Jumatano, 11 Mei 2016

Usikubali Mambo Madogo Yakuharibie Siku Yako!!!


Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Maisha bila ya falsafa ni sawa na bendera iliyotundikwa. Bendera hii haina maamuzi yoyote, bali hufuata uelekeo wa upepo. Hakuna hatari kubwa ya kuishi kama kukosa falsafa ya maisha yako. kwa sababu utajikuta unafanya vitu ambavyo hujui kwa nini unafanya, na vibaya zaidi unapoteza muda na kukosa vile ambavyo ni vya msingi sana kwenye maisha yako. Ndiyo maana ni muhimu sana kujijengea falsafa ya maisha ambayo itatuongoza kwenye nyakati zote za maisha yetu.
 

Karibu tena leo tunakwenda kuangalia eneo dogo sana na la maisha yetu lakini linalobeba maana kubwa sana. Eneo hili ni yale mambo madogo madogo yanayotokea kwenye maisha yetu ya kila siku. Tunaweza kuyaona ni madogo, lakini yanahusika sana kwenye jinsi maisha yetu yanavyokwenda.
 

Siku zetu huwa zinaanza vizuri sana, tukiwa na matarajio mazuri sana, mpaka pale inapofikia hatua sisi wenyewe tunaharibu siku zetu. Nina imani umewahi kumaliza siku zako nyingi ukiwa na msongo wa mawazo, ukiwa na hasira na ukiwa unajisikia vibaya au hata kukata tamaa kabisa, si ndiyo?
 

Sasa naomba nikuulize swali moja, katika siku hizo, je uliamka asubuhi ukajiambia ya
kwamba leo lazima nimalize siku yangu nikiwa na msongo wa mawazo? Au leo lazima nimalize siku yangu nikiwa nimegombana na mtu?
 

Watu wote huwa tunaanza siku zetu na matarajio mazuri, tukiwa na matarajio chanya ya kwenda kuitumia siku vyema. Hakuna mtu anatoka kitandani akiwa na dhamira ya kuwa na siku ya hovyo, lakini siyo wote wanamaliza siku zao wakiwa vizuri kama walivyoanza. Hii ina maana kwamba kuna kitu kinatokea hapo katikati ambacho kinaharibu yale matarajio ambayo mtu alianza nayo siku yake.
 

Kitu kinachoongoza kuharibu siku za watu wengi ni mambo madogo madogo yanayotokea kwa kila mtu. Na siyo kwamba mambo haya madogo ndiyo yanaharibu siku, bali mtu anavyoyachukulia mambo haya ndiyo kunasababisha siku yake kuharibika. Kwa kifupi wewe mwenyewe ndiyo unachagua kuharibu siku yako kwa jinsi unavyochukulia yale mambo ambayo yanatokea kwenye siku yako.
 

Mambo mengi ni madogo.
Asilimia kubwa ya mambo yanayotokea kwenye maisha yetu ni mambo madogo. Na hapa nasema madogo kumaanisha kwamba hayana umuhimu mkubwa kama ambavyo tunayapa sisi wenyewe.
 

Kwa mfano umemsalimia mtu halafu hakuitika, hili ni jambo dogo sana lakini sisi wenyewe tunaweza kulikuza sana. Tunaweza kufikiria labda mtu yule ana hasira na wewe, au anakuonea wivu, au anakudharau na mengine mengi. 

Kwa fikra hizi unajijengea mtizamo hasi mtu yule na kupelekea siku yako kuwa vibaya. 
Lakini huenda mtu yule hakukusikia vizuri wakati unamsalimia, au ana mawazo mengi kutokana na matatizo anayopitia yeye binafsi. Tunaweza kuchagua kupokea jambo dogo na kulielewa kisha kusonga mbele, au tunaweza kuamua kulikuza jambo hilo na siku yetu nzima ikaharibika kwa jambo hilo.
 

Au inawezekana umeweka malengo na mipango yako vizuri, na ukaweka juhudi zote unazohitajika kuweka ili kufikia malengo hayo, lakini ukapata majibu ambayo hukutegemea kabisa kupata. Hili ni jambo dogo sana kwa sababu hakuna mtu aliyekuhakikishia kupata kile unachotaka, na hivyo unaweza kujifunza na kuboresha zaidi baadaye. Lakini wengi wamekuwa wanakuza hali kama hiyo, na kuanza kujikumbusha mambo mengine ambayo wamewahi kushindwa, pia anaweza kutafuta ni watu gani wamehusika kwa yeye kushindwa. Kwa njia hii mtu anakuza jambo hilo na kujikuta anapata msongo wa mawazo.
 

Mambo mengi yanayotokea kwenye maisha yetu na siku zetu ni mambo madogo, ambayo tunatakiwa kuyaelewa na kusonga mbele na maisha yetu. Lakini sisi wenyewe tumekuwa tunakazana kuyakuza kitu ambacho kinavuruga kabisa siku zetu.
 

Yaelewe mambo madogo.
Ili kuepuka mambo haya madogo kuharibu siku zetu, ni lazima tuwe na njia bora ya kuyajua mambo madogo na kutoruhusu mambo haya yaingilie siku zetu.
 

Kwenye jambo lolote linalotokea kwenye maisha yako, jiulize je jambo hilo litakuwa na maana miaka kumi ijayo? Au mitano, au hata mwaka mmoja ujao? Jiulize je jambo hilo linakuhusu wewe moja kwa moja, kama ni changamoto je umeisababisha wewe moja kwa moja? Na kama ni changamoto, je unaweza kuitatua wewe moja kwa moja? Kama jibu ni ndiyo itatue, kama huwezi kuitatua achana nayo.
 

Usiendelee kuumiza kichwa chako kwa mawazo ya kitu kilichotokea, tatua au achana nacho. Pia usijaribu kutafuta mahusiano ya kilichotokea wewe na mambo mengine yaliyowahi kutokea au na watu wengine. Jua kitu kimetokea na chukua hatua katika kutatua kilichotokea.
Jidhibiti wewe mwenyewe.
 

Haijalishi ni kitu gani kimetokea kwenye maisha yako, wewe mwenyewe ndiye mwenye nguvu ya mwisho, ya kuamua kama kitu hiko kinaharibu siku yako au la. Hata kama ni kitu kibaya kiasi gani kimetokea, bado wewe ndiye mwenye maamuzi. Na unaweza kutumia maamuzi haya kama unaweza kujidhibiti wewe mwenyewe.
 

Na sehemu muhimu ya kujidhibiti ni kwenye hisia. Hisia zina nguvu sana na mara nyingi hisia zinapokuwa juu uwezo wa kufikiri unakuwa chini. Hivyo dhibiti sana hisia zako. Hisia kama za hasira zinaweza kukusukuma kufanya mambo ambayo utayajutia hapo baadaye. Inapotokea mtu amefanya jambo au kuna jambo limetokea ambalo limekukasirisha, usichukue maamuzi ukiwa na hasira, badala yake tulia na rudi kwenye hali yako ya kawaida ndiyo uamue ni hatua gani utachukua.
 

Usikubali kabisa kufanya maamuzi kwa sababu ya hasira ulizonazo, au furaha uliyonayo, badala yake fanya maamuzi ukiwa umetulia na umefikiri kwa kina ni kitu gani unakwenda kufanya.
 

Mambo mengi yanayotokea kwenye maisha yako ni madogo, usiruhusu yaharibu siku yako au maisha yako. Ukiielewa vizuri falsafa hii kila siku utakuwa na maisha ya furaha na mafanikio. Kwa sababu kuweza tu kutulia na kudhibiti hasira zako ni mafanikio tosha kwa sababu utaweza kufanya maamuzi bora sana kwako.
 

Usikubali mambo madogo yavuruge mipango yako ya kuwa na siku bora. Endelea kufanyia kazi malengo na mipango yako ya siku, huku ukielewa kinachokutokea hakina nguvu ya kuharibu siku yako kama wewe mwenyewe hutatoa ruhusa hiyo.

0 comments: