Jumapili, 27 Machi 2016

Tabia Na Kanuni Zinazoongoza Maisha Yako Zinazoweza Kukujenga Au Kukubomoa


“Nyimbo nzuri zinazosikika ni tamu lakini nyimbo nzuri zisizosikika ni tamu zaidi”.
 
Hayo ni maneno yake John Keats, mtunzi mashuhuri wa mashairi kutoka Uingereza. Mtunzi huyu anataka tufahamu kuwa maneno yale yanayotoka kinywani mwa mtu na kusikika si yale yaliyomo ndani ya mtu huyo, maana yale yanayotoka nje ya mtu hayawezi kumfanya mtu awe jinsi alivyo bali maneno yale yanayosema kwa sauti ya chini isiyosikika ndiyo yanamfanya mtu awe jinsi alivyo. Hali hii ni dhahiri kabisa katika maisha yetu. 
 
Mara nyingi watu wanapenda waonekane wazuri na wenye jambo jema wakiwa mbele za watu, husema kwa namna ya kujisifia katika mambo fulani fulani ili mradi tu waonekane wema. Lakini ukweli ni kwamba ndani ya watu hawa huwa kuna maneno yanayosikika kwa sauti ya chini chini  yakimsema mtu huyo jinsi alivyo, haya maneno ndiyo yanayomfanya mtu awe jinsi alivyo kuanzia tabia, sura yake, mwenendo wake wa kila siku na hali yake ya mahusiano na watu wengine, wakati mwingine huathiri afya ya mtu huyo.

Mtu Mmoja Ni Watu Wengi Ndani Yake.
 
Usishangae ndivyo ukweli ulivyo, ndani ya mtu mmoja kuna mawazo zaidi ya maelfu kadhaa yanayopita kila wakati na kila wazo linaongea maneno yake. 
 
Don Miguel Luiz anayaita mawazo hayo watu wengi. Mawazo yale yanayopita mara kwa mara ndani ya mtu ndiyo yanayotengeneza fikira ya mtu hiyo. Fikira ni mkusanyiko wa mawazo ya muda mrefu ndani ya mtu yanayofanya tabia ya mtu huyo iwe jinsi ilivyo. 
 
Tabia za mtu zinajengwa na mawazo hayo na ikitokea kila wazo linaongea bila kumsikiliza mwenzake huwa hakuna maelewano ndani ya mtu huyo na hali hiyo huitwa msongo wa mawazo.
 
Tabia  ya mtu na kanuni zake za kuishi zinatengenezwa kwa namna hii ya mawazo kupita ndani yake. Mawazo yale yanayopita mara kwa mara hutengeneza fikira na fikira ya mtu hutengeneza tabia. Hivyo mtu huishi kwa kufuata fikira na tabia hizo. Sasa, tabia hizo zinaweza kuwa nzuri au mbaya kwenye kila hali, mfano kwenye swala la afya, akili,mahusiano, familia nk.
Utoaji Wa Maamuzi Yako.
 
Umekuwa ukifanya maamuzi yako kwa namna gani punde unapokutana na jambo linalohitaji kufanyiwa maamuzi? Mfano kwenye biashara yako, masomo yako, kwenye mahusiano yako, kwenye kuchukua hatua za mafanikio yako nk. 
 
Namna unavyofanya maamuzi ndiyo tabia yako ilivyo kwenye swala la maamuzi yako. Kama huwa unatoa maamuzi kwa jaziba haraka haraka je, umeshagundua inakuletea madhara gani? 
 
Mara nyingi mtu anayetoa maamuzi haraka haraka baadae akija kutulia hugundua kuwa uamuzi wake haukuwa sahihi na mara nyingi hujuta au hupata gharama kubwa sana. Namna ya utoaji maamuzi ni tabia ambayo ukiitumia vizuri inaweza kukusaidia na kukujenga lakini ukiitumia vibaya inaweza kukuharibia kabisa baadhi ya mambo muhimu. 
 
Jichunguze sasa uone udhaifu wako kwenye utoaji wa maamuzi uko wapi kisha chukua hatua za namna ya kujithibiti kulingana na namna unavyohitaji. Ikiwa unatabia ya kutoa maamuzi haraka haraka na imekuwa ikikugharimu, basi tengeneza utaratibu mzuri wa kufikiri na kutoa maamuzi.

Afya Yako Inategemea Tabia Yako
 
Tabia yako na kanuni zako za maisha zinamchango mkubwa sana kwenye afya yako.  Kama unatabia ya kula baadhi ya vyakula vinavyoathiri afya yako, kwa asilimia kubwa afya yako itaathirika. Au kama unatabia mbaya zozote zinazohatarisha afya yako basi kuna uwezekano kweli afya yako inaweza kuathirika kwa namna moja au myingine. 
 
Siku moja nilikuwa nazungumza na Mkurugenzi wa kampuni fulani katika mazungumzo yetu ya kawaida akanambia jambo muhimu sana katika maisha ni afya. Tena akaendelea kusema  “Unapokuwa na ndoto za kuanzisha kampuni lako binafsi, kitu cha kwanza ni kutunza afya yako maana kama afya ilategalega ufanisi wako katika  kampuni utayumba”.
 
Kuna msemo usemao “afya ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu”. Hilo ni kweli lakini tabia zako zinamchango mkubwa sana kwenye afya yako. Tabia yako na kanuni zako za kuishi zinaweza kujenga au kubomoa afya yako. Chukua hatua madhubuti juu ya afya yako mwenyewe.

Fani Yako Na Taaluma Yako Vinaendeshwa Na Tabia Yako.
 
Mara nyingi nimeona madaktari bingwa wanavuta sigara. Lakini akienda mtu mwenye matatizo ya upumuaji utakuta wanamshauri ikiwa ni mvutaji sigara aache kuvuta sigara! kinachoshanishangaza mbona  yeye anayekwambia usivute sigara tena ni daktari na anajua madhara ya sigara na haachi kuvuta sigara?. 
 
Sio upande wa madaktari tu bali ni kila fani na taaluma za watu kuna miiko wanaojifunza inayowakataza kufanya mambo fulani kwa faida yake mwenye fani hiyo mfano waalimu, wanasheria, wahasibu, nk. lakini tunaona wengi hawatii mafunzo hayo yenye thamani kwao. Kumbe tatizo ni tabia na kanuni za maisha, mara nyingi ndizo zinaamua maisha ya mtu huyo yaweje.  
 
Unatakiwa kufanya maamuzi magumu punde unapogundua kuwa tabia inakupeleka kubaya ni lazima kusema hapana kwa tabia hiyo. Kutochukua hayo maamuzi magumu kunapelekea kujengeka au kubomolewa katika misingi sahihi ya mafanikio yako.

Tabia Yako Hutafuta Watu Wenye Tabia Inayofanana Nayo.
 
Je, umeshawahi kukaa kwenye kundi la watu wenye tabia tofauti na wewe? Ulijisikiaje?. Bila shaka ulijisikia mpweke japokuwa umezungukwa na watu wengi. Sio wewe bali ni tabia yako ilikuwa haifurahii watu wenye tabia hiyo. Sio kwamba unawachukia bali tabia yako inapiga kelele ndani yako kwa sauti ile isiyosikika ikisema hapa sio mahala pangu hapa sio mahala pangu. Kwa kelele hizi za tabia zako utajikuta unakosa amani katikati ya watu hao lakini utashangaa wenzako wenye tabia zinazoendana wanafurahi na kushangilia.
Jichunguze, huwa unajisikia kuwa na watu wenye tabia gani? Kama huwa unajisikia vizuri kukaa na watu wanaopenda kuzungumzia mafanikio basi hilo ni tumaini ipo siku utafanikiwa na kama unapenda kukaa na watu wasemaji, wenye maneno mengi yasiyofaa ujue kuwa unaharibikiwa maana mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Chukua hatua mapema juu ya tabia na mienendo ya maisha yako kwa sababu kuna kujengeka au kubomolewa.

Tabia Ya Macho na Moyo Ni Mzizi Wa Mambo Mengi.
 
Macho yanatabia. Yanaweza kufundishwa namna ya kuangalia na anayeyafundisha macho kuangalia ni moyo. Moyo hufundisha macho na hudhibiti tabia ya macho. Mfano kipindi mimi nipo mdogo darasa la nne hivi nilikuwa napenda sana ngoma lakini sikuwa na fursa ya kwenda ngomani maana nilikuwa bado mdogo hivyo sikuwa naruhusiwa, moyo ulikuwa unaumia sana kwa kukosa fursa hiyo. Moyo ulikuwa unafurahi sana siku nikipewa nafasi ya kwenda kuona ngoma hizo, moyo ulikuwa unaridhika ukiona. Kadri nilivyokuwa nakua moyo uliacha kutamani tena ngoma na kwa sababu hiyo uliyafundisha macho kutopenda kuangalia ngoma na ndivyo nimekuwa hadi leo. 
 
Bila shaka mpenzi msomaji umeshawahi kukutana na kitu fulani kikakuvutia sana ukajilazimisha kutokiangalia ila moyo ukaanza kupiga kelele nataka nikione nataka nikione nataka nikione, usipouzuia moyo utageuka kuangalia kitu hicho ndivyo tabia ya moyo kuyasakizia macho kuona hata kama jambo hulipendi kuliona. 
 
Kinachotakiwa ili kuweza kuitawala tabia ya macho na moyo isiweze kukuvuruga. Unatakiwa kujifunza namna ya kuzishinda tabia za moyo na macho. 
 
Ziko mbinu nyingi za kushinda tabia hizi mfano kwa kusoma neno la Mungu na kulitenda katika maisha yako. Chunga moyo wako kuliko mambo yote maana unaweza kukujenga au kukubomoa.
“Maana Yale Yanayotoka Nje Ya Mtu Hayawezi Kumfanya Mtu Awe Jinsi Alivyo Bali Maneno Yale Yanayosema Kwa Sauti Ya Chini Isiyosikika Ndiyo Yanamfanya Mtu Awe Jinsi Alivyo”.

0 comments: