Hii ni Hadithi nzuri
inayoweza kubadilisha siku yako
Kulikuwa na kijana mmoja
mdogo mwenye umri wa miaka minane (8), alimwendea babu yake na kumwuliza; “Babu
nataka nifanikiwe sana kwenye maisha yangu. Naomba unipe mbinu za kufanikiwa”.
Babu akamwangalia mjukuu wake kwa muda kidogo bila kumjibu kitu, baadaye
akamwambia “nifuate”; basi yule kijana mdogo akaongozana na babu yake kwenda
kwenye kitalu cha miti. Walipofika pale
walinunua miche miwili ya miti kisha wakarudi nyumbani.
Walipofika nyumbani babu
akachukua mche mmoja wa mti kati ya ile miwili waliyonunua akaupanda nje kidogo kwenye eneo
la wazi karibu na nyumbani. Kwa kawaida eneo ambalo alikuwa anaishi babu huyo
na mjukuu wake lilikuwa kame na linaupepo mkali sana ambao hutimua vumbi kubwa.
Miti mingi mikubwa huvunjika matawi yake kutoka na upepo huo.
Mche wa pili, babu
aliupanda kwenye chungu kilichojazwa udongo wenye unyevunyevu. Kisha hicho
chungu akakiweka pembeni ya nyumba karibu na dirisha kwenye eneo lenye kivuli. Mara
baada ya kupanda miche yote, babu akamwuliza mjukuu wake unafikiri ni mche upi
utasitawi sana?. Bila kusita kijana
akasema nafikiri huu uliowekwa kwenye chungu utasitawi sana kwa sababu
unaudongo wenye unyevunyeu lakini pia sio rahisi upepo au ukame kuuathiri mche
huu.
Baada ya majibu hayo babu
hakumjibu kitu mjukuu wake. Siku si nyingi yule kijana alianza masomo, baada ya miaka mitatu akarudi nyumbani kwa
babu yake wakati wa likizo. Siku ile walifurahi wote kuonana baada ya muda
mrefu kupita, Siku hiyo waliendelea na mazungumzo yao. Yule kijana akamwuliza
tena babu yake; “Babu nilikuuliza swali, mimi nataka kufanikiwa zaidi maishani
mwangu nifanye nini? Kipindi kile nilikuuliza hukunijibu naomba unijibu leo
basi;.
Babu akamwambia mjukuu
wake twende tukaiangalie miti tuliyopanda siku zile. Wakaenda kuangalia,
alichoshangaa yule kijana aliukuta ule mti walioupanda nje kwenye uwazi na
kwenye eneo lenye upepo mwingi, ulikuwa umestawi sana na ulikuwa mrefu wenye
afya kuliko ule mti waliopanda kwenye chungu. Uliopandwa kwenye chungu ulikuwa
haujasitawi sana wala haukurefuka kama ule mwingine hata haukuwa na matawi
mengi kama ule mwingine.
Kijana alishangaa sana
maana alichokiona ni kinyume na jinsi alivyokuwa anafikiria. Kisha babu yake
akamwambia; “Kama unataka kufanikiwa
sana ni lazima ukubali kupambana na changamoto wala usithitubutu kukimbilia
kivulini. Unapokuwa kivulini anga halitakutuza tuzo bali litamtuza aliyejuu
yako na wewe utabaki kwenye udongo wenye unyevunyevu lakini huna mizizi imara
wala matawi yako hayatasitawi sana”.
Babu akaendelea kumwambia
mjukuu wake; Umeuona ule mti tuliopanda kwenye eneo la wazi umestawi sana kwa
sababu ulikumbana na changamoto nyingi sana za ukame na upepo mkali, changamoto
hizo zimefanya mizizi ya mti huo izame chini sana ili kuyafikia maji mengi lakini
pia ili kujilinda na upepo mkali.
Zaidi ya yote anga
hukituza kitu chochote kinachosimama chenyewe kikaonekana. Kwahiyo na wewe
ukitaka kufanikiwa mjukuu wangu ni lazima ujifunze kuonekana kama wewe wala
usithubutu kuwa kivulini mwa mtu mwingine kwa sababu ukiwa kivulini mwa mtu
mwingine atakayeonekana ni yule anayekupa kivuli na anga litampa tuzo huyo. wala
sio wewe.
Kumbuka ule mti tulioupanda
kwenye chungu, tuliweka udongo unaoweza kujaza chungu hicho, kwa maneno mengine
tulipima udongo wenye kutosha kujaza chungu hicho lakini ule mti tulioupanda
nje kwenye eneo la wazi haupimiwi udongo, udongo wote ni wake. Vivyo hivyo na
wewe mjukuu wangu kama unataka kufanikiwa epuka mtu fulani kukupimia kiasi cha
mafanikio yako. Mtu anayekupimia pesa anataka usisitawi sana. Kwanini usiwe
huru kupata kiasi chochote cha mafanikio unayotaka bila kupimiwa? Jifunze mjukuu
wangu kuwa huru kama vile mti tulioupanda kwenye eneo la wazi ulivyokuwa huru
ndio maana ulistawi sana.
Mjukuu wangu nataka kukuambia kwamba wanaofanikiwa
zaidi ni wafanyabiashara na wajasiriamali kwa sababu hawapimiwi pesa bali
wanakusanya bila kikomo. Fanya hivyo mjukuu wangu kisha utafanikiwa na siku
zote ikumbuke mifano hii ya miti miwili itakusaidia sana kufanikiwa kwako.
Yule kijana alifurahi sana
majibu yenye busara ya babu yake na alimwahidi babu yake kwamba atayatenda kwa
vitendo mafundisho yake.Mwisho wa hadithi.
Bila shaka umejifunza
mengi kutokana na hadithi hii. Jitahidi uyafanyie kazi unayojifunza.
Tunapenda kusikia kutoka kwako pia kupitia comment zako!