Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu leo tunakwenda kuangalia njia ya uhakika ya kudhibiti Fikra zetu ili kuwa na uhuru na maisha yetu.
Kitu muhimu sana tunachotaka kwenye maisha yetu, ili tuweze kuyafurahia na tuweze kufanya yale yanayotupeleka kwenye mafanikio makubwa ni uhuru. Uhuru ndiyo hitaji la msingi la kila binadamu, lakini siyo wote tumeweza kuwa na uhuru. Pamoja na kwamba tunaishi kwenye nchi huru, lakini bado wengi maisha yao yamefungwa. Na vifungo hivi vinaanzia sehemu moja muhimu ambayo ni fikra zetu.
Hakuna kitu kina nguvu kwenye maisha yako kuzidi fikra zako. Kile unachofikiri kwa muda mrefu ndiyo kinachotokea kweny
e maisha yako. Fikra zako zina nguvu ya uumbaji, kila ambacho kimetokea kwenye maisha yako, kimeanzia kwenye fikra zako. Kila kitu unachofanya kinaanza na fikra, unakuwa na fikra ambazo zinakuwezesha kuleta kwenye uhalisia.
Haijalishi unapitia nini kwenye maisha yako, fikra zako zinaweza kubadili kabisa hali yoyote unayopitia. Kama ukiweza kudhibiti mawazo yako, unaweza kujijengea uhuru wa maisha yako na kuweza kuwa na maisha ya furaha na mafanikio.
Zifuatazo ni njia unazoweza kutumia kudhibiti fikra zako ili kuwa na uhuru wa maisha yako.
1. Jiamini kwamba unaweza.
Hatua ya kwanza ya kudhibiti fikra zako ni kuamini ya kwamba unaweza kuleta mabadiliko kwenye maisha yako. Amini una uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. bila ya kujali hali yoyote unayopitia, jiamini kwamba unaweza kuondoka kwenye hali hiyo na kuwa na maisha bora zaidi. Amini kwamba unaweza kuwa bora zaidi ya hapo ulipo sasa, na chochote unachotaka unaweza kukifikia kama utaweka juhudi.
2. Epuka kukaribisha mawazo hasi.
Mawazo hasi yana tabia moja, yanaanza kidogo kidogo na yanakaribisha mawazo mengine hasi na baada ya muda unaona kila kitu hakiwezekani. Ili kuepuka hali hiyo zuia mawazo hasi, pale ambapo unaona mawazo hasi yanaanza kukujia kuhusu hali yoyote, fikiria upande chanya wa hali hiyo. Unapofikiria upande chanya unaweza kuona mambo yanawezekana kuliko unapofikiria upande hasi. Kumbuka haya yote yanaanzia kwenye mawazo yako na mara zote mambo huwa siyo mabaya kama ambavyo tunafikiri yatakuwa.
Jua wakati ambapo mawazo hasi yanaanza kuingia kwenye fikra zako na ondokana nayo, kwa kuangalia upande chanya wa jambo au uwezo wako mwenyewe.
3. Acha kujumuisha mambo.
Kama kuna hali mbaya imetokea kwenye maisha yako, au kama umewahi kupitia magumu kwenye maisha yako, haimaanishi kwamba wewe ni mtu w akupitia magumu wakati zote.
Au wewe ndiyo mwenye kisirani kuliko wengine wote. Hii ni tabia ya kujumuisha mambo ambayo inawafanya watu kuchukulia hali moja mbaya inamaanisha maisha yao yote ni mabaya. Haijalishi unapitia nini leo, kesho yako bado inaweza kuwa bora kuliko leo. jua ya kwamba hakuna kinachotokea, au kilichotokea ambacho kimezuia fursa zako za mbele, ni mpaka pale utakapoamua mwenyewe.
Usikubali mawazo yako yatumie kilichotokea kuharibu maisha yako ya kesho, jua kwamba una nafasi ya kuwa na maisha bora wakati wowote licha ya kujali umepitia nini kwenye maisha.
4. Acha kuchukulia vitu kwa ubinafsi.
Chochote kinachotokea kwenye maisha yako, ni lazima uweze kukitofautisha na wewe binafsi. Mara nyingi watu wamekuwa wakichukulia matukio yanayotokea na kuyafanya kuwa wao binafsi. Hapa mtu anaposhindwa kitu anachukulia kwamba ameshindwa kwa sababu yeye hafai. Au mtu anapomkatalia kitu, anachukulia kwamba amemkataa yeye kwa sababu hafai. Chochote kinachotokea kwenye maisha yako hakitokei kwa sababu yako wewe, bali kinatokea kama sehemu ya maisha. Kushindwa hakumaanishi kwamba wewe hufai, na hata mtu anapokataa kile unachomwambia haimaanishi kwamba amekukataa wewe, au ameona wewe hufai.
Elewa kwamba wewe ni wewe na matukio yanayotokea ni matukio, utabaki kuwa wewe kama utaweza kudhibiti mawazo yako.
5. Acha kukimbilia kuhukumu.
Binadamu tuna tabia moja, kwa jambo lolote ambalo linatokea, huwa tunatafuta sababu ya kulielezea na haijalishi kama sababu hiyo ni halisi au siyo, huwa tunakimbilia kuhukumu.
Kwa kukimbilia kuhukumu tunakosa fursa nzuri ya kufikiri kwa kina na kujifunza zaidi kwenye kile ambacho kimetokea. Tunapohukumu tunachukulia kile ambacho tumeona au kusikia bila ya kuchimba kwa undani na mara nyingi tunakuwa tunakosea.
Ili kudhibiti mawazo yako acha kuhukumu, chochote kinachotokea kuwa na fikra huru ili kujifunza zaidi na kuona ni nini hasa kimesababisha. Kwa njia hii utaona ukweli na kuweza kuchukua hatua bora.
Bila ya kudhibiti mawazo yako yanaweza kukufanya uone maisha ni magumu na hatari sana. Yanaweza kukufanya ukate tamaa na ushindwe kuchukua hatua kwenye mambo ambayo ni muhimu kwako na hivyo kuishi maisha yanayokosa uhuru. Kwa kukosa maisha ya uhuru huwezi kuyafurahia maisha na hayawezi kuwa bora. Nunua uhuru wako kwa kuanza kudhibiti fikra zako.
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea uhuru wako kwa kudhibiti mawazo yako.
Makirita Amani
0 comments:
Chapisha Maoni