WATU wenye ulemavu wa ngozi (albino) kati ya 40 hadi 43 wameuawa na watu wasiojulikana katika kipindi kati ya mwaka 2006 na 2014 kutokana na imani mbalimbali ikiwemo ushirikina.
Hayo yamo katika majibu aliyotoa bungeni jana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yussuf Masauni alipokuwa akijibu swali nyongeza la Mbunge wa
Viti Maalumu, Mgeni Jadi Kadika ( CUF).
Masauni amesema katika kushughulikia suala hilo la mauaji ya albino watuhumiwa 133 walikamatwa na kati yao 19 wameshahukumiwa katika mahakama mbalimbali.
Amesema mikoa inayoongoza kwa mauaji hayo ni pamoja na Mwanza, Shinyanga na Kigoma na kuongeza kuwa polisi inaendelea kukomesha mauaji hayo kwa kuongeza ulinzi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Naibu Waziri alisema polisi kupitia Polisi jamii inatoa elimu kwa umma juu ya madhara ya vitendo vya kikatili vya mauaji na kujeruhi vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa msukumo imani potofu za ushirikina.
0 comments:
Chapisha Maoni