AINA ZA UKATILI WA KIJINSIA
UKATILI wa kijinsia ni jambo kubwa
kwenye ajenda za haki za binadamu kimataifa, na unaweza kuwapata
wanaume, wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakubwa.
Hali hii
inatokana na mifumo mbalimbali iliyopo na uhusiano wa kijinsia ulivyo
katika jamii zetu hapa nchini ambapo jinsi moja hujiona ni bora kuliko
nyingine.
Kwa miaka mingi mwanaume amechukuliwa kuwa daraja la juu
kuliko mwanamke katika nyanja zote za kijamii, kiutamaduni, kisiasa na
kiuchumi.
Utaratibu huu umejengwa tangu enzi na enzi katika ngazi ya familia hadi taifa.
Kuna aina tofauti za ukatili wa kijinsia na hii inategemeana na utamaduni na historia ya jamii husika.
Mara nyingi ukatili huu hufanyika kati ya wanandoa au wapenzi. Hata
hivyo wanawake wamekuwa wakisumbuliwa zaidi na ukatili wa kijinsia
katika uhusiano huo.
* Ukatili wa kimwili.
Ukatili wa kimwili ni kitendo anachofanyiwa mtu kinachohusisha kuumizwa mwili na huweza kuonekana moja kwa moja.
Wakati mwingine mtendewa ukatili anaweza kuyahisi maumivu bila mtu mwingine kutambua kuwa amefanyiwa ukatili wa kimwili.
Baadhi ya mifano ya ukatili kimwili ni pamoja na vipigo, shambulio la
mwili, kuchomwa mwili moto, matumizi ya silaha, kuvuta nywele, kusukuma,
kumpiga kichwa ukutani na kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu
yoyote mwilini.
* Ukatili wa kisaikolojia.
Ni ukatili
ambao mtu anatendewa na unamsababishia maumivu kihisia, ambapo mtu
mwingine hawezi kutambua kuwa mwenzake ametendewa ukatili hadi mazingira
yatakapojitokeza na mtendewa akajieleza.
Mifano ya ukatili wa aina
hii ni pamoja na matusi kwa njia ya maneno au ishara yenye lengo la
kudhalilisha, vitisho na kutishia kufanya fujo, maneno ya kufedhehesha,
kudharauliwa hadharani, kutishia kutoa siri, kuingiliwa faragha,
kutishiwa kuuawa, wivu wa kupindukia ama kunyang’anywa watoto kwa
makusudi.
* Ukatili wa uhusiano wa kingono.
Ukatili huu huambatana na vitendo vinavyohusiana na masuala ya ngono.
Kwa mfano bughudha za kijinsia, kujamiiana kwa maharimu, ubakaji ndani
ya ndoa, ulawiti, utekaji na usafirishaji wa wanawake au wanaume na
watoto kwa ajili ya ngono, utumwa wa kingono, mashambulio na kuingiza
vitu vigumu kwenye sehemu za siri.
Vitendo vingine ni kujaribu
kulazimisha ngono, kuweka mazingira ya ngono isiyo ya ridhaa au ubakaji,
kupima ubikira, kulazimisha kutoa mimba, kukataza matumizi ya utaratibu
wa kuzuia mimba, kulazimisha mimba, kulazimisha ngono bila kujali
kuambukiza magonjwa na kulazimishwa kufanya biashara ya ukahaba.
* Ukatili wa kiuchumi.
Ukatili wa kiuchumi ni aina ya ukatili ambayo inamnyima fursa za
kiuchumi mwanamke au mwanaume katika kujiongezea kipato na kuchangia
katika maendeleo.
Aina hii ya ukatili huwapata wanawake kutokana na hali yao ya kuwa tegemezi kwa wenzi wao.
Kitendo cha wanawake kuwa tegemezi kwa wanaume kinawaathiri sana kwani
wanakosa kauli katika mali za familia na hawashirikishwi katika uamuzi
wa maendeleo.
Waaathirika wakubwa wa aina hii ya ukatili ni wanawake na wasichana.
Mifano ya ukatili wa kiuchumi ni kama vile kunyang’anywa mali, ubaguzi
katika fursa za kujipatia mahitaji muhimu kama chakula, malazi na
mavazi, kunyimwa haki za kurithi, elimu duni na mianya finyu ya fursa za
kujielimisha, kunyimwa sehemu ya mapato ambayo ni jasho lako na
kukatazwa kufanya kazi.
* Ukatili wa mila potofu. Ukatili huu
unatokana na mila na desturi za jamii zetu ambazo zinakinzana na haki za
binadamu, hivyo kuchangia kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Baadhi ya mifano ya ukatili wa kijinsia unaotokana na tamaduni au mila
potofu ni kama vile ndoa za kushurutisha, ndoa za utotoni, kutakasa
wajane, kurithi wajane, ukeketaji, matambiko ya kingono kwa watoto, ndoa
za maharimu, kufungiwa au kuwekwa ndani kwa shuruti, ndoa za ushirika,
miiko ya chakula na ukatili utokanao na mahari.
* Mahali pa kupata msaada.
Mwathirika hana budi kutafuta msaada kwa mtu anayemwamini au kuripoti polisi. au wasiliana na
TABORA NEW HOPE AGENY (TANEHA) +255 753 062 458 AU +255 762 336 533
Jumatatu, 1 Februari 2016
UKATILI WA KIJINSIA
3:05:00 PM
5 comments
5 comments:
Kwani mashirika na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali wana deal na wanawake pekee kama ndio kundi pekee linalonyanyasika?
mimi nina uhakika kuwa hata wanawake pia wanawanyanyasa sana wanaume lakini wanaume wachache sana wenye ujasiri wa kujitokeza na kutoa malalamiko.
Hivyo maoni yangu ni kuwa muwajengee uwezo na wanaume ili kuwapa ujasiri wa kujitokeza kutoa malalamiko yao.
ni kweli wanawake wanaonekana kunyanyasika zaid kwa kuwa wao wanaujasiri mkubwa sana wa kulalamika tofauti na sisi wanaume ambao wengi wanaona ni aibu kubwa kulalamika kuwa wananyanyaswa na wake zao.
TANEHA fanyeni mkakati wa kuwajengea uwezo na wanaume!!
Kuna rafiki yangu mmoja anatumikia kifungo gerezani kwa sababu ya kumfanyia ukatili mkewe kwa kumjeruhi vibaya, lakini nilipomtembelea gerezani alinisimulia jinsi ambavyo mkewe alikuwa akimnyanyasa kisaikolojia kwa muda mrefu na alishindwa kuvumilia zaidi pale alipogundua kuwa mkewe anamnyanyasa kwakuwa ana bwana mwingine mwenye uwezo mkubwa ambaye mkewe alimtamkia wazi kuwa hata mtoto wao mdogo alikuwa ni wa yule jamaa wa nje.
sasa kama rafiki yangu angekuwa na ujasiri wa kujitokeza na kupata ushauri pengine asingejikuta yuko gerezani.
TANEHA Toeni elimu
ukatili ni janga kubwa sana haswa kwa huku vijijini ni balaa sana.
Tutembeleeni huku wilaya ya Uyui,Tabora mtusaidie
Ahsanteni sana wadau kwa maoni yenu. Tunaahidi kuyafanyia kazi kwa uzito wa kipekee.
endeleeni kutupa maoni yenu kila mpatapo nafasi.
With thanks
Dennis John Kumwenda - Executive Secretary
Chapisha Maoni