyo sio tu kumwonesha fundi vipimo bali pia inamhamasisha anayejenga kila aionapo anatamani zaidi aendelee kujenga ili aikamilishe. 
Bila ramani kunakukosea vipimo lakini pia hukatisha tamaa maana huoni mwisho wake utakuwaje. Vivyo hivyo unapojenga himaya yako lazima uandae andiko (financial plan) itakayo kusaidia kuiona himaya yako ukiwa mwanzoni.

Jambo la Tatu: Chukua Muda Kupata Maarifa Na Kutafuta Fursa.
Itahitaji muda kidogo kujifunza mambo muhimu ya awali mfano sheria za uendeshaji biashara, namna ya uwekezaji, masoko na hesabu na uhasibu. Mambo hayo ni muhimu unapotaka kujenga himaya yako. Pia kutafuta fursa ni jambo ambalo unatakiwa ulipe kipaumbele ili utakapo anza kujenga himaya yako uwe unajua fursa zipo sehemu gani, na itakuwa rahisi kwako kuzitumia. 
Utajifunza mambo hayo yote kwa kusoma vitabu, kufanya maongezi na watu wenye himaya tayari, kuzungumza na watu wenye fani unazotaka kuzitumia mfano, wanasheria, wahasibu, wafanyabiashara n.k. njia nyingine nzuri ni ya kutembelea miradi na kujifunza namna ya uendeshaji wa miradi hiyo.

Jambo la nne: Kuna kitu kinaweza kukutoa nje ya mstari
Kuna mambo mengi yanatakiwa kukamilishwa au mengine utaendelea nayo huku ukiendelea kujenga himaya yako. Jambo la muhimu kabisa ni kulishika ni nidhamu katika hatua hii. Tena, kumbuka kutunza afya yako ili ufikie malengo yako. Tabia zozote zinazokutoa kwenye mstari wa ujenzi wa himaya unatakiwa uziepuke au uziache. 
Mungu ni muhimu sana kumshirikisha ili akutie nguvu za kujenga  himaya yako. Unatakiwa kujifunza kila siku wakati wote ukiwa unajenga himaya yako kwa kusoma vitabu na kwa namna yoyote itakayo kuongezea ufahamu na bidii ya kuendelea kujenga himaya yako.

“Hakuna kazi ngumu kama kujenga kitu kikubwa kisichokuwepo na ambacho wewe ndiye mwanzilishi wake. Inahitaji juhudi kubwa, maarifa mengi, uzoefu wa kutosha, ubunifu mwingi na zaidi ya hayo inahitaji maono dhahiri.”

0 comments: