Ujue ukweli nao utakuweka huru.
Hii ni kauli ambayo huwa inatumika kwenye falsafa za dini mbalimbali. Ili tuwe na maisha bora na ya uhuru, ni lazima tuujue ukweli. Kutokujua ukweli kunatufanya tuwe watumwa na tushindwe kuzitumia fursa mbalimbali zinazotuzunguka kwenye maisha yetu.
Pamoja na umuhimu huu wa ukweli, bado ukweli umekuwa ni kitu kigumu sana kwa watu wengi kuujua. Unaweza kushangaa kwa nini baadhi ya watu wanafanya mambo ambayo wewe huwezi kufanya kabisa, wakati wao wanaona wako sahihi sana kwa kile wanachofanya.
Linapokuja swala la kuujua ukweli, kuna mitazamo miwili.
Mtazamo wa kwanza wa ukweli.
Mtazamo wa kwanza ni kwamba naujua ukweli na chochote kinachoenda tofauti na hiki siyo kweli.
Huu ndio mtazamo ambao asilimia zaidi ya 90 ya watu wote duniani wanao. Tuna upendeleo kwa kile ambacho tunakijua au kukizoea. Na tunachukulia huu ndiyo ukweli pekee uliopo, hakuna ukweli mwingine zaidi ya huu.
Mtazamo huu kuhusu ukweli umekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wengi kuweza kuchukua hatua za kuboresha maisha yao. Hii ni kwa sababu watu wameshaamua kuchagua njia fulani na hawapo tayari kujaribu njia nyingine inayopingana na ile waliyozoea.
Mtazamo huu wa ukweli kuwa kile ambacho tunaamini sisi umejengwa kwa muda mrefu sana kwetu na umepewa msisitizo na jamii tulizokulia, elimu tulizopata na imani za kidini tulizonazo.
Jamii inatuaminisha vile ambavyo waliotangulia walikuwa wakiamini, na hivyo tunakua tukijua kitu fulani kiko hivi, tunapopata taarifa nyingine ambayo ni kinyume na tunavyoamini, tunapinga na kukataa kabisa. Tunaendelea kushikilia kile ambacho tumekuwa tunaamini siku zote. Hii ndiyo sababu ya kuwepo na baadhi ya mila ambazo hazina maana lakini bado watu wanazishikilia.
Kwenye mfumo wa elimu, tunapewa njia moja ya kuiendea dunia, njia hii inaaminika ndiyo njia pekee na bila ya njia hii hakuna maisha bora. Watu wengi wamekuwa wakiaminishwa hawawezi kuwa na maisha bora kama hawakupata elimu kubwa sana. Watu hawa wakipewa taarifa tofauti kwamba wanaweza kuwa na maisha bora wanakataa kwa sababu wanachoamini ni tofauti. Au kwa mwajiriwa kuweza kuondoka kwenye ajira na kujiajiri, inakuwa vigumu kwa sababu imani yake yote ni kwamba njia ya uhakika ya kuingiza kipato ni kupitia ajira. Hivyo atakapopata taarifa tofauti na ukweli aliopokea, hawezi kukubaliana nazo.
Mtazamo wa pili wa ukweli.
Mtazamo wa pili ni kuwa tayari kujifunza vitu vipya. Huu ndio mtazamo unaowapeleka watu kwenye ukweli na kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Katika mtazamo huu mtu anajua ya kwamba pamoja na kile ambacho amekuwa akiamini kwa muda mrefu, bado kuna vitu vingi sana ambavyo havijui. Na hivyo anakuwa tayari kujifunza pale anapopata nafasi ya kujifunza.
Mtu mwenye mtazamo wa kupokea na kujifunza kwa mambo mapya, anaondoa upendeleo wowote kwa kile anachoamini ni ukweli, na anachukua taarifa, kuifikiria kwa kina na kisha kuondoka na kitu anachoweza kukifanyia kazi, ili kuboresha maisha yake zaidi.
Mtazamo huu wa pili ndio umewezesha sayansi kukua na uvumbuzi mpya kupatikana kila siku. Hata kama kitu kipo sahihi kabisa, watu bado wanaendelea kuhoji ubora wake na kama kinaweza kuwa bora zaidi. Na kwa njia hii tumeshuhudia ukuaji mkubwa sana kwenye teknolojia.
Kutumia mtazamo wa ukweli katika ukuaji binafsi.
Teknolojia inakua kwa kasi sana kuliko ukuaji wa binadamu. Hii ni kwa sababu watu wapo tayari kuhoji kuhusu vitu lakini sio kujihoji wao wenyewe.
Huwezi kuwa na maisha bora kama hukui, na sio kukua tu kimwili, bali kukua kiakili na kukua kiroho. Kukua kimwili ni rahisi, kwa sababu unakula basi utakua. Ukuaji wa akili unafanyika kwa kiasi, kama unapenda kusoma na kuongeza maarifa utakua kiakili.
Ni ukuaji wa kiroho ndipo ambapo wengi wamekwama. Na tunakwama kwenye ukuaji wa kiroho kwa sababu hatupo tayari kujifunza vitu vipya, hatupo tayari kupokea ukweli mpya, tumechagua kuamini kitu kimoja na kuona hiki ndio chenyewe. Tunapopata taarifa nyingine zinazoendana tofauti na kile tunachoamini, wala hatujiulizi mara mbili, badala yake tunakikataa mara moja na kuona hakifai kabisa.
Hatua ya kuchukua.
Unahitaji kubadili mtazamo wako juu ya ukweli, usione kwamba kile unachoamini ndio ukweli pekee, kuwa tayari kupokea hata kile ambacho ni tofauti na unachoamini. Na hupokei tu kwa kutumia moja kwa moja, badala yake unapokea na kuchunguza kwa undani, kisha unaona ukweli uko wapi.
Ujue ukweli na ukweli utakuweka huru. Na ukweli sio huo unaojua sasa, ukweli ni mkubwa sana na unajua sehemu kidogo sana ya ukweli. Kuwa tayari kujifunza vitu vipya, kuwa tayari kuchunguza kwa makini na utaona ni jinsi gani kuamini kitu kimoja kunakuzuia kuujua ukweli.
Nakutakia kila la kheri katika kuijenga falsafa mpya ya maisha yako, ambayo itakuwezesha kuwa na maisha bora, ya furaha na mafanikio makubwa. kumbuka kila kitu kinaanza na wewe binafsi, hivyo fungua akili yako, jipe ruhusa ya kupokea maarifa mbalimbali, fikiri kwa kina na kisha chukua hatua.
*****************************
0 comments:
Chapisha Maoni