Habari za leo mwanafalsafa ya maisha?
Ni matumaini yangu unaendelea vyema sana, huku ukijijenga falsafa mpya na bora sana ya maisha yako. Naendelea kukukumbusha kwamba unahitaji kujenga falsafa mpya ya maisha yako kwa sababu maisha uliyopokea kwenye jamii hayana falsafa. Watu wanaishi kama wanavyowaona wengine wakiishi na hili limeleta changamoto kubwa kwa jamii nzima.
Tunazungumzia sana furaha kwa sababu huu ndio msingi wa maisha yetu, bila ya furaha maisha yanakuwa magumu sana na hatuwezi kufikia kile ambacho tunakitaka. Na hapa kwenye furaha ndipo penye changamoto nyingi sana, kwa sababu kwa kiasi kikubwa hatuielewi furaha ya kweli tunawezaje kuipata.
Tulishajifunza kupitia falsafa hii mpya ya maisha ya kwamba furaha haitokani na vitu, hakuna kitu au mtu yeyote anayeweza kukuletea
wewe furaha, bali furaha inaanzia ndani yako mwenyewe. Unapaswa kuwa na furaha hapo ulipo sasa kwa jinsi ulivyo, hakuna kitu chochote cha ziada unachohitaji ndio uweze kuwa na furaha.
Lakini hili nalo limekuwa na changamoto, sawa una furaha kwa vile ulivyo, lakini hapo kunakuja kitu kimoja, haturidhishi na vile tulivyo navyo.
Unakuta mtu umeweka malengo kwamba unahitaji kufikia kitu fulani, au kupata kitu fulani, unaweka juhudi na kweli unakipata. Na unapokipata ni lazima utakuwa na furaha, kwamba umeweka juhudi na umefikia kile ulichotaka. Lakini baada ya muda unazoea kitu kile au hali ile, na kuanza kuona unahitaji kupata zaidi ya pale.
Labda lengo lako lilikuwa kujenga nyumba, ukaweka juhudi na ukafanikiwa kukamilisha nyumba yako, ukafurahi sana. Lakini baada ya hapo unaanza kuona nyumba yako haijakaa kisasa kama za wengine, au ni ndogo sana au kuna vitu fulani vinakosekana.
Hapo sasa furaha yako inaisha na unaanza kuangalia zaidi kile ambacho kinakosekana.
Kwa kifupi tunaweka juhudi kupata kitu, na tunapopata tunafurahia, lakini baada ya hapo tunaanza kukizoea, na kuona hakitoshi tena tunahitaji kupata zaidi, na hapo furaha yetu inapotea.
Changamoto kubwa ni kwamba binadamu haturidhiki, na hii siyo mbaya, ila ubaya ni pale kutokuridhika kwenye kunaingilia furaha yetu, kwani kwa njia hii tunajikuta tunaishi maisha kama ya utumwa. Inatufanya tuone kile ambacho tunacho sasa hakina thamani na hivyo kuona kama maisha yetu hatujaweza kufanikisha mambo makubwa.
Ni vizuri kutaka kupata kilicho bora zaidi, lakini hili halimaanishi kwamba kile ambacho umepata sasa hakina maana, kina maana kubwa sana na unahitaji kuiheshimu.
Je unawezaje kuondokana na hali hii inayokuondolea furaha?
Njia bora kabisa ya kuondokana na hali hii ni kujipa taswira kwamba kile ulichonacho kimeondoka kabisa kwenye maisha yako. Na kuona je maisha yako yatakuwaje.
Kama ni nyumba umeiona haikufai tena, fikiria nyumba hiyo imeungua moto, ukiwa bado hujapata nyumba nyingine, fikiria ni kwa jinsi gani utakavyosumbuka. Kama ni gari umekuwa unaiona ya kawaida, pata taswira kwamba hunayo tena, labda umeibiwa au imeungua moto na hutaipata tena, ni kwa jinsi gani utasumbuka.
Hata kama ni watu vile vile jipe taswira hii, kwamba watu hawa ambao umeshazoea kuwaona kila siku na kuona wapo tu, pata taswira kwamba wameondolewa kwenye maisha yako moja kwa moja. Labda wamesafiri kwenda nchi za mbali au wamefariki dunia, ni kwa kiasi gani utakuwa umewakosa?
Ni nini faida ya kufanya zoezi hili?
Unapofanya zoezi la kujipa taswira ya kukosa kile ambacho unacho siyo kujijengea mtizamo hasi ambao unaleta hofu ya kukosa, badala yake unajijengea mtizamo wa shukrani kwa kile ambacho tayari unacho.
Zoezi hili linatukumbusha ya kwamba hivi vitu ambavyo tunaviona vya kawaida kwa sasa vina thamani kubwa sana kwetu. Tunaviona vya kawaida kwa sababu tunaona vipo na vitaendelea kuwepo, ila vitakapoondoka kwenye maisha yetu ndiyo tutaona pengo kubwa linaloachwa na kuondoka kwa vitu hivi.
Kwa kujikumbusha umuhimu huu wa vitu kabla havijaondoka tutaweza kurudisha furaha yetu na thamani kwa vitu hivyo. Tutaanza kuona kwamba hata kama kuna vitu ambavyo tumekosa, lakini bado maisha yetu siyo ya hovyo kabisa kwa sababu kuna hivi ambavyo tumeweza kuvifanikisha au tuna watu ambao wanatujali bila ya kuangalia tuna nini au tumefanya nini.
Na kwa kuona thamani hii ya vitu ambavyo tayari unavyo, inakupa hamasa ya kuweka juhudi zaidi ili kupata vilivyo bora zaidi. Kwa kuthamini ulichonacho kunakufanya uone umuhimu wa kukiboresha zaidi na akili yako inakuonesha fursa bora zaidi za kupata kilicho bora.
Tunachohitaji kufanya ni kuvipenda vile ambavyo tayari tumeshakuwa navyo, vile ambavyo tayari tumeshavizoea. Kwa sababu tumekuwa tunajidanganya ya kwamba vitu hivi vipo na sisi milele, lakini huo sio ukweli. Kuna wakati utakuwa na kitu mara ya mwisho, kuna wakati utakula chakula fulani mara ya mwisho, kuna wakati utakutana na mtu kwa mara ya mwisho, na kuna wakati utakuwa na kile unachokipenda kwa mara ya mwisho.
Usichukulie kitu chochote kile kwa mazoea, ni adui wa furaha yako.
Thamini kile ambacho unacho sasa, hata kama bado unahitaji zaidi. Hii itakuwezesha kuthamini maisha yako na kukuletea furaha. Ni furaha hiyo ndiyo itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa zaidi duniani.
Endelea kujijengea falsafa ya maisha ili uweze kuishi maisha bora, ya furaha na yenye mafanikio. Ni wewe mwenyewe ndiye wa kuamua hayo, na unaweza kuamua sasa kwa kuchagua ni maisha yapi unataka kuishi. Kama unataka kuishi kwa mazoea kama wengine, au kama unataka kuishi kwa misingi ambayo inatokana na sheria za asili ambazo haziyumbi kamwe.
0 comments:
Chapisha Maoni