Jumamosi, 6 Februari 2016

ASILIMIA 15 YA WANAWAKE NCHINI WAMEKEKETWA - SERIKALI

SERIKALI imesema asilimia 15 ya wanawake nchini wamekeketwa, huku mikoa mitano ikiwa imekithiri kwa vitendo hivyo.
Mikoa hiyo na asilimia ya ukeketaji kwenye mabano ni pamoja na Manyara (71), Dodoma (64), Arusha (59), Singida (51), na Mara (40).
Akizungumzia maadhimisho ya siku ya ukeketaji leo kwa niaba ya waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Sihaba Nkinga alisema vitendo vya ukeketaji bado vimeshamiri nchini.

“Ukatili huu wa ukeketaji umekuwa ukijidhihirisha katika sura mbalimbali zikiwemo za baadhi ya makabila kuhalalisha vitendo hivyo kwa kisingizio cha mila na desturi za kabila husika,” alisema Nkinga.
Alisema ukeketaji ni udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike na huhatarisha maisha yao, lakini vitendo hivyo vinaendelea kufanyika kwa siri katika jamii huku madhara yake yakiwa ni vifo, vilema na maradhi kama fistula.
Nkinga alisema mbali na kuwepo kwa mwamko kutoka kwa jamii wa kuripoti matukio ya vitendo hivyo bado ipo kazi kubwa ya kufanya kwa kuwa suala la kubadili fikra na mitizamo ya jamii haiwezi kuisha kwa siku moja kwa kuwa vitendo hivyo bado vinaendele kutokea.
Kuhusu maadhimisho, alisema kitaifa yatafanyika mkoani Singida huku mikoa mingine ikiadhimisha kwa matukio kadha wa kadha lengo likiwa ni kuongeza uelewa kwa jamii ili kutokomezwa kwa ukeketaji nchini.

0 comments: